Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa kidijitali unaokua kwa kasi, taarifa za afya zimekuwa zikisambaa kwa urahisi mkubwa, lakini wataalamu wa afya wanaonya kuwa si kila unachokiona mtandaoni ni salama kwa afya yako.

Taarifa potofu (misinformation) zimekuwa tishio kubwa, zikichangia watu kufanya maamuzi hatarishi kuhusu afya zao, ikiwemo kukataa chanjo, kutumia vipodozi au dawa zisizo sahihi, au kuamini tiba zisizothibitishwa kisayansi.

Leo, Aprili 5, 2026, dunia inaanza rasmi maadhimisho ya Siku ya Afya Duniani 2026 yanayofanyika Aprili 7 mwaka huu, yaliyobeba ujumbe mzito: “Pamoja tutumie sayansi kwa manufaa yetu sote.” Lengo ni kuhamasisha jamii kuchagua ukweli badala ya upotoshaji na kusisitiza umuhimu wa sayansi katika kulinda maisha ya binadamu.

Utafiti wa mwaka 2025 kuhusu mitandao ya kijamii ulibaini kuwa taarifa potofu za afya husambaa kwa kasi kubwa kupitia mitandao hiyo, huku watu wachache wenye ushawishi wakichangia kueneza sehemu kubwa ya taarifa hizo.

Lakini kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, kila chanjo, tiba na mafanikio ya afya tunayoyaona leo yanatokana na utafiti wa kisayansi uliothibitishwa kwa ushahidi.

Hata hivyo, ongezeko la taarifa zisizo sahihi mtandaoni linahatarisha mafanikio hayo kwa kupunguza imani ya jamii kwa wataalamu wa afya na mifumo rasmi ya huduma.

“Katika dunia inayokabiliwa na changamoto nyingi za kiafya, tunahitaji kusimama na sayansi kwa kuzingatia ushahidi, ukweli na mwongozo wa kitaalamu,” amesisitiza Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, katika taarifa yake ya maadhimisho ya mwaka huu.

Kufuatia hilo, wataalamu wa afya nchini wameonya kuongezeka kwa taarifa na matangazo ya matibabu yasiyo na uthibitisho wa kisayansi yanayosambazwa kupitia mitandao ya kijamii, wakisema mwenendo huo unahatarisha maisha ya wananchi.

Mkuu wa Idara ya Upasuaji katika Hospitali ya Muhimbili-Mloganzila, Erick Muhumba, amesema licha ya kuwapo kwa uhuru wa watu kuchapisha maudhui mtandaoni, bado kuna haja ya udhibiti na ufuatiliaji makini ili kulinda usalama wa jamii.

“Kunakuwa na uhuru wa watu kuposti chochote mtandaoni, wakati huo huo kuna changamoto ya uelewa kwa jamii, kwani haifuatilii na kusoma kabla ya kukubali kutumia. Mtu anatumia upasuaji kukuza makalio, kisha anakwenda kuudanganya umma kwamba ukipaka dawa hii unapata matokeo, ilhali ni uongo na dawa hiyo haijathibitishwa kisayansi,” amesema.

Amesema baadhi ya watu wasio wataalamu wa afya wamekuwa wakitoa ushauri wa tiba au kupendekeza matumizi ya dawa bila ujuzi sahihi, hali inayoweza kusababisha madhara makubwa kiafya.

“Unakuta mtu anashauri matumizi ya dawa au hata taratibu za kimatibabu zinazohusisha kugusa mwili wa binadamu bila kuwa na taaluma husika. Hii ni hatari, na vyombo vinavyosimamia vinapaswa kufuatilia kwa karibu,” amesema Dk Muhumba, ambaye pia ni mtaalamu wa upasuaji wa kurekebisha maumbile.

Ameongeza kuwa changamoto kubwa ni uelewa mdogo kwa baadhi ya wananchi wanaoamini kirahisi kila wanachokiona mtandaoni bila kufanya uhakiki wa taarifa hizo.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Mugisha Nkoronko, amesema ni muhimu kwa jamii kuzingatia matumizi ya sayansi ya tiba katika kufanya maamuzi ya kiafya.

Akizungumzia maadhimisho ya Siku ya Afya Duniani, Dk Nkoronko amesema dunia inahimizwa kutumia sayansi kwa manufaa ya wote na kupinga upotoshaji wa taarifa za afya.

“Sayansi ya tiba imejengwa katika misingi ya utafiti, majaribio na uthibitisho. Hatuwezi kuruhusu taarifa zisizo na ushahidi kusambazwa na kuaminika kirahisi,” amesema.

Amesisitiza kuwa, kutokana na maendeleo ya teknolojia, watu wengi sasa wanazungumzia masuala ya afya bila kuwa na ushahidi wa kisayansi, jambo linaloweza kupotosha umma.

Aidha, amewataka wananchi kuepuka kutumia dawa au kuanza matibabu kwa kutegemea dalili walizoziona mtandaoni pekee; badala yake, wafike katika vituo vya afya ili kupata uchunguzi na matibabu sahihi.

“Ni lazima tutumie sayansi kuthibitisha ugonjwa kabla ya kuanza tiba. Hata kama ni upasuaji, lazima ufanyike chini ya wataalamu waliothibitishwa,” ameongeza.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, wataalamu hao wamezitaka taasisi za utafiti na afya kama Taasisi ya Afya Ifakara na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu kuendelea kutoa elimu kwa umma na kushirikiana na mamlaka za udhibiti kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia wananchi.

Pia wamehimiza matumizi sahihi ya teknolojia, ikiwemo akili mnemba (AI), katika sekta ya afya, wakisema inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kuboresha huduma endapo itatumika kwa kuzingatia misingi ya kitaalamu na maadili.

Wamesisitiza kuwa mapambano dhidi ya taarifa potofu yanahitaji ushirikiano wa wadau wote, ikiwemo serikali, wataalamu wa afya na wananchi wenyewe, ili kuhakikisha jamii inalindwa dhidi ya madhara yanayoweza kuepukika.

Kampeni ya mwaka mzima ya Siku ya Afya Duniani inalenga kuonyesha nguvu ya ushirikiano wa kisayansi duniani, kuanzia tafiti za lishe bora, maji safi na usafi wa mazingira, hadi maendeleo ya chanjo, dawa na tiba za magonjwa sugu na afya ya akili.

Aidha, inahimiza nchi kuimarisha uwezo wa tafiti na kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa usawa.

“Jukumu la kupambana na taarifa potofu si la serikali au taasisi pekee, bali ni la kila mtu. Wananchi wanahimizwa kuchagua vyanzo vinavyoaminika, kushirikisha taarifa sahihi katika jamii zao na kuchukua hatua zinazotegemea ushahidi wa kisayansi.

“Katika wakati ambapo taarifa zinaenea kwa kasi kuliko wakati mwingine wowote, ujumbe wa mwaka huu unabaki kuwa wazi: kuchagua taarifa sahihi ni hatua ya kwanza kuelekea maamuzi bora ya afya na hatimaye maisha bora kwa wote,” amesema Dk Tedros.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *