Maadhimisho ya Siku ya Afya Duniani 2026 yamekuja na wito mzito kwa Watanza­nia kusimama na sayansi ili kulinda afya na kujenga mus­takabali bora, huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likisisitiza kuwa ushahidi wa kisayansi ndio nguzo ya maendeleo ya sekta ya afya.

Kaulimbiu ya mwaka huu, “Pamoja kwa Afya; Simama na Sayansi,” inalenga kuhama­sisha matumizi ya ushahidi katika kufanya maamuzi, kui­marisha mifumo ya afya na kukabiliana na changamoto zinazoibuka ikiwemo magon­jwa ya mlipuko na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa WHO, sayansi imekuwa na mchango mkubwa katika kuokoa maisha nchini Tanzania kupitia huduma kama chanjo, uchunguzi wa magon­jwa, pamoja na mifumo ya ufua­tiliaji wa magonjwa. Hatua hizi zimewezesha kuboreshwa kwa huduma za afya na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika.

Taasisi za utafiti nchini zimetajwa kuwa nguzo muhimu katika mafanikio hayo. Taasisi kama Taasisi ya Taifa ya Uta­fiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Taasisi ya Afya ya Ifak­ara (IHI), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbi­li (MUHAS) na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) zimeku­wa mstari wa mbele kuzalisha ushahidi unaosaidia kuboresha sera na huduma za afya.

Matokeo ya matumizi ya sayansi yanaonekana wazi, iki­wemo kupungua kwa vifo vya watoto chini ya miaka mitano, pamoja na kuboreshwa kwa huduma za uzazi salama na upasuaji.

Tafiti zinaonyesha kuwa matumizi ya mbinu za kisay­ansi katika huduma za afya yamechangia kupunguza maambukizi baada ya upasuaji na vifo vya mama wakati wa kujifungua.

Aidha, WHO imeeleza umuhimu wa mbinu ya “Afya Moja” (One Health) inayoun­ganisha afya ya binadamu, wanyama na mazingira, husu­san katika kukabiliana na magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binad­amu na changamoto za maz­ingira.

Hata hivyo, changamoto kama upotoshaji wa taar­ifa za afya mitandaoni bado zinaathiri juhudi hizi. WHO imetoa wito kwa wananchi, wataalamu wa afya na waandi­shi wa habari kusambaza taar­ifa sahihi na zinazotegemea ushahidi.

Mratibu wa Kuimarisha Mifumo ya Afya (HSS), Dk Thomas Fedjo Tefoyet akizungumza kwa niaba ya Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania, Dk Alex Gasasira waka­ti wa maadhimisho ya Siku ya Afya Duniani yaliyokuwa na kaulimbiu: “Kwa pamoja, tutumie sayansi kwa manufaa ya wote.”

Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Afya kwa Umma kuto­ka Wizara ya Afya, Dk Rahma Hingora anasema Serikali kwa kushirikiana na WHO inaende­lea kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kuibeba sayansi katika kulinda afya, akihusisha juhudi hizo na kaulimbiu ya mwaka ya “One Health” inay­ounganisha afya ya binadamu, wanyama na mazingira.

Kwa mujibu wake, magon­jwa ya mlipuko kama Marburg Virus Disease na Mpox yana­onesha umuhimu wa ushirikia­no huo, kwani mengi hutokana na mwingiliano kati ya binad­amu, wanyama na mazingira.

Mkurugenzi wa Kukuza na Kuratibu Tafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Bin­adamu Tanzania, Dk Nyanda Ntinginya, anasema taasisi hiyo imeendelea kuzalisha ushahidi wa kisayansi kwa zaidi ya mion­go minne na nusu ili kusaidia kuboresha sera na mifumo ya afya nchini.

Anasema NIMR inashiriki­ana na wadau wa ndani na nje ya nchi katika kufanya tafiti na kutafsiri matokeo yake ili yaweze kutumika katika kufan­ya maamuzi sahihi ya kiafya.

Naye Mkurugenzi wa Kiu­fundi wa Mradi wa Usalama wa Afya Duniani kutoka CIHEB Tanzania, Dk Siril Kullaya, anasema takribani asilimia 60 hadi 70 ya magonjwa ya mlipu­ko yanatokana na wanyama na mazingira.

Anasisitiza kuwa matumizi ya mkakati wa “Afya Moja” yanawezesha kugundua na kud­hibiti magonjwa mapema kabla hayajaenea kwa binadamu, huku akibainisha kuwa ushiriki­ano kati ya sekta za afya ya bin­adamu, mifugo na mazingira ni muhimu katika kukabiliana na changamoto hizo.

“Afya na uchumi vinaenda pamoja. Tukishirikiana vizuri kama Taifa, tutaimarisha usalama wa afya na kuchochea maendeleo ya kiuchumi,” anas­ema Dk Kullaya.

Akizungumza kupitia ujumbe wake rasmi, Mkuru­genzi wa WHO Kanda ya Afrika, Dk Mohamed Janabi anas­ema kaulimbiu ya mwaka huu, inaakisi mchango mkubwa wa tafiti za kisayansi katika kuokoa maisha na kuboresha huduma za afya duniani.

Anasema maendeleo ya kisayansi yamewezesha kupati­kana kwa kinga bora, matibabu madhubuti na kuongeza umri wa kuishi kwa wananchi, huku Afrika ikiwa mstari wa mbele katika baadhi ya mafanikio hayo.

“Wanasayansi wa Afrika, taasisi na jamii zimekuwa na mchango mkubwa katika kuk­abiliana na changamoto za kiafya. Mfano ni maendeleo ya haraka ya chanjo za Ebola wakati wa milipuko ya magon­jwa Afrika Magharibi na Kati,” anasema.

Anaongeza kuwa uwezo wa uchunguzi wa vinasaba (genomic sequencing) nchi­ni Afrika Kusini uliwezesha kubainika mapema kwa aina mpya za virusi vya UVIKO-19, hatua iliyosaidia dunia kuchu­kua tahadhari mapema.

Anasema jitihada za afya ya umma zinazotegemea usha­hidi wa kisayansi zimeleta mafanikio makubwa, hata hivyo, amebainisha kuwa bado Afrika inakabiliwa na changa­moto nyingi ikiwemo magon­jwa sugu, milipuko mipya ya magonjwa na mifumo dhaifu ya afya.

Anaeleza kuwa mkakati wa Afya Moja unaohamasisha ush­irikiano kati ya sekta mbalim­bali umesaidia nchi nyingi za Afrika kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa, tathmini ya hatari na mwitikio wa dharura za kiafya.

Pamoja na mafanikio hayo, bado kuna upungufu wa fedha za utafiti, mifumo ya ufuatili­aji isiyo imara na udhaifu katika mifumo ya tahadhari za mape­ma.

Kwa sasa, nchi 46 za Afrika zimeandaa mipango ya kitaifa ya usalama wa afya, huku nchi zote wanachama zikiwa na mikakati ya kukabiliana na usu­gu wa dawa dhidi ya vimelea.

Pamoja na mafanikio hayo, bado kuna upungufu wa fedha za utafiti, mifumo ya ufuatili­aji isiyo imara na udhaifu katika mifumo ya tahadhari za mape­ma.

WHO imezitaka Serikali za Afrika kuongeza uwekezaji wa ndani katika sayansi na ubunifu, huku ikiwahimiza washirika wa kimataifa kuunga mkono juhudi zinazoongozwa na Afrika kwa usawa na kuongeza upatikanaji wa teknolojia na maarifa.

“Ubunifu wa kisayansi unapaswa kuwafikia wote. Ugunduzi ambao hauwafikii wanaouhitaji zaidi bado ni kazi ambayo haijakamilika,” ana­sisitiza Dk Janabi.

Kwa ujumla, ujumbe wa mwaka huu unasisitiza kuwa kila mmoja ana nafasi ya kuchangia kwa kuamini say­ansi, kutumia ushahidi na kush­iriki katika kujenga jamii yenye afya bora.

WHO imezitaka taasisi za afya na watafiti nchini kuimari­sha matumizi ya sayansi ya utekelezaji ili kuboresha hudu­ma za afya na kuleta matokeo chanya kwa wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tan­zania, Dk Alex Gasasira, Dk Thomas Fedjo Tefoyet, Mratibu wa Kuimarisha Mifumo ya Afya (HSS) anasema mafanikio ya afya yanategemea si tu kugun­dua suluhisho, bali jinsi yana­vyotekelezwa katika mazingira halisi ya jamii.

Anasema taaluma za utafiti wa utekelezaji, utafiti wa uen­deshaji na utafiti wa vitendo zina mchango mkubwa kwa kuwa zinajibu maswali muhimu kama “nini kinafanya kazi, wapi, kwa nani na kwa namna gani.”

“Hata kama utafiti wa msingi ni muhimu, haukidhi mahi­taji yote. Tanzania ina nafasi kubwa ya kufanya vizuri zaidi kwa kuingiza ushahidi moja kwa moja kwenye mifumo ya huduma za afya,” anasema.

Anaeleza kuwa matumizi sahihi ya takwimu katika kupanga huduma, tathmini za ubora na uwezo wa wataalamu kubadilisha afua kulingana na mazingira yao ni miongoni mwa mambo yatakayosaidia kuongeza ufanisi wa sekta ya afya.

Hata hivyo, anasema bado kuna changamoto kadhaa ziki­wemo usambazaji hafifu wa matokeo ya tafiti, upungufu wa rasilimali, pamoja na mifumo isiyoratibiwa vizuri ya tak­wimu.

Anataja pia hitaji la taasisi kama SUA na NIMR kuongeza juhudi katika tafiti za magon­jwa yanayojitokeza na kurejea, pamoja na magonjwa yali­yopuuzwa na afya ya akili kwa vijana.

WHO inaendelea kuwahimi­za watafiti vijana na wahudumu wa afya walioko mafunzoni kut­ambua kuwa nchi yao inahitaji utaalamu wao wa kisayansi na ubunifu wao. WHO itasimama bega kwa bega na Serikali ya Tanzania na inathibitisha upya dhamira yake ya kushirikiana ili kuhakikisha kuwa sayansi inanufaisha wananchi wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *