Zanzibar. Ukifika Zanzibar, ukiacha vivutio vya utalii kama fukwe za bahari na mitaa ya kihistoria ya Stone Town, kuna jina moja ambalo ukiyakanyaga maeneo ya Makadara hata mtoto mdogo anakuelekeza.

Huyo si mwingine, bali ni Mwanahawa Ally, malkia wa muziki wa taarabu aliyetikisa Afrika Mashariki kwa miongo kibao. Mwananchi ilifunga safari kutoka Dar es Salaam hadi Unguja kufanya mahojiano na mwanamama huyo ambaye amefunguka mengi ikiwemo maisha yake ya sasa baada ya kutangaza kustaafu lakini bado anaonekana kuendelea kufanya shoo. Endelea kusoma utafahamu zaidi.

Chimbuko lake

Mwanahawa Ally si mzaliwa wa Zanzibar kwa asilimia mia moja kulingana na chimbuko la wazazi wake, baba yake alitokea Mtwara, Tanzania Bara na kutua Zanzibar ambako alikutana na mama yake na kufanikiwa kupata watoto watano, Mwanahawa akiwa kitinda mimba.

“Nimelelewa na wazee wa kizamani. Wanaume wa zamani walikuwa hawapendi mtoto wa kike kwenda shule,” amesimulia Mwanahawa

Badala yake, alielekezwa zaidi kusoma Madrasa, ambako kuimba kwake kaswida kulianza kuijenga sauti yake ya dhahabu ambayo leo inafahamika kote. Safari yake ya muziki ilianzia jikoni na kwenye shughuli za kufua nguo. 

“Mimi sikujua kama nina kipaji, Nilikuwa nikikaa napenda sana kuimbaimba kama niko jikoni nafua, nafanya nini, naigiza wale niliokuwa ninawaona matawini”.

Mwaka 1966 ndipo aliingia rasmi kwenye  Taarab, akivutiwa na vikundi vya kizamani vilivyokuwa vikiimba kwenye matawi ya vyama.

Alianzia kikundi cha Culture (Kino Culture) mwaka 1964 ndicho kilichompa jina kubwa na kumfanya arekodi wimbo wake wa kwanza redioni uliokuwa unahusu siasa na mapinduzi, kabla ya kuingia kwenye nyimbo za mapenzi.

Wimbo wake wa kwanza kurekodiwa uliitwa “Maisha ya Vijijini”, wimbo wa kisiasa uliotungwa baada ya Mapinduzi ya Zanzibar uliokuwa unaelezea uhalisia wa maisha ya wakati huo.

Tangu hapo, Mwanahawa amepita katika makundi mengi makubwa ikiwemo Angufafa (1980), East African Melody (1995), Jahazi Modern Taarab, na Zanzibar Stars.

Amesema muziki wa zamani haukuwa unalipa lakini kidogo alichokuwa anapata kwenye shughuli zake alijiwekeza taratibu hadi kujenga nyumba ambayo anaishi hadi sasa.

“Sisi zamani tulikuwa tunaimba kama upenzi sio ajira,” amesema akielezea tofauti ya zamani na sasa ambapo wasanii wanategemea mikataba mikubwa na mauzo ya mitandaoni.

Kwake, utajiri ulitokana na ‘tunza’ za jukwaani. Pesa hizo ndizo zilizomsaidia kujenga nyumba yake kidogo kidogo

“Nikiokota huko saa mbili nikiamka nanunua tofari, nanunua mchanga mpaka imekuwa hivi,”amesema

Anasema nje ya kujenga nyumba mafanikio yake makubwa ameweza  kusomesha watoto, wajukuu, na sasa vitukuu (virembwe) ambao wote wanasoma kupitia kazi yake ya kuimba.

“Sina kazi nyingine zaidi ya kuimba na hivyo hii kuimba nilifanikiwa kusomesha watoto, wajukuu na sasa virembwe jambo ambalo nashukuru japo sio kubwa,”amesema

Bifu za Taarab

Mkongwe huyu amekiri kuwa muziki wa Taarab una mambo mengi ya nyuma ya pazia, hasa bifu za wanawake na muda mwingine zinavuka mipaka.

Anakumbuka tukio moja la kusikitisha ambalo lilimtoa machozi mama yake. “Nishafanyiwa mambo ya kiswahili sifichi. Nimelala mzima, asubuhi naamka nina majipu kichwani, mdomo jipu linaning’inia,” anasimulia kwa uchungu.

Mama yake alilia akisema, “Mwanangu, huo ndio mdomo unaoimbia leo upo hivo?”.

Mbali na hayo, Mwanahawa aliwahi kukutana na changamoto ya kuchukiwa na hadi kutaka kupigwa ili asipafomu vizuri jukwaani.

Anakumbuka safari moja ya kikundi cha Culture ambapo mmoja alimtukania mama yake kwa mpango uliosukwa ili kumvunja moyo.

“Unajua mambo ya wanawake tulikuwa sijui Mtwara kama nakumbuka basi nilichaguliwa kupafomu kumbe wenzangu hawakufurahia hilo wakapanga njama ya kutaka kunipiga kunitukana ili nikipigana nao nifukuzwe sijui ikawaje mmoja wao akaja kuniambia mpango wao kwahiyo walivyokuja nikawapotezea.”

Anaendelea kuimba 

Ingawa miaka miwili iliyopita Mwanahawa alitangaza kuacha kuimba kutokana na umri na matatizo ya kiafya, bado anaonekana kwenye baadhi ya matamasha na sehemu mbalimbali akiimba.

“Siimbi kwa Raha, natafuta tonge ili mkono uingie kinywani kwa sasa, uzee na maradhi ya miguu lakini uwezo wa kusimama dakika chache kuimba ninao kwahiyo unaponiona napanda steji, sifanyi kwa raha, nafanya kwa shida.”

Anaeleza kuwa hawezi kuacha muziki kabisa kwa sababu bado ana majukumu ya familia na pesa anayopata inamsaidia kuendesha maisha.

“Watu wanakuja hapa Mwanahawa njoo utuimbe njoo sasa mimi muda mwingine nakuwa nachoka lakini naenda kwa sababu kwanza nahitaji pesa, hata nikimba nyimbo mbili tu wao wameridhika.”

Anasema amekuwa akipata simu nyingi za kuimba nje ya mikoa na Dar.”Kusema ukweli naweza nisipumzike kwa sababu watu ni wengi wananipigia simu tena Zanzibar ni asilimia chache lakini Dar ni wengi sana kwa hiyo tunawasiliana wanatuma pesa ya usafiri hadi huko kisha nakwenda.”

Milioni moja

Anasema shoo anazopiga pesa kubwa ni Sh1 Milioni ambazo mara nyingi anapewa na watu wengi kutoka Dar pesa ambayo anakiri imekuwa ikimsaidia kwa kiasi kikubwa.

“Huwa tunaelewana wakinipigia nataja dau langu na wao wanasema wana kiasi gani lakini kwa Dar pesa nyingi ni Milioni moja nawaimbia kwenye mashughuli yao ya matamasha kisha naondoka.”

Hizi pendwa

Anasema kwenye matamasha na shughuli nyingi anazoalikwa nyimbo zake mbili zimekuwa zikipendwa na watu ‘Rabini Linde’ na ‘Umaskini Wangu’.

Wimbo wa ‘Umaskini Wangu’ anasema umekuwa kama wimbo wa taifa kwenye harusi, na ndio unaompa pesa  nyingi ‘kutuzwa’ zaidi hadi leo.

“Sijajua kwanini mfano hapa Zanzibar nikiimba utasikia mtu na mimi nikiwa na shughuli yangu nitakualika uniimbie wimbo huo na kweli, wanaona bora niimbe nyimbo hizo mbili tu kuliko kuimba nyimbo nyingi.”

Yanga kindakindaki

Kama ilivyo kwa mashabiki wengi wa zamani, Mwanahawa Ally ni shabiki lialia wa klabu ya Yanga. Mapenzi yake kwa timu hiyo hayakuanza hivi karibuni, tangu enzi za kina Fatuma Karume.

“Mimi mshabiki wa Yanga sirudi nyuma. Kindakindaki kama kauli yao, ‘Nyuma Mwiko’,” anasema kwa mbwembwe.

Anakumbuka machungu ya kufungwa goli 6-0 na mahasimu wao Simba miaka ya nyuma, tukio ambalo lilimfanya atake kulia akiwa hotelini Dar es Salaam.

“Siku hiyo nakumbuka tulikuwa na tamasha sasa sikuwa na Amani nasikia mara la tatu la nne hadi sita roho iliniuma sana na sikuwa na siku nzuri stejini.”

Mwanahawa amempa sifa  Rais wa sasa wa Yanga, Hersi Said. “Namkubali sana na namwombea Mungu awe na moyo huohuo wa kuendeleza asirudi nyuma. Nikimuona jukwaani kakaa, najua huyu kiongozi mahiri”.

Anamkubali Pakome

“Hapa kwangu siku inayocheza Yanga sitaki mtu afanye mchezo… lazima niangalie na wanajua wanakaa pembeni hadi mechi inapomalizika”.

Mchezaji anayemkubali zaidi kwa sasa ni Pacome Zouzoua kutokana na kiwango bora anachoonyesha kiungo mshambuliaji huyo raia wa Ivory Coast.

Ushauri kwa vijana 

Mwanahawa anasema sio kwamba muziki wa taarabu umepotea bali vijana wanapotea kutokana na kutokuwa tayari kuelekezwa na wale waliowatangulia.

“Sisi tulikubali kufunzwa na kukosolewa, lakini waimbaji wa sasa hivi ukimkosoa anaona kama ushamtukana”.

Anasisitiza kuwa yeye hana roho mbaya na yuko tayari kumfundisha kijana yeyote anayehitaji msaada wake ili kukuza kipaji chake.

Mbali na hilo Mwanahawa Ally anahitimisha kwa kusema kuwa maisha ya sanaa yanahitaji uvumilivu na moyo wa kike. Licha ya changamoto zote, bado anaimba.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *