
Dar es Salaam. Singida Black Stars leo, Ijumaa, Aprili 10, 2026 imetangaza kumuajiri aliyekuwa Kocha Mkuu wa Maniema ya DR Congo, Papy Kimoto kuwa Meneja wake Mkuu akichukua nafasi ya Othmen Najjar ambaye imeachana naye mwanzoni mwa wiki hii.
Taarifa ya Singida Black Stars imeeleza kuwa Kimoto ameambatana na Kapiten Dora ambaye atakuwa kocha msaidizi huku Muhibu Kanu akiendelea kuwa Kocha Mkuu.
“Uongozi wa Klabu ya Singida BS unapenda kuujulisha umma, mashabiki na wadau wa soka kuwa umefikia makubaliano ya kumuajiri Papy Kimoto kuwa Meneja Mkuu wa Timu, pamoja na Kapiten Ngoyi Dora kuwa Kocha Msaidizi, wote wakisaini mikataba ya mwaka mmoja na miezi mitatu.
“Aidha, Muhibu Kanu ataendelea kushika nafasi ya Kocha Mkuu hadi mwisho wa msimu huu, akisimamia kikamilifu majukumu ya kiufundi kwa kushirikiana na safu mpya ya Benchi la Ufundi.
“Uongozi una imani kuwa muundo huu mpya utaimarisha utendaji wa timu, kuongeza nidhamu na kurejesha ushindani unaotarajiwa,” imefafanua taarifa hiyo.
Kimoto anajiunga na Singida Black Stars akiwa na uzoefu wa kutosha wa kufundisha soka kwa ngazi ya klabu alioupata kwa kuzinoa timu tano tofauti nchini DR Congo.
Timu hizo ni Maniema, OC Renaissance, St- Eloi Lupopo, JS Kinshasa na AS Dragons.
Ni Kocha mwenye leseni Daraja A ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) inayomuwezesha kuwa Kocha Mkuu wa timu katika mashindano ya Klabu Afrika na hata timu za Taifa na amekuwa akipendelea kutumia mfumo wa 4-3-3.
Kabla ya Ukocha, Kimoto alikuwa mchezaji wa kimataifa wa DR Congo na ametumikia klabu nyingi barani Ulaya zikiwezme Sint Truiden, Lokeren na Standard Liege za Ubelgiji, Bursaspor ya Uturuki pamoja na Hapoel Ramat Gan na Hapoel Petah Tikva za Israel.
Mafanikio makubwa ya Kimoto katika ukocha ni kuiongoza Maniema kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.
Aprili 6 mwaka huu, Singida Black Stars ilitangaza kuvunja benchi lake la ufundi kutokana na mwenendo usioridhisha katika Ligi ambapo pia ilitangaza kukata mishahara ya wachezaji kwa asilimia 40.