Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeendelea kudumisha utaratibu wa kuwaenzi waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwaombea dua kila mwaka, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao katika kupigania uhuru, haki na umoja wa kitaifa.

Utaratibu huo hufanyika kuanzia Aprili Mosi hadi 7 kila mwaka, siku ya kumbukizi ya kifo cha Rais wa kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amani Karume, ambaye alifariki dunia mwaka 1972. Wiki hiyo hutumika kama kipindi maalum cha kutafakari historia ya mapinduzi na mchango wa viongozi waliotangulia mbele ya haki.

Akizungumza wakati wa shughuli za kuwaenzi waasisi hao, Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, amesema viongozi hao walifanya mapinduzi makubwa yaliyowezesha kupatikana kwa maendeleo, amani na mshikamano uliopo Zanzibar leo.

Shariff ameyasema hayo alipotembelea na kushiriki dua katika makaburi ya aliyekuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi mstaafu, marehemu Khamis Darwesh Mdingo, pamoja na Kanal mstaafu Seif Bakari Omar, maarufu Kiembe Samaki, katika Wilaya ya Magharibi B.

Amesema waasisi hao walijitoa kwa hali na mali kuhakikisha wanajenga taifa lenye mshikamano na utulivu, na kwamba ni wajibu wa Serikali kuendeleza misingi hiyo kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

“Tunapaswa kuwashukuru na kuwaenzi wazee wetu hawa kwa mchango wao mkubwa. Mwenyezi Mungu awalipe kwa mema yote waliyotenda kwa ajili ya nchi yetu,” amesema Shariff.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuitunza historia ya Mapinduzi ili iwe rejea kwa vizazi vijavyo kujifunza na kuelewa safari ya taifa lao.

Kwa upande wake, Asya Khamis Darwesh, mtoto wa marehemu Khamis Darwesh, amesema familia yao imeendelea kufuata mafunzo ya baba yao aliyesisitiza umoja na ushirikiano. Aliiomba Serikali kuendelea kulinda tunu hizo ili kudumisha amani iliyopo nchini.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Juma Malik Akili, ameshiriki dua ya kumuombea marehemu Abdallah Said Natepe iliyofanyika nyumbani kwake Mwachealale, Wilaya ya Magharibi A.

Katika dua hiyo, Dk Akili amesema viongozi hao walijitoa kikamilifu katika harakati za ukombozi, na hivyo ni vyema kuendelea kuwaombea ili wapate rehema na thawabu mbele ya Mwenyezi Mungu.

Amewashukuru wanafamilia wa marehemu kwa kuridhia kuendelezwa kwa utaratibu huo wa kila mwaka, akibainisha kuwa ushirikiano wao ni msingi wa kudumisha kumbukizi hizo muhimu za kitaifa.

Akiongoza dua hiyo, Sheikh Shariff Abdul-Rahman kutoka Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar amesema kuwa ibada hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa jitihada za Serikali katika kuwaenzi viongozi waliolitumikia taifa kwa uadilifu.

Naye Ali Abdallah Said, mtoto wa marehemu Natepe, amesema wamejifunza mengi kutoka kwa baba yao, hususan kuhusu umuhimu wa mshikamano na maadili mema katika jamii. Alisema familia yao imefarijika na utaratibu huo wa Serikali unaowakumbuka wapendwa wao.

Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Nadir Abdullatif, ameeleza kuwa viongozi wa sasa wanaendelea kujifunza misingi ya nidhamu, uwajibikaji na uadilifu kutoka kwa waasisi hao. Alitoa kauli hiyo aliposhiriki dua ya kumuombea marehemu Luteni Kanali mstaafu Said Iddi Bavuai katika eneo la Shakani, Wilaya ya Magharibi B.

Amesema licha ya kupita kwao, mchango wa viongozi hao unaendelea kuwa dira katika uongozi wa nchi, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuthamini jitihada zao.

Kwa upande wao, wanafamilia wa marehemu walishukuru Serikali kwa kuanzisha utaratibu huo wa kuwaombea dua, wakieleza kuwa unawapa faraja na kuthibitisha kuwa mchango wa wapendwa wao unatambuliwa na kuthaminiwa.

Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Mudrik Ramadhan Soraga, amesema Serikali imeweka utaratibu huo ili kuenzi, kuwafariji wanafamilia na kuwaombea rehema viongozi waliotangulia mbele ya haki.

Akizungumza katika kijiji cha Mndo, Wilaya ya Magharibi A, wakati wa dua ya kumuombea marehemu Said wa Shoto, Soraga amesema marehemu huyo alikuwa mstari wa mbele kupigania haki na kupambana na dhuluma, hivyo ni muhimu kuendelea kumkumbuka kwa mchango wake.

“Ili kuthamini viongozi wetu, ni lazima tuwarithishe vizazi vyetu historia na maadili yao,” amesema Soraga.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na familia za waasisi wa Mapinduzi kwa kuhakikisha kumbukizi zao zinaenziwa ipasavyo.

Naye Mfaume Said wa Shoto, mtoto wa marehemu, amesema familia imefarijika na hatua hiyo, akieleza kuwa juhudi za baba yao zimezaa matunda ambayo yanaendelea kunufaisha jamii ya Wazanzibari hadi leo.

Kwa ujumla, wiki ya kumbukizi ya waasisi wa Mapinduzi imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kutafakari historia ya Zanzibar, kuenzi mchango wa viongozi waliotangulia na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *