Dar es Salaam. Kawaida mtu mwenye tabia ya kuongea kwa kulalamika kupita kisasi, mtaani humuita mtu mwenye gubu. Hili unaweza kusema ni jina linalomfaa kabisa Mussa Piliton “Baba Atu” ambaye ni mchekeshaji.
Kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii, jina Baba Atu siyo geni tena limekuwa miongoni mwa majina yanayotikisa kupitia video za ucheshi akimfanyia gubu mkewe aitwaye ‘Mama Atu’.
Akizungumza na Mwananchi Baba Atu ameeleza changamoto, maumivu na mapambano aliyokutana nayo katika safari yake ya kujitafuta kwenye Sanaa.
Baba Atu anasema kipaji chake cha uchekeshaji kilianza kujitokeza tangu akiwa shule ya msingi. Tofauti na wenzake walipenda michezo, yeye alijikuta akivutiwa zaidi na uchekeshaji.
“Nilikuwa nikisikia kuna burudani yoyote lazima niwepo. Hata nilipokuwa sekondari, wenzangu walikuwa wanakwenda kucheza mpira, mimi nilikuwa naenda kuwachekesha watu,” anasimulia.
Baada ya kumaliza kidato cha nne hakupata nafasi ya kuendelea na masomo kutokana na changamoto za kifamilia. Akaamua kuingia kwenye shughuli za kujitafutia kipato, ikiwamo kazi ya uchomeleaji wa vyuma.
Lakini mwaka 2018, alipopata simu, aliona ni wakati wa kujaribu bahati yake kwenye utengenezaji wa maudhui mtandaoni.
“Mwanzoni mapokezi yalikuwa ya kawaida, lakini mwaka 2019 nikaanza kuona mwanga,” anasema.
Anasema safari yake ilianza kupata mwanga baada ya kushiriki mashindano ya uchekeshaji ya Tulia Trust Comedy yaliyofanyika Mbeya mwaka 2023 na kuibuka mshindi wa kwanza.
Aidha mwaka uliofuata 2024 anasema akashinda tena mashindano ya Cheka Tu yaliyofanyika Mbeya. Ushindi uliomfungulia milango ya kuhamia Dar es Salaam ili kuendeleza ndoto zake za ucheshi na utengenezaji wa maudhui.
Chanzo cha jina Baba Atu
Anasema wazo la kuanzisha uhusika wa Baba Atu lilikuja 2025 baada ya kumaliza kurekodi kazi nyingine.
“Tulikuwa tumekaa tunakula, tukasema hapa kuna kitu tunaweza kufanya. Nikamwambia mwenzangu atakuwa Mama Atu, mimi Baba Atu. Niliposti video, lakini nilishangaa kuona watu wengi wakisema niendeleze. Nilipoingia mitandaoni nikakuta mapokezi makubwa. Hapo ndipo safari ya Baba Atu ilipoanzia.”
Anasema kabla ya Baba Atu tayari alikuwa amecheza nafasi mbalimbali ikiwamo jambazi, mchungaji na wahusika wengine. Lakini hakuna iliyopokelewa vizuri kama Baba Atu.
Urafiki na Mama Atu
Akizungumzia ushirikiano wake na Mama Atu, anasema walikutana kupitia Cheka Tu na kuanza kufanya kazi pamoja.
“Ni rafiki yangu wa karibu sana na mfanyakazi mwenzangu. Tumetoka mbali. Tunaheshimiana sana. Kuhusu mahusiano, siwezi kusema lolote kwa sababu lolote linaweza kutokea,” anasema.
Gubu lake mtaji
Wengi humfahamu Baba Atu kama mwanaume mwenye gubu na anayependa kufoka. Anasema sehemu kubwa ya tabia hiyo ni maisha halisi aliyokulia.
Amezaliwa Iringa katika jamii ya Wahehe lakini amekulia Mbeya kwa Wanyakyusa. Anasema watu wengi wa familia yake ni waongeaji, huku akimtaja baba yake.
“Mama yangu ni mpole, lakini naambiwa baba yangu alikuwa mtu wa kuongea sana lakini mama alikuwa hajibu kama anavyofanya mama Atu. Hata mimi hilo gubu lipo ndani yangu, ingawa kwenye kontenti naliongeza kidogo kwa ajili ya burudani,” anasema.
Anasema huwa haandiki skripti kama wanavyofanya wengi, bali anafanya kwa hisia na uhalisia.
Sababu watu kupenda maudhui ya Baba Atu
Kwa mujibu wa Baba Atu, siri kubwa ya mafanikio ya maudhui hayo ni kwamba yanaakisi maisha ya kila siku ya familia nyingi.
“Wanawake wengi wanasema Mama Atu ananilea sana. Wengine wananiambia wangekuwa wao wangenipiga hata na mwiko. Watu wanaona ni maisha yao ya kawaida, ndiyo maana wanapokea vizuri,”
Anasema mara nyingi hupata mawazo kutoka kwa watu wanaomwandikia ujumbe wakisimulia changamoto zao za ndoa, kisha yeye huzipanua na kuzigeuza kuwa maudhui ya vichekesho.
Changamoto kazini
Anakumbuka mwanzo Mama Atu alikuwa anapata wakati mgumu kuzoea kufokewa wakati wa kurekodi.
“Alikuwa anapaniki na kusema mbona namfokea kweli. Ilituchukua muda mpaka akaelewa kuwa ni sehemu ya kazi,” anasema
Anasema hata majirani na mwenye nyumba waliwahi kuamini kuwa wanagombana kweli, huku wengine wakimpigia simu wakimtaka aache kumtesa Mama Atu.
Tukio ambalo hatalisahau
Pamoja na mafanikio anayopata sasa, anasema kuna tukio moja lilimuumiza sana.
Anasimulia kuwa aliwahi kupata nafasi ya kutumbuiza kwenye tamasha la Cheka Tu ambalo lilihudhuriwa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete lakini baadaye mambo yaligeuka.
“Nilikuwa nimemtoa mama nyumbani aende akaangalie TV ili anione. Mwisho wa siku sikuchekesha. Nilijitahidi kukubali kuwa ni sehemu ya kazi, lakini mpaka leo nikikumbuka naumia. Rais alifika kwahiyo walichekesha wasanii wakubwa mimi niliambiwa nitachekesha lakini bahati mbaya muda uliisha kabla ya mimi kuchekesha,” anasema.
Katika ukuaji kwenye tasnia Baba Atu anasema bado hajafika anapotaka kufika.
“Namshukuru Mungu kwa kila hatua. Umaarufu umekuja, lakini siwezi kujivuna kwa sababu najua kesho anaweza akaja mtu mwingine. Ninachokiomba ni Mungu aendelee kunipa ubunifu,” anasema.
Anasema anachokipigania zaidi ni kuhakikisha kundi lao linaendelea kuwa imara na halivunjiki kutokana na mafanikio.
Mtazamo wake kuhusu ndoa
Kwa mtazamo wake, teknolojia na utandawazi ni miongoni mwa sababu zinazochangia kuvunjika kwa ndoa nyingi siku hizi.
Anaamini zamani watu walikuwa wanajifunza kuvumiliana zaidi. Huku sasa wengi wakikimbilia kuingia kwenye ndoa kabla hawajafahamiana vya kutosha.
“Siku hizi watu wanakutana mwezi tu wanaoana lakini hiyo ni tofauti na zamani watu walichunguzana. Licha ya hivyo utandawazi ni changamoto kubwa mwanamke hata akiwa na degree nne anatakiwa kuelewa yeye ni mke sasa wengi hawataki kukubali hilo,” anasema.
Baba Atu anaonya wasanii kuacha tabia ya kudharau wenzao.
“Mastaa wakubwa hawaonyeshi majivuno, lakini sisi ambao bado tunapambana ndiyo tunavimbiana. Hiyo ndiyo inayorudisha nyuma ukuaji wa tasnia ya komedi.”
Kisa cha Baba Atu kumsema mke wa mtu
Mbali na kutengeneza maudhui, anasema gubu lake limegeuka fursa.
Anasimulia kuna wanaume wanaomlipa fedha ili akawafokee wake zao kwa niaba yao.
“Kuna mzee aliniajiri nikavae uhusika wa mjomba nikamkanye mke wake maana siyo kila mwanaume ni muongeaji yaani nilikua jicho nyanya nilimsema mpaka mwanamke mwenyewe akasema hii ishu imekuwa siriazi.
“Nilifanya kazi hiyo na tangu hapo nikaanza kupata watu wengi wanaonitafuta kwa kazi kama hizo. Wengine tunafikia hata kuandikishiana mikataba,” anasema.
Anasema siyo tu kwenye ndoa ugomvi wowote ananunua hata masuala ya kijamii kama kumsema mtu mwenye tabia ya kutolipa hela ya taka au kufanya usafi kwenye nyumba za kupanga.