Dar es Salaam. Mashirika ya misaada na Umoja wa Mataifa yameonya mfumo wa afya nchini Venezuela umefikia ukomo wa uwezo wake kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililolikumba jimbo la La Guaira wiki moja iliyopita, huku idadi ya vifo ikizidi kuongezeka na matumaini ya kuwapata manusura yakizidi kufifia.

Kwa mujibu wa serikali ya Venezuela, zaidi ya watu 1,900 wamefariki dunia, huku maelfu wakijeruhiwa na wengine zaidi ya 16,000 wakibaki bila makazi.

Taarifa za nchini humo zinaeleza kuwa shughuli za uokoaji zimeingia katika hatua ngumu zaidi baada ya siku tatu za mwisho kuonyesha kupungua kwa kasi ya kuokolewa kwa manusura.

Serikali imetangaza baada ya watu 5,380 kuokolewa katika siku mbili za mwanzo, ni watu wanne pekee waliopatikana wakiwa hai siku iliyofuata.

Meja Jorge Montanero, kiongozi wa timu ya uokoaji kutoka Ecuador, amenukuliwa na vyombo vya habari akisema hali ya matumaini imepungua kwa kiasi kikubwa.

“Tunaamini siku zimepita na wale tutakaowapata sasa watakuwa wamekufa,” amesema Montanero alipotembelea maeneo yaliyopata maafa.

Umoja wa Mataifa kupitia mratibu wake mkazi Caracas, Gianluca Rampolla, umeeleza hali ni ya wasiwasi mkubwa, ukikadiria maelfu ya mifuko ya kuhifadhi miili tayari inahitajika kutokana na ongezeko la miili inayotolewa kila siku chini ya vifusi.

“Tunaona mzigo mkubwa zaidi ya ule uliotarajiwa. Huduma za afya na vyumba vya kuhifadhia maiti vimeelemewa,” amesema Rampolla, akionya kuhusu hatari ya milipuko ya magonjwa katika maeneo yaliyoathirika.

Mashirika ya misaada yanasema hospitali nyingi zimeharibiwa vibaya na nyingine zimekosa wataalamu wa afya, hali inayozidisha hatari kwa majeruhi waliobaki.

Wakati huohuo, ongezeko la magonjwa ya kuambukiza linahofiwa kuanza kujitokeza kutokana na msongamano wa watu na miili katika maeneo ya makazi ya muda.

Kikosi cha uokoaji kutoka Marekani, Ecuador na Ureno kimepunguza operesheni zake katika baadhi ya maeneo baada ya kukosa dalili za manusura.

Katika mji wa Macuto, inaripotiwa kuwa jana Jumanne Juni 30,2026 operesheni zilisimama baada ya zaidi ya saa 40 za utafutaji bila mafanikio.

Mamlaka zinasema takriban majengo 59,000 yameharibiwa au kuporomoka kutokana na mitetemeko miwili mikubwa iliyopiga kwa sekunde chache.

Umoja wa Mataifa umetoa wito wa msaada wa dharura wa takriban Sh40 bilioni kwa ajili ya makazi ya muda, chakula na huduma za afya kwa zaidi ya watu 30,000 walioathirika, huku ukisisitiza hali inaweza kuwa mbaya zaidi iwapo msaada hautapatikana kwa haraka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *