Moshi. Baadhi ya wananchi mkoani Kilimanjaro wamelalamikia baadhi ya wafanyabiashara wa maduka ya rejareja mkoani humo kuwapandishia bei ya sukari kiholela, wakisema hali hiyo inazidi kuwaumiza kutokana na ugumu wa maisha.

Leo Jumamosi, Aprili 4, 2026, Mwananchi limepita katika maduka mbalimbali ya rejareja Manispaa ya Moshi na kushuhudia ongezeko hilo la bei kutoka Sh3,000 hadi Sh3,500 kwa kilo.

Wakizungumzia kupanda kwa bei hiyo, wananchi hao wameitaka Serikali kuchukua hatua za haraka kudhibiti bidhaa hiyo muhimu ili ipatikane kwa bei nafuu kwa wananchi wa kipato cha chini.

Akizungumza, mkazi wa Moshi, Evenline Mrosso, amesema kupanda kwa bei ya sukari kunawaumiza zaidi wananchi wenye kipato cha chini, ambao tayari wanakabiliwa na changamoto za kiuchumi.

“Bei ya sukari imekuwa juu sana ukilinganisha na kipato chetu sisi watu wa chini, inakuwa vigumu kumudu mahitaji ya kila siku,” amesema.

Kwa upande wake, mkazi mwingine wa Moshi, Jenes James, ameomba Serikali kutafuta suluhisho la kupunguza ugumu wa maisha kwa kuhakikisha bidhaa hiyo muhimu inapatikana kwa bei nafuu.

“Leo tunaambiwa sukari imepanda bei, wakati inazalishwa hapa hapa Moshi. Tunaomba Serikali iangalie jambo hili kwa umakini kwa sababu wananchi wa chini ndio tunaoteseka,” amesema.

Naye, mkazi mwingine wa mkoa huo, Janeth Temu, amesema baadhi ya wafanyabiashara wanachangia kupanda kwa bei hiyo ya sukari na kwamba wanapandisha kiholela.

“Jana nimezunguka maduka mengi ya rejareja na kukuta yote yanauza Sh3,500. Ukiwauliza, wanasema hata wao wamenunua kwa bei ya juu kutoka kwa wauzaji wa jumla,” amesema.

Akizungumza, mmoja wa wafanyabiashara wa duka la rejareja mjini Moshi, Geofrey Joseph, amesema wamelazimika kupandisha bei ya sukari kutokana na kwamba wanauziwa kwa bei ya juu kwenye maduka ya jumla pamoja na gharama za usafiri kupanda.

“Vitu sasa hivi vimepanda bei, gharama za usafiri zimekuwa kubwa na hata huku tunakonunulia sukari wametupandishia bei, hivyo na sisi ni lazima tupandishe,” amesema mmoja wa wafanyabiashara hao.

Mmoja wa wasambazaji wa sukari mjini hapa, kutoka kampuni ya Marenga Investment, Joseph Kimoso, amesema kama wasambazaji wakubwa wa sukari mjini hapa hawajapandisha bei ya sukari kama inavyodaiwa.

“Sisi hatujapandisha bei ya sukari, mfuko mmoja wa kilogramu 50 tunauza kwa Sh124,000 na ni bei ya siku zote,” amesema mfanyabiashara huyo.

Alichokisema RC Babu

Akizungumzia kupanda kwa bei ya sukari, Mkuu wa Mkoa huo, Nurdin Babu, amesema katika mkoa huo hakuna bei mpya ya sukari iliyotangazwa na kwamba wakiwabaini wafanyabiashara ambao wamepandisha bei kiholela watachukuliwa hatua za kisheria.

“TPC ambao ni wazalishaji wa sukari hawajanipa taarifa kwamba wamepandisha bei. Nitoe wito kwa wafanyabiashara wote ambao wamepandisha sukari kiholela, tutawachukulia hatua za kisheria. Tayari nimeshatuma watu wangu baada ya kusikia hizo fununu wapite ili waangalie kama ni kweli tutachukua hatua,” amesema RC Babu.

“Kama TPC ambao ni wazalishaji na kiwanda kipo Moshi na hawajapandisha bei ya sukari, kwa nini wafanyabiashara wapandishe bei ya sukari? Hatuwezi kuwaonea wananchi, kiwanda kipo Moshi na kina sukari ya kutosha.”

Akizungumza Mwanasheria wa Kiwanda cha Sukari cha TPC ili kujua kama wamepandisha bei hiyo ya sukari, David Shillatu amesema sukari haijapanda bei na kwamba wanachokifanya wafanyabiashara hao ni kuwapa taharuki wananchi bila sababu.

“Hakuna sababu ya kupandisha sukari, wanataka kupanikisha wananchi kwa kuwauzia bei za juu. Hakuna kuwaumiza wananchi kwa kuwauzia bei za juu. Sisi wazalishaji tupo vizuri na tunawakaribisha waje wanunue kwa utaratibu, wasiwasababishie wananchi wakanunua sukari kwa Sh3,500, hapana,” amesema Shillatu.

Amesema, licha ya kwamba kipindi kama hiki cha kuanzia mwezi Machi kila mwaka shughuli za uzalishaji husimama kwa muda kupisha mvua za masika, bado sukari wanayo ya kutosha zaidi ya tani 18,000.

“Kipindi kama hiki huwa tunasimamisha shughuli za uzalishaji wa sukari kupisha mvua za masika kila mwaka, na sasa hivi tuna tani za sukari 18,000. Hakuna sababu ya watu kuuza sukari kwa kupaniki,” amesema Shillatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *