
Huu ni uchunguzi wa kipekee wa RFI kuhusu vita vya siri vinavyoendelea katika bara la Afrika, kati ya Kyiv na Moscow nchini Libya. Vita hivi vinafanyika kwa siri na vikijikita kwenye maslahi ya kiuchumi na kijeshi, pamoja na mapambano ya madaraka, ya Urusi na Ukraine, nchi mbili ambazo ziko vitani kwa zaidi ya miaka minne. Sehemu ya mwisho ya awamu tatu: Je, Afrika imekuwa ukumbi mwingine wa vita kati ya Urusi na Ukraine?
Imechapishwa:
Dakika 4 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kwa kukiri uwepo wa wanajeshi wa Ukraine magharibi mwa Libya, je, serikali ya Abdel Hamid Dbeibah inatafuta kukabiliana na athari za uwepo wa mamluki wa Urusi katika kambi ya mashariki mwa Libya, inayoongozwa na Marshal Khalifa Haftar?
Vikosi vya kwanza vya Urusi vilikuwepo Libya mwaka wa 2016. Tripoli pia inatafuta kuweka usawa wa madaraka na mamlaka mashariki, katika nchi hii iliyogawanyika ambapo pande mbili zinapambana kwa ajili ya madaraka.
Ushirikiano wa kijeshi, mafunzo, na mauzo ya silaha, pamoja na uwekezaji katika sekta ya mafuta, ni sehemu ya makubaliano haya kati ya Kyiv na Tripoli, kulingana na vyanzo vyetu vya Libya.
Mada yeti
Hata hivyo, Urusi na Ukraine zinaitumia Libya kama kikwazo cha uwepo wao kwingineko barani Afrika.
Hivi majuzi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi ilimshutu Waziri Mkuu wa Libya na Ukraine kwa kuunga mkono makundi yenye silaha huko Sahel, kwa usaidizi wa moja kwa moja wa idara ya ujasusi ya Uingereza.
Chanzo cha kidiplomasia cha Afrika kimeripoti kwa RFI kauli ambayo kinasema kilipokea kutoka kwa afisa wa Azawad Liberation Front (ALF), kundi lenye silaha lililopo Mali: “Tuliwatuma vijana kwenda Ukraine kufundishwa mbinu za uendeshaji wa ndege zisizo na rubani.” “
Upanuzi wa maeneo ya migogoro nchini Libya na kwingineko barani Afrika unaonyesha nia ya wazi ya Ukraine ya kukabiliana na Urusi, ambayo imekuwa imara barani Afrika kwa miaka kadhaa, kijeshi na kiuchumi.
Sahel
Msimu uliopita wa vuli, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi Maria Zakharova alisema kwamba mamlaka ya Ukraine ilikuwa ikitoa silaha na kuwafunza “magaidi barani Afrika, haswa nchini Mali.” Katika mwezi huo huo, Vasily Nebenzia, mwakilishi wa Urusi kwa Umoja wa Mataifa, alidai kwamba “mamlaka ya Ukraine inawaunga mkono magaidi, haswa katika Sahel.”
Kwa upande wake, Ukraine ilikiri baadaye kwamba ilitoa usaidizi wa kijasusi baada ya FLA kuchukuwa udhibiti maeneo kutoka mikononi mwa jeshi la Mali na wawakilishi wake wa Urusi mnamo Julai 2024 huko Tinzaouaténe. Kulingana na Gazeti la Le Monde, huu ulikuwa “msaada wa busara lakini wa uamuzi kutoka Kyiv,” ambao unaonyesha kwamba matumizi ya ndege hizi zisizo na rubani “sio fumbo tena.”
Mwanzoni mwa mwezi Agosti 2024, Mali ilikata uhusiano wa kidiplomasia na Kyiv, ikiishutumu Ukraine kwa kuchukua jukumu muhimu katika kushindwa kwa jeshi la Mali kaskazini mwa nchi.
Pia upande wa kijeshi, lakini zaidi magharibi mwa Afrika, mnamo Novemba 27, 2025, shambulio lililenga meli ya mafuta iliyokuwa imetia nanga kilomita 19 kutoka pwani ya Senegal katika Bahari ya Atlantiki. Meli hii, Mersin, iliondoka Taman, bandari iliyoko karibu na Mlango-Bahari wa Kerch, ambao hutenganisha Urusi bara na Crimea. Meli hii inayomilikiwa na kamuni ya usafiri ya Uturuki ya Besiktas Shipping, iliharibiwa vibaya.
Miongoni mwa dhana zilizochunguzwa na mamlaka ya Senegal ni shambulio lililopangwa na Ukraine. Leo, wataalamu wa kijeshi wanabanisha kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba ilikuwa ndege isiyo na rubani ya Ukraine na sio vilipuzi vilivyowekwa kwa mkono.
“Ushirikiano maalum” Je, Sudani ni mfano mwingine wa vita hivi vya siri vya Urusi na Ukraine barani Afrika? Kwa vyovyote vile, mwezi Oktoba mwaka uliyopita, jeshi la Sudan lilitangaza vifo vya mamluki kadhaa wa Ukraine wanaopigana katika safu ya wanajeshi wa Vikosi vya msaada wa Haraka (RSF) huko Darfur, bila kutoa maelezo zaidi. Hii iliwasilishwa na Moscow kama “uthibitisho zaidi wa kuhusika kwa Kyiv” katika migogoro barani humo. Ikumbukwe kwamba mamluki wa Urusi pia wanashiriki katika vita nchini Sudan.
Wiki iliyopita, shirika la habari la Kiarabu la Ukraine liliripoti kwamba Kyiv ilikuwa ikitafuta kuendeleza mkakati wa kuimarisha uwepo wake barani Afrika na kupanua ushirikiano na nchi hizi. Kulingana na tovuti hii maalum ya serikali, mkutano ulioongozwa na Kyrylo Budanov, mkuu wa utawala wa rais wa Ukraine, ulifanyika kwa lengo hili. Maafisa kadhaa wa kidiplomasia na ujasusi wa ngazi ya juu walishiriki, pamoja na wataalamu wa Afrika. Mkutano huu ulibainisha nchi zilizopewa kipaumbele kwa kuongeza “ushirikiano huu maalum,” katika Afrika Kaskazini na Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Katika Afrika, ushindani huu wa kimkakati kati ya Urusi na Ukraine ni sehemu ya ushindani unaoendelea kati ya Moscow na washirika wa Kyiv wa Magharibi, ambao, mwanzoni mwa vita mwaka wa 2022, walizihimiza nchi za Afrika kuunga mkono Ukraine.