Raia wa Ufaransa Cécile Kohler na Jacques Paris “wako huru na wako njiani kuelekea nchini Ufaransa, baada ya miaka mitatu na nusu wakiwa nchini Iran,” ambapo walifungwa kwa muda mrefu na kisha kuwekwa chini ya kifungo cha nyumbani katika ubalozi wa Ufaransa, ​​rais Emmanuel Macron ametangaza leo Jumanne, Aprili 7.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Cécile Kohler na Jacques Paris wameondoka Iran, ambapo walikuwa chini ya kizuizi cha nyumbani katika ubalozi wa Ufaransa huko Tehran tangu mwezi Novemba 2025, baada ya zaidi ya miaka mitatu wakiwa kizuizini. “Hii ni faraja kwetu sote na, bila shaka, kwa familia zao.” “Asante kwa mamlaka ya Oman kwa juhudi zao za upatanishi, kwa idara za serikali, na kwa raia ambao walihamasishwa bila kuchoka na hivyo kuchangia kurejea kwao,” ameongeza Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Kulingana na vyanzo vilivyo karibu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noël Barrot, wafungwa hao wawili wa zamani waliondoka Iran siku ya Jumanne “alfajiri” wakiwa na balozi wa Ufaransa nchini Iran na chini ya ulinzi wa kidiplomasia, na “kwa sasa wako Azerbaijan.” Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa inaandaa kurejea kwao Ufaransa kutoka Azerbaijan.

“Wako HURU!” 

Raia hawa wawili wa Ufaransa walihukumiwa, hasa kwa ujasusi kwa niaba ya Israel, kabla ya kuwekwa chini ya kifungo cha nyumbani katika ubalozi wa Ufaransa mapema mwezi Novemba, Emmanuel Macron ametangaza siku ya Jumanne. “Wako HURU!” “Walionyesha hisia na furaha yao kwa matarajio ya kurudi hivi karibuni katika nchi yao na kukutana na wapendwa wao,” ameongeza Jean-Noël Barrot, Waziri wa Mambo ya Nje.

Cécile Kohler, profesa wa fasihi mwenye umri wa miaka 41, na Jacques Paris, mwalimu mstaafu mwenye umri wa miaka 72, walikamatwa Mei 7, 2022, siku ya mwisho ya safari ya utalii nchini Iran. Walihukumiwa kifungo cha miaka 20 na 17 jela mnamo mwezi Oktoba 2025, hasa kwa ujasusi, kabla ya kuachiliwa huru mnamo Novemba 4, 2025, lakini wakiwa na marufuku ya kusafiri iliyowazuia kuondoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Wanadiplomasia walifanya kazi bila kuchoka ili kuweza kuachiliwa kwao, katika muktadha uliokuwa mgumu zaidi kutokana na vita nchini Iran, vilivyoanza mnamo Februari 28. Jean-Noël Barrot alizungumza na mwenzake, Abbas Araghchi, siku ya Jumapili.

Wanasiasa wamekaribisha kwa kauli moja kuachiliwa kwa wafungwa hao wa zamani. “Ufaransa imeonyesha umoja na uhamasishaji usioyumba ili raia hawa waweze kuachiliwa,” ametangaza Spika wa Bunge la kitaifa Yaël Braun-Pivet.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *