Meneja wa zamani wa Manchester United na Real Madrid, Carlos Queiroz jana Jumatatu, Aprili 13, 2026 ametambulishwa rasmi kuwa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Ghana ‘Black Stars’.

Queiroz anajaza nafasi iliyo wazi baada ya kutimuliwa kwa Otto Addo wiki iliyopita kutokana na mwenendo usiovutia wa timu hiyo.

Taarifa ambayo imetolewa na Chama cha Mpira wa Miguu Ghana (GFA) imeeleza kuwa Queiroz anaanza majukumu yake haraka iwezekanavyo.

Kocha Mkuu wa kikosi cha timu ya taifa ya Ghana, Carlos Queiro. Picha na Mtandao

“Queiroz ana rekodi kubwa na ya kuvutia katika Kombe la Dunia. Aliiongoza Afrika Kusini kufuzu kwa Kombe la Dunia mwaka 2002, aliiongoza Ureno kufika hatua ya mtoano mwaka 2010, na aliisimamia Iran katika mashindano ya mwaka 2014 na 2018.

“Pia amewahi kushika nyadhifa za ukocha nchini Misri, Oman, Japan na Qatar, na anatarajiwa kutumia uzoefu wake mkubwa wakati wa Kombe la Dunia,” imefafanua taarifa ya GFA.

Muda mfupi baada ya Queiroz kutambulishwa, Kocha huyo ametoa shukrani zake za dhati huku akitoa ahadi ya kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri.

“Mpira wa miguu umenipa maisha yaliyojaa changamoto, mafunzo na safari zisizosahaulika kote ulimwenguni. Leo, ninakubali jukumu hili kwa ari na kujitolea vilevile vilivoniongoza katika taaluma yangu yote.

Sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Ghana. Picha na Mtandao

“Ghana ni taifa lenye vipaji, fahari na roho ya kipekee ya soka. Nafika nikiwa na heshima kwa historia yake na imani katika mustakabali wake. Kwa pamoja, kwa umoja, nidhamu na malengo makubwa, tutafanya kazi kuheshimu matarajio ya taifa kubwa la soka.

“Hii si kazi ya kawaida tu ni dhamira. Nipo tayari kutoa kila nilicho nacho katika uzoefu na maarifa yangu kwa mara nyingine tena, kwa ajili ya kuitumikia michezo na furaha ya watu,” amesema Queiroz.

Katika Kombe la Dunia 2026, Ghana imepangwa katika kundi L na timu za England, Croatia na Panama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *