Dar es Salaam. Dereva wa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Heche, Suez Maradafu, amefariki dunia katika nyumba ya wageni aliyokuwa amefikia mkoani Kigoma.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Philimon Makungu, amethibitisha kifo hicho leo Julai Mosi, 2026, akisema mwili wa marehemu umechukuliwa na kuhifadhiwa Hospitali ya Mkoa wa Kigoma, Maweni.

Amesema uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha kifo hicho.

Taarifa za kifo cha Maradafu zilitolewa awali na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Goluwa, aliyesema mwili wa marehemu ulikutwa ndani ya nyumba ya wageni aliyokuwa amefikia, ukiwa karibu na mlango wa chumba chake.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda Makungu amesema Maradafu alibainika amefariki dunia leo asubuhi baada ya watu waliokuwa naye kushindwa kumpata.

“Jana jioni alikuwa anamwendesha Heche, baadaye akaenda kulala. Asubuhi alipogongewa mlango hakuamka. Hatuwezi kueleza kilichomsibu hadi uchunguzi wa madaktari ukamilike,” amesema Makungu.

Alipoulizwa iwapo kuna mtu yeyote anayehisiwa kuhusika na tukio hilo, Kamanda Makungu amesema ni mapema kutoa hitimisho, akisisitiza kuwa uchunguzi bado unaendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *