NDANI ya klabu kubwa kama Yanga, maisha ya mchezaji yanazunguka zaidi ya dakika 90 za uwanjani. Ni maisha yanayohitaji nidhamu, uvumilivu, ushindani wa hali ya juu na uwezo wa kukabiliana na presha kutoka kwa mashabiki, viongozi na hata nafsi yako mwenyewe. Hapa ndipo tofauti ya mchezaji wa kawaida na mchezaji anayejitambua huonekana.

Kupitia mahojiano ambayo Mwanaspoti imeyafanya na kipa namba mbili wa Yanga, Abdultwalib Mshery, anaelezea kwa undani fikra, mtazamo na malengo ya mchezaji anayepambana kujijenga ndani ya mazingira ya ushindani mkubwa. Pia anagusia tukio la ubingwa wa Mapinduzi lililomtoa machozi.

Huku akiweka wazi namna ushindani wa namba uliopo kati yake na kipa wa timu ya Taifa ya Mali, Djigui Diarra, unavyozidi kumsogeza kufikia malengo makubwa aliyojiwekea, huku akisisitiza kwamba muda ndio unaamua kila kitu.

DIARRA SIO KIKWAZO

Anasema haamini kuwa uwepo wa Diarra unamzuia kufikia mafanikio yake, bali anaona kila kitu kina muda wake. Anaeleza kuwa ana imani na uwezo wake na anaamini kuwa ataendelea kupata nafasi zote anazozihitaji kwa wakati sahihi. Anasema hana haraka kwani anaelewa mafanikio huja kwa hatua na uvumilivu.

“Sio kweli kwamba uwepo wa Diarra ndio umenipotezea nafasi katika timu ya Taifa, nadhani muda ukifika nitaenda tena wala sio shida. Hata Yanga pia muda ukifika nitacheza na nafasi yangu timu ya Taifa bado ipo sana, na sina haraka; najua ni masuala ya muda na ninaamini kwenye uwezo wangu,” anasema Mshery.

MAISHA NDANI YANGA

Kipa huyo anasema maisha ndani ya Yanga yako katika mazingira mazuri yanayowapa nafasi ya kufanya kazi kwa utulivu na kuelekeza nguvu zao kwenye kufikia malengo ya timu.

Anaeleza kuwa kila mchezaji anatambua wajibu wake na umuhimu wa kushirikiana ili kuhakikisha klabu inapata mafanikio. Ukubwa wa Yanga unaleta matarajio makubwa, hivyo kila mmoja analazimika kujituma zaidi ili kuendana na hadhi ya klabu hiyo. “Maisha ndani ya Yanga yako poa, tunapambania timu yetu iweze kufikia malengo. Kama unavyojua hii ni klabu kubwa, lazima mahitaji yake yawe vivyo hivyo,” anasema.

KAZI WALIYONAYO

Mshery anasema msimu huu wanakabiliwa na ushindani mkubwa kwa sababu timu zote zimeimarika na hakuna mechi rahisi tena. Anaeleza kuwa wapinzani wamepiga hatua kubwa na sasa wana uwezo wa kushindana na timu kubwa, jambo linaloifanya ligi kuwa ngumu zaidi.

Anasema hali hiyo inaongeza thamani ya ubingwa kwani hautapatikana kirahisi bali kwa juhudi kubwa na umakini wa hali ya juu.

“Kama wachezaji wa kila maeneo msimu huu tuna kazi kubwa ya kufanya, kwa sababu timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara si za kitoto; unaona kabisa kila siku zinavyozidi kuimarika,” anaeleza kipa huyo.

“Ukweli, wapinzani wote wamekuwa na viwango bora sana ambavyo vimeweza kubishana na klabu kubwa kama Yanga, na hapo ndipo zinaleta ugumu wa ligi na hata ubingwa utakuwa wa kipekee.”

NAFASI KIKOSINI

Kipa huyo aliyetua Yanga Januari 2022 kutoka Mtibwa Sugar anasema kukosa nafasi ya kucheza ni sehemu ya ushindani na si jambo la kulalamikiwa, bali ni ishara kwamba aliyepo anafanya vizuri zaidi.

Anaeleza kuwa kama mchezaji aliyepo juu asingekuwa kwenye kiwango kizuri, basi nafasi zingetolewa kwa wengine. Kila mmoja anapaswa kuheshimu ubora wa mwenzake na kuendelea kujipanga kusubiri nafasi yake.

“Kukosa nafasi sio suala baya wala zuri, ila inaleta maana kwamba aliye juu yetu ni bora na anafanya vyema kwa muda ambao anaupata. Laiti angekuwa hafanyi vyema, basi tungekuwa tunapata nafasi sisi ambao tuko nyuma yake. Lakini yote kwa yote kila mtu anaona ubora wake na anastahili kuwa hapo alipo,” anasema.

KUHUSU DIARRA

Akimzungumzia kipa namba moja wa kikosi hicho na timu ya taifa ya Mali, Djigui Diarra, anasema ni bora na mwenye sifa zinazomfanya astahili nafasi yake ndani ya kikosi. Licha ya ushindani uliopo, bado anajifunza mambo mengi kutoka kwake, hasa utulivu na namna anavyofanya maamuzi uwanjani.

Anasema kujifunza kutoka kwa mchezaji bora kunamsaidia kukuza uwezo wake na kumjenga zaidi kitaalamu.

“Licha ya kwamba tunapokezana namba (nafasi), lakini Diarra ni kipa mkubwa sana na bora, ana kila sababu ya kuwa pale. Kwangu mimi ananifundisha mambo mengi. Ukimuangalia tu, unaona anastahili kuwa pale; ana utulivu mkubwa, anacheza kwa akili kubwa. Najifunza vingi kutoka kwenye ile nafasi,” anasisitiza Mshery.

TUKIO LA KUSISIMUA

Anasema alipitia hisia kali baada ya ushindi kwenye mechi ya Kombe la Muungano 2026 iliyopigwa Zanzibar kwa sababu ya uzito wa mashindano na matarajio yaliyokuwepo.

Katika mchezo huo wa fainali ambao Yanga ilikutana na Azam FC, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara waliibuka na ushindi wa penalti 5-4, Mshery akifuta mikwaju mmojawapo.

Nyanda huyo anaeleza kuwa kucheza kwenye timu kubwa kunahitaji matokeo chanya na hakutaka kubeba lawama ya kushindwa. Licha ya kufanya makosa, alijirekebisha kwa wakati na kusaidia timu kufikia lengo, jambo linaloonesha kukua kwake kiakili na kimchezo.

“Kwenye ile mechi ya Kombe la Muungano nililia baada ya timu kutoka na ushindi; nadhani kilikuwa kitu kikubwa sana. Tupo kwenye timu kubwa ambayo kila mtu akiiangalia anatamani kuona tunapata mafanikio,” anasema Mshery.

“Kwa hiyo sikupenda kuwa na historia mbaya, hasa kwenye michuano migumu kama ile na timu kukosa kombe. Licha ya makosa niliyofanya, nilijisahihisha na nikafanikisha.”

NJE YA UWANJA

Kipa huyo anasema maisha yake nje ya uwanja ni ya utulivu na yanahusisha muda mwingi na familia yake. Hali hiyo humsaidia kuwa na utulivu wa akili na kujiandaa vizuri kwa majukumu ya mechi.

Anasema pia anajituma kufanya mazoezi binafsi, jambo linalomsaidia kuendelea kuboresha uwezo wake. “Nje ya uwanja mimi ni mtu ambaye napenda sana kukaa na familia. Kiufupi, mimi ni mtulivu na hufanya mazoezi binafsi muda mwingi.”

MALENGO YA MSIMU HUU

Akigusia malengo, Mshery anasema makubwa ni kujiandaa ili kuboresha kiwango cha uchezaji, na hutumia muda wake kufanya maandalizi ya ziada ili kuhakikisha anakuwa tayari wakati wowote atakapopata nafasi.

Anasema maandalizi hayo yatamsaidia kuepuka pengo la kiwango anapopata nafasi ya kucheza. “Ili kuhakikisha naendelea kuwa bora msimu huu, malengo yangu ni kufanya maandalizi zaidi ambako kutanipelekea mimi kuweza kufanya vizuri. Kwa sasa ambapo Diarra yupo, maandalizi ndiyo kitu pekee ninachotakiwa kukifanya kwa muda mrefu zaidi ili muda ukifika basi kusiwe na pengo kubwa,” anasema.

HAKUNA MATATA

Anasema mashabiki hawapaswi kuwa na wasiwasi endapo kutakuwa na mabadiliko ya kikosi kwa sababu timu ina uwezo wa kuendelea kufanya vizuri.

Anaeleza kuwa mafanikio ya timu hayategemei mchezaji mmoja bali juhudi za pamoja, kwani kila mchezaji yuko tayari kupambana ili kuhakikisha timu inapata matokeo chanya.

“Kukosekana kwa Diarra kusiwatie hofu mashabiki. Hakuna msimu ambao hayupo, kwa sababu hakuna msimu ulimalizika akiwa amecheza mechi zote.

“Kwa hiyo hata sisi tulicheza na timu ikaenda kupata ubingwa, na kiukweli tutapambana kwa sababu kila mtu anatamani kuona mafanikio ya timu.”

HAKUNA ZOEZI GUMU

Anasema mazoezi magumu ni sehemu ya mafanikio yake na ndiyo yanayomsaidia kuwa bora zaidi. Anaeleza kuwa anayaona mazoezi hayo kama fursa ya kujijenga badala ya mzigo, kwani mapenzi yake kwa kazi yake yanamfanya akubali changamoto zote na kuzitumia kama njia ya kufikia mafanikio.

“Ni kweli kwenye nafasi yangu nafanya mazoezi magumu, lakini ndiyo ubora wangu unapopatikana, kwa hiyo napenda kila kitu ninachokifanya.”

TAKWIMU ZAKE

Msimu huu Mshery amekaa golini kwenye mechi tatu, zikiwemo mbili za nyumbani dhidi ya Fountain Gate na Mashujaa, na mchezo mmoja wa ugenini dhidi ya Coastal Union, ambazo zote hakuruhusu bao na Yanga ikishinda zote. Yanga msimu huu kabla ya jana ilikuwa imeruhusu mabao matatu kwenye mechi zake 16 dhidi ya KMC (4-1), Dodoma Jiji (3-1) na Mtibwa Sugar (1-1), ambazo zote Diarra alikuwa golini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *