Dodoma. Uamuzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kusitisha leseni ya mtandao wa Jamiiforums kwa siku 90 umesababisha mtumiaji wa jukwaa hilo, Fortunatus Buyobe, kufungua shauri la kikatiba kupinga uamuzi huo.

Buyobe, anayewakilishwa na wakili John Seka, amevuka hatua ya awali baada ya Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dodoma, kutupa mapingamizi yaliyowasilishwa na TCRA pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Shauri hilo linasikilizwa na jopo la majaji watatu—Arnold Kirekiano, Dk Lilian Mongela na Hadija Kinyaka, likiwahusisha Vapper Tech Limited, kampuni inayomiliki Jamiiforums, kama mlalamikiwa wa kwanza, huku TCRA na AG wakiwa wa pili na wa tatu.

Kwa mujibu wa hati ya madai, Buyobe anapinga uamuzi wa TCRA wa Septemba 6, 2025, wa kusitisha leseni ya Jamiiforums kwa madai ya kuchapisha maudhui yanayokiuka sheria, tamaduni na desturi za nchi.

Kwa mujibu wa shauri hilo, TCRA ilidai maudhui hayo yaliathiri umoja wa kitaifa, amani, utulivu na kudhalilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, Buyobe, ambaye ni mtumiaji aliyethibitishwa wa mtandao huo, anadai hatua hiyo inakiuka haki zake za kikatiba za kutafuta, kupokea na kutoa taarifa na imeathiri uhuru wake wa kutoa maoni.

Pia, anapinga Kanuni namba 9(a), (c), (e), (g) na (j), lakini pia Kanuni za 12(a)(i), 15(A), pamoja na aya ya 3(a), 9 na 10 ya Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni za mwaka 2020, kwani zinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara za 18(a), (b), (c), (d), 20(1) na 29(1).

Buyobe anaiomba mahakama itamke kuwa kusitishwa kwa leseni kunakiuka haki za kimsingi kama zilivyoainishwa katika Ibara za 18 na 29 za Katiba.

Mbali na maombi hayo, anaomba mahakama itamke kuwa baadhi ya vifungu vya Kanuni ya 9, 12, 15 na 16 na GN namba 538 ya mwaka 2020 vinakiuka Ibara za 18(a), (b), (c), (d), 20(1) na 29(1) za Katiba.

Pia, anaiomba mahakama itoe tamko kuwa kusitishwa kwa leseni kulikiuka Ibara ya 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR), kifungu cha 9 cha Mkataba wa Kiafrika wa Haki za Binadamu na Watu na kifungu cha 19 cha Tamko la Kimataifa la Haki za Kibinadamu.

Awali, TCRA na AG waliwasilisha pingamizi mbiili wakidai shauri hilo halina uwezo wa kisheria kwa kushindwa kutumia njia mbadala, kinyume na masharti ya kifungu cha 8(2) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu (BRADEA), Sura ya 3, toleo lililorekebishwa la mwaka 2023.

TCRA na AG wamewakilishwa na wakili wa Serikali Mkuu, Vivian Method, wakati Jamiiforums inawakilishwa na wakili Peter Manjanjala.

Katika pingamizi la pili, walidai ombi la namna hiyo lilishatolewa uamuzi kuhusiana na masharti yaliyopuuzwa ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta za mwaka 2020 kama ilivyorekebishwa, kwa kuamuliwa na mahakama hiyo.

Hata hivyo, wakili Seka alipinga hoja hizo akieleza kuwa kifungu cha rufaa ndani ya sheria ya TCRA kinamhusu mwenye leseni pekee, si mtumiaji kama mlalamikaji.

Alisisitiza kuwa shauri hilo linahusu ukiukwaji wa haki za kikatiba za mtu binafsi.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, mahakama iliamua kuwa pingamizi zilizowasilishwa hazina mashiko, na kwamba mlalamikaji amekidhi vigezo vya sheria ya Bradea na kwamba, kwa uchambuzi wa hoja zote za kisheria, wanaona shauri hili liko kisheria kwenda katika hatua ya pili ya kusikilizwa kwa shauri la msingi.

Uamuzi huo ulitolewa Machi 17, 2026, na kuchapishwa katika tovuti ya TanzLII, ukiruhusu kesi hiyo kuingia hatua inayofuata ya usikilizwaji wa hoja za msingi.

Mahakama inatarajiwa kutoa uamuzi Aprili 9, 2026, kuhusu ombi la Buyobe la kutaka kuhoji kiapo cha TCRA, akidai hakijitoshelezi.

Upande wa Serikali umesisitiza kuwa kiapo hicho kinatosha, hivyo uamuzi huo utaelekeza hatua inayofuata ya mwenendo wa kesi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *