
Baada ya Marekani na Iran kukubaliana kusitisha vita kwa wiki mbili, ili kupisha mazungumzo, Tehran sasa inatarajiwa kufungua mlango wa Bahari wa Hormuz siku ya Alhamisi au Ijumaa, kuruhusu meli za mafuta kuanza kupita, ikiwa ni mojawapo ya makubaliano kwenye mkataba huo.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kufuatia tangazo hilo, mataifa mbalimbali duniani yakiongozwa na China, Urusi na Umoja wa Mataifa, yamekaribisha hatua hiyo ya Marekani na Iran, hatua ambayo wanasema itasaidia kuleta amani ya kudumu katika eneo la Mashariki ya Kati.
Baada ya tangazo hilo, bei ya mafuta ilishuka duniani, huku pipa la mafuta likiuzwa kwa Dola 95.
Naye rais Donald Trump kupitia mitandao yake ya kijamii ya Thruth amesema Iran haitarotubisha tena madini ya uranium, na nchi hizo mbili zitashirikiana kuondoa chembechembe za nyuklia zilizozikwa ardhini baada ya shambulizi ya mwaka uliopita, kauli ambayo imesisitizwa na Waziri wake wa ulinzi Pete Hegseth.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif, amesema mazungumzo kati ya Marekani na Iran yataanza siku ya Ijumaa, jijini Islamabad.
Sharif, amesema anatumaini kuwa mazungumzo hayo, yatasaidia kupatikana kwa suluhu ya kudumu, baada ya Marekani na Iran kukubaliana kusitisha vita kwa wiki mbili.
Kuelekea katika mazungumzo hayo, Iran imedai kushinda vita dhidi ya Marekani, na kusisitiza kuwa mchakato huo haumanishi kuwa vita vimekwisha, huku jeshi la kulinda mapinduzi ya nchi hiyo likisema haliamini ahadi za Marekani.