Hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu inaanza leo kwa uwepo wa mechi mbili zitakazochezwa katika miji tofauti barani Ulaya kuanzia saa 4:00 usiku kwa muda wa Afrika Mashariki.

Mchezo ambao unaonekana utabeba hisia za wengi leo ni baina ya Real Madrid dhidi ya Bayern Munich itakayochezwa katika Uwanja wa Santiago Bernabeu, Hispania.

Mafanikio ya timu hizo mbili katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na mashindano ya ndani katika nchi zao kwa kila moja yanafanya mchezo wa leo kusubiriwa kwa hamu na idadi kubwa ya wapenzi wa soka ulimwenguni.

Wakati Real Madrid ikiwa bingwa wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wakitwaa taji hilo mara 15, Bayern Munich yenyewe imechukua ubingwa wa mashindano hayo mara sita.

Utamu mwingine wa mechi ya leo ni historia ya timu hizo kuwa ndizo zimekutana mara nyingi zaidi katika mashindano ya Ulaya.

Timu hizo zimewahi kukutana mara 28 ambapo Real Madrid imeibuka na ushindi mara 13, Bayern ikipata ushindi mara 11 na michezo minne baina yao ikimalizika kwa sare.

Wenyeji Real Madrid wanaingia uwanjani wakiwa na historia nzuri dhidi ya wapinzani kutoka Ujerumani katika mechi 23 zilizopita ambapo imepata ushindi mara 16, kutoka sare sita na kupoteza mchezo mmoja tu.

Katika mchezo huo wa leo, Real Madrid itawakosa Thibaut Courtois na Rodrygo ambao ni majeruhi kama ambavyo ilivyo kwa Sven Ulreich upande wa Bayern Munich.

Refa kutoka England, Michael Oliver ndiye amepangwa kuchezesha mechi hiyo akisaidiwa na Stuart Burt na James Mainwaring na refa wa akiba Andrew Madley wote wakiwa wanatoka England pia.

Jijini Lisbon, Ureno katika Uwanja wa José Alvalade, wenyeji Sporting Lisbon wataikaribisha Arsenal katika mechi nyingine ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Timu hizo zimewahi kukutana mara mbili ambapo kila moja imepata ushindi mara moja.

Mchezo huo utachezeshwa na marefa kutoka Ujerumani ambapo wa kati atakuwa ni Daniel Siebert huku wasaidizi wakiwa ni Jan Seidel na Rafael Foltyn na wa akiba akipangwa kuwa Daniel Schlager.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *