MAAFANDE wa Mashujaa wameshindwa kutamba Kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini, Kigoma, baada ya kulazimishwa suluhu (0-0), dhidi ya kikosi cha Pamba Jiji, ‘TP Lindanda’ au ‘Wanakawekamo’, katika mechi kali na ya kusisimua ya Ligi Kuu.

Katika mechi hiyo, mashujaa imeshindwa kulipa kisasi kwa wapinzani wao, baada ya pambano la raundi ya kwanza la Ligi Kuu Bara lililopigwa Kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini, Mwanza, mwenyeji, Pamba Jiji kushinda mabao 2-1, Oktoba 17, 2025.

Mechi hiyo ya raundi ya kwanza iliyokuwa ya vuta nikuvute, mabao ya Pamba yalifungwa yote na Peter Lwasa dakika ya 16 na 64, huku kwa upande wa bao la kufutia machozi la kikosi hicho cha maafande likifungwa na, Baraka Mtuwi, dakika ya 45.

Licha ya timu hizo kutengeneza mashambulizi mengi ya kufunga, ila safu za ushambuliaji zilishindwa kutumia vyema nafasi hiyo, hivyo, kusababisha miamba hiyo kushindwa kutambiana na kulazimishina suluhu ambayo ni faida zaidi kwa Pamba Jiji.

Matokeo ya leo yanakuwa na faida zaidi kwa Pamba, kwani mara ya mwisho ilipotembelea Kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, ilichapwa mabao 2-0, Februari 19, 2025, yaliyofungwa na Hassan Hadji ‘Cheda’ dakika ya 35 na David Ulomi, dakika ya 83.

Mechi hii ni ya 18, kwa Mashujaa FC, ambapo imeshinda nne, sare nane na kupoteza sita, ikiwa nafasi ya 11 na pointi 20, huku kwa upande wa Pamba ikishinda sita, sare nane na kupoteza mitatu kati ya 17, ikishika nafasi ya tano na pointi 26.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *