Dar/mikoani. Baadhi ya viongozi wa dini wameonyesha kuguswa na hali ya kuporomoka kwa maadili katika jamii, wakisisitiza umuhimu wa kurejea kwenye misingi ya ukweli, huku wakikemea tabia ya wananchi kushangilia vifo vya viongozi.

Viongozi hao wa kiroho, wamesema mwenendo huo ni dalili ya hatari ya mmomonyoko wa utu na mshikamano wa kijamii lakini upande wa wa pili, waliopo madarakani wakmetakiwa kujitafakari.

Kauli za viongozi hao wa dini, zinakuja wakati ambao kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu kuonyesha kufurahishwa pale kunapotokea kiongozi wa umma au chama tawala amefariki dunia.

Imekwenda mbali zaidi hadi baadhi wamekuwa wakiandika katika kurasa zao za mitandao ya kijamii, wakiomba baadhi ya viongozi wakumbukwe na matukio yatakayoondoa uhai wao.

Tabia hizo, zimewahi kukemewa hata na viongozi wa Serikali, akiwemo Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, aliyesema siku hizi watu wanatumia vibaya mitandao ya kijamii kuandika kuhusu vifo kama vile havitawahusu.

Viongozi hao wa dini katika mahubiri yao na wengine walipozungumza na Mwananchi jana Jumamosi, April 4, 2026 kupata ujumbe wao wa Pasaka, wamesema kilichopo ni dalili ya migawanyiko na kukosekana kwa haki na utu, hali hiyo ambayo inaenda kuathiri mustakabali wa Taifa.

Inaashiria tatizo kubwa

Akitoa mahubiri kwenye ibada ya Ijumaa Kuu, Aprili 3, 2026 katika Parokia ya Bikira Maria wa Mlima wa Karmeli, Bunju Dar es Salaam, Askofu wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo, Stephano Musomba alisema mwenendo wa kufurahia vifo unaashiria kuwepo kwa tatizo kubwa la kijamii linalohitaji mjadala wa kina ili kupata suluhisho la kudumu.

Askofu Musomba amesema kinyume na hali ilivyo sasa, mila za Kiafrika zimekuwa zikithamini mshikamano na maombolezo wakati wa vifo, badala ya kushangilia.

“Mila zetu za Kiafrika si kawaida mtu anakufa leo unashangilia, si kawaida. Huwa tunalia, eeh, tena hadi mtu anakubeba, lakini leo watu wanashangilia.

“Tunapoliona hilo viongozi wanalalamika, wananchi wanalalamika bila kuangalia nini kilichotufikisha hapo. Kwa nini tumefika hapa, kwa nini tunashangilia vifo vya wenzetu? Tukae chini tujadili pamoja, tumekosea wapi,” amesema Askofu Musomba.

Askofu Musomba ametoa wito kwa wananchi kuzingatia mazungumzo na majadiliano kama njia ya kutatua tofauti za kisiasa na kijamii, badala ya kukuza chuki na migogoro.

Tutafute ufumbuzi

Askofu wa Kanisa la Zanzibar International Christian Center (ZICC), Dickson Kaganga aliungana na Askofu Musomba akisema kwa hali ilivyo, watu kufikia hatua ya kushangilia vifo vya wenzao, sio utamaduni wa Watanzania bali kama taifa kila mtu kwa nafasi yake wapaswa kujiuliza.

 “Kwasasa ukipita mitandaoni, unasema loh! hali si shwari, zamani tulikuwa mtu akifa watu wanasikitika, bila kujali itikadi za vyama, kabila wala dini,” amesema.

Kiongozi huyo wa kiroho amesema: “…kwa sasa hali ilivyo tunapaswa kujiuliza wapi tumeteleza, tukae meza moja kutafuta ufumbuzi.”

Tuthamini utu

Akizungumza na Mwananchi, Askofu wa Kanisa la Anglikan Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sostheness amesema Pasaka ni sikukuu ambayo wayahudi walisherekea kwa ajili kufurahia kukombolewa kutoka mateso ya Wamisri.

“Ndani ya sikukuu hiyo tunajifunza kuishi katika matendo mema na kuthamini utu wa mtu mwingine kama Mungu alivyotathamini utu wa mwanadamu.

Kuhusu baadhi ya Watanzania kushangalia vifo vya viongozi, Askofu Sostheness amesema kiasili Watanzania hatuna utamaduni huo, kwani kifo ni jambo la huzuni.

“Kama kuna jambo lolote lenye kuleta uchungu au hasira liwekewa namna bora la kushughulikia, kuliko kuvunja utamaduni na kuondoa hali ya kuthamiana kama Watanzania,” amesema Askofu Sostheness.

Wakati wa kujisahihisha

Askofu wa Kanisa la Evangelical Brotherhood Church, mkoani Mbeya, Rabbi Mwakanani amesema wakati Wakristo wakisherekea kufufuliwa kwa Yesu, Watanzania wanapaswa kuwa na mwanzo na mwelekeo mpya kwa mtu mmoja mmoja ili kuijenga nchi.

Amesema yaliyojitokeza yanapaswa kubaki kama sehemu ya funzo na kuacha chuki binafsi, visasi akiwaomba viongozi wa Serikali na dini kujisahihisha na kujitafakari pale walipokosea ili kuongoza Taifa kwa mtazamo mpya.

Mwakanani aliungana na viongozi wengine kukemea wanaofurahia mitandaoni vifo vya viongozi akisema si jambo zuri japokuwa inabaki kuwa ujumbe kwa viongozi wote mbali na upande wa siasa, hivyo lazima wajitafakari.

Askofu mstaafu wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Solomon Masangwa amesema ni muhimu kwa Taifa kurejesha amani na kusahau ya kale yaliyotokea.

Dk Masangwa amesema Pasaka ni siku ya kusheherekea ufufuo wa Yesu Kristo ambayo kwa tafsiri nyingine ni maisha mapya katika Kristo.

Dhana ya ukweli

Katika ibada hiyo, Askofu Musomba amesisitiza kuhusu umuhimu wa kusema ukweli kuhusu uhalisia wa mambo yalivyo na si kama watu wanavyotaka yawe.

“Ni ukweli kwamba tutakufa hata usiposimulia, hata ukijidai, ukijivuna, ukisema nina mali nyingi na kuona wengine hawana maana, utakufa ni kweli. Ni ukweli kwamba dunia inalizunguka jua si jua linaiuzunguka dunia,” amesema.

“Watu wanatafuta ukweli katika kusoma, lakini katika kuutafua ukweli huo wanaposoma wengi hawana ujasiri wa kuukabili na kuukubali kutokana na hofu walionayo ya kubomoa misingi ya walichokuwa wanafanya kwa muda mrefu,” amesema Askofu Musomba.

Mbali na hilo, Askofu Musomba amesisitiza kuwa ukweli ndio unaoleta maendeleo, akionya kuwa Taifa litarudi nyuma endapo uchawa utaendekezwa pasipo kuambizana ukweli.

Askofu Musomba amesisitiza njia ya pekee ni kukaa na kuelemishana sambamba na kuangalia kilichosababisha hali kufikia ilipo, akisisitiza ukweli ndio utakaoponya.

Suala la ukweli lilizungumzwa na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza katika salamu zake za Pasaka akiwataka waumini na jamii kwa ujumla kurejea katika msingi wa ukweli, akisisitiza kuwa ufufuko wa Yesu Kristo ni ushuhuda wa ushindi wa ukweli dhidi ya uongo.

Askofu Bagonza alifafanua mitume waliotoa ushuhuda huo walikuwa na dhamira ya kuondoa mashaka kwa watu wote ili waamini ukweli huo, huku akisisitiza kuwa hata wale waliomtesa na kumuua Yesu walipaswa kujua kuwa ukweli hauwezi kufichika milele.

“Tabia ya watu kukwepa ukweli haikuanza leo,” amesema Askofu huyo, akiongeza tofauti na zamani ambapo watu waliogopa kusema uongo, sasa hali imebadilika na wengi wanaogopa kusema ukweli.

Pamoja na hayo, zamani watu waliogopa kusema uwongo. Siku hizi watu wanaogopa

“Ni nini kimetokea? Watu wa zamani waliogopa kusema uwongo ili wasife na watu wa siku hizi wanaogopa kusema ukweli ili wasife. Aliyewaua wasema uwongo zamani ni Mungu (Matendo 5: 4b). Anayewaua wasema ukweli siku hizi ni mtu mwongo anayeongozwa na shetani baba wa uwongo,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *