
KIUNGO wa Simba Queens, Vivian Corazone amesema hakuna mechi rahisi kwenye ligi hiyo kwani kila timu inapambana zaidi inapokutana nayo.
Simba iko kileleni na pointi 34 baada ya mechi 12 na Jumatano hii itacheza mchezo wa raundi ya 13 dhidi ya Bunda Queens ugenini saa 10 jioni.
Corazone amesema ukubwa wa Simba unazifanya timu pinzani kuongeza juhudi zinapokutana nao, jambo linaloongeza ushindani mkubwa uwanjani.
Amesema kila mchezo dhidi ya Simba huwa na presha tofauti kutokana na historia na mafanikio ya timu hiyo katika soka la wanawake.
“Hakuna timu rahisi, kila timu inakuwa ngumu zaidi inapocheza na Simba, hivyo tuko makini msimu huu ili kuhakikisha malengo yanatimia,” amesema Corazone na kuongeza;
Akizungumzia mechi na Bunda amesema “Kila tukikutana na Bunda wanatupa changamoto, lakini tunaamini tumejipanga vizuri kuhakikisha tunafanya vizuri japokuwa sio rahisi kuchukua pointi tatu.”