Kenya. Mwanamuziki wa Kenya Bien Aimé Baraza, amesema ‘Finale’ wimbo aliofanya na Alikiba uliandikwa miaka miwili iliyopita.
Akizungumza na Nation Lifestyle, Bien ameeleza kuhusu safari ya wimbo huo, kufanya kazi na mastaa wakubwa wa Afrika Mashariki, fedha katika muziki, pamoja na albamu yake mpya inayotarajiwa kutoka hivi karibuni
Amesema yeye pamoja na mtayarishaji wa muziki Abba waliandika wimbo huo ‘Finale’ miaka miwili iliyopita. Wimbo huo ulikuwa umehifadhiwa kwenye simu yake kwa muda mrefu.
Amesema waliurekodi wakiwa Tanzania, ambapo Abba pamoja na Darassa walikuwa studio siku hiyo. Wakati wa kurekodi, walimshauri amuite Alikiba kwa sababu ingekuwa na faida kibiashara.
Bien alimwita mara moja na Alikiba akakubali kushiriki. Baada ya kurekodi sehemu yake, wimbo huo uliendelea kubaki kwenye simu yake kwa sababu Bien alikuwa amepanga kuuongeza kwenye albamu yake itakayozinduliwa mwezi Juni.
Hata hivyo, baadaye aliona itakuwa vizuri kuuachia sasa. Ndani ya wiki mbili tu tangu utoke, bado unaendelea kufanya vizuri na ku-trend katika mitandao ya kijamii.
Kuhusu kiwango cha Alikiba
Bien amesema Alikiba ni mfano mzuri wa msanii anayejua kudumu kwa muda mrefu katika muziki.
Amesema mtu yeyote anayeielewa biashara ya muziki na suala la kudumu kwa muda mrefu ataelewa thamani ya Alikiba. Kulingana na Bien, Kiba hafanyi muziki kwa kutegemea hype au kiki kama ilivyo kwa baadhi ya wasanii.
Ameongeza kuwa katika tasnia ya muziki Tanzania kuna mambo mengi ya kiki, lakini Kiba amebaki kuwa yuleyule na msimamo wake. Bien amesema amejifunza mengi kutoka kwake, hasa utulivu wake, namna anavyojiendesha, pamoja na umuhimu wa kuwa na uthabiti katika kazi.
Kwa nini wimbo ulichelewa kutolewa?
Bien amesema kila kitu hutegemea muda sahihi. Kulikuwa na nyakati alitaka kuuachia wimbo huo lakini mazingira hayakuwa sahihi.
Amesema wakati fulani kulikuwa na matukio mengi ya kisiasa, hivyo akaamua kusubiri. Wakati mwingine Alikiba alikuwa anatoa wimbo mwingine, hivyo akaona si vizuri kutoa wao wakati huo. Kwa kifupi, kulikuwa na nyakati ambazo mmoja wao hakuwa tayari, hadi wakati huu ambapo wote walikuwa tayari ndipo wakaamua kuutoa.
Je, alijua ungekuwa hit?
Bien amesema mafanikio ya nyimbo nyingi hutegemea baraka za Mungu.
Amesema katika maisha yake ameandika nyimbo nyingi sana na tayari amewahi kuwa na hits kadhaa, lakini hana fomula maalumu ya kutengeneza hit. Kulingana naye, msanii huingia studio na kuandika nyimbo nyingi bila kujua ni ipi itakuwa maarufu, hivyo ni muhimu kuichukulia kila wimbo kana kwamba unaweza kubadilisha maisha yako.
Ujumbe wa ‘Finale’
Bien amesema wimbo huo unahusu hatua ya mwisho ya jambo fulani, ambapo mambo makubwa huwa yako hatarini.
Ujumbe wake ni kuwa watu wasijali sana maneno ya wengine bali wafuatilie malengo yao. Ndiyo maana katika wimbo huo wanasisitiza kauli ya “usilale leo”, wakimaanisha kuwa mtu anatakiwa kufanya kazi kwa bidii kufikia malengo yake.
Anasema unapofikia hatua ya mwisho ya jambo fulani, ina maana umeshinda vikwazo vingi njiani. Hivyo ujumbe wa wimbo huo ni kuendelea kujisukuma mbele na kusherehekea mafanikio.
Ushirikiano na wasanii wa Afrika Mashariki
Bien amesema ana nyimbo nyingi alizofanya na wasanii kutoka Rwanda pamoja na Tanzania.
Amesema baadhi ya nyimbo hizo zilirekodiwa miaka miwili au mitatu iliyopita na bado ziko kwenye mpango wa kutolewa. Ingawa kwa mashabiki zitaonekana mpya, ukweli ni kwamba zilirekodiwa muda mrefu uliopita.
Kuhusu kustaafu muziki
Bien amesema haoni kama ataacha muziki kabisa. Hata hivyo, anaamini nafasi yake katika tasnia inaweza kubadilika kadri muda unavyokwenda.
Kwa sasa yuko mstari wa mbele kama msanii, lakini baadaye anaweza kufanya kazi za nyuma ya pazia, kufundisha au hata kushiriki katika sera za muziki. Anasema muziki kwake si kazi tu, bali ni huduma, na anataka kuendelea kuutumikia kwa muda mrefu kadri atakavyoweza.
Albamu yake mpya
Bien anasema hii itakuwa albamu yake ya pili kama msanii binafsi, lakini bado hajui idadi kamili ya nyimbo zitakazokuwamo.
Amesharekodi zaidi ya nyimbo 40, hivyo bado anajadili na timu yake. Wenzake wanapendekeza albamu iwe na takribani nyimbo 12 ili iwe fupi na rahisi kwa wasikilizaji. Lakini yeye anaamini ana mambo mengi ya kusema, hivyo wanajaribu kupata uwiano kati ya matakwa ya mashabiki na ubunifu wake.
Mashabiki wategemee nini?
Bien anasema anaamini albamu hiyo inaweza kuwa moja ya albamu bora kabisa kutoka Kenya.
Anasema amekuwa akichunguza na kujifunza sauti za tamaduni mbalimbali nchini humo, kutoka maeneo kama Mount Kenya, pamoja na jamii kama Waluhya na Wakamba. Lengo lake ni kuunda muziki wa pop unaochanganya vionjo vya muziki wa asili wa Kenya.
Anasema wasanii wa Nigeria wamefanikiwa duniani kwa sababu muziki wao umejikita katika utamaduni wao, na anataka kufanya kitu kama hicho kwa muziki wa Kenya.
Chanzo chake kikubwa cha kipato
Bien anasema kipato chake kinatoka kwenye vyanzo mbalimbali.
Anapata fedha kupitia matangazo ya biashara (endorsements), miradi ya ubunifu, pamoja na kuwa balozi wa Basketball Africa League, jambo linalomfanya kusafiri mara nyingi hadi kwenye matukio yanayohusiana na National Basketball Association.
Pia anapata mapato kupitia majukwaa ya muziki kama YouTube, Spotify na Mdundo. Aidha, bado anapata mapato kupitia nyimbo za kundi la Sauti Sol pamoja na kampuni yao ya Sol Generation.
Kuhusu kufikisha miaka 40
Bien anasema kuzeeka si jambo baya. Anaamini kadri anavyoongeza umri, ndivyo anavyopata marafiki wengi zaidi, mitandao ya watu wengi zaidi, na fedha zaidi.
Anasema hana mpango maalum kwa miaka ya 40, bali ataendelea kuishi maisha yake kama kawaida.
Namna anavyosherehekea siku yake ya kuzaliwa
Bien anasema hupenda kukaa nyumbani siku yake ya kuzaliwa, kuagiza chakula, kula sana na kununua nguo mpya.
Pia anasema hapendi kupokea zawadi kwa sababu mara nyingi watu wanaotoa zawadi wanatarajia kitu kurudi kwao. Badala yake, huwa anawaomba watu wachangie kituo cha watoto yatima anachokisaidia.
Shinikizo la jamii kuhusu ndoa na watoto
Bien anasema haamini katika shinikizo la jamii kuhusu masuala ya ndoa na watoto.
Anaamini kila mtu anapaswa kuishi maisha yake kwa namna anayoona inafaa. Kama mtu anataka kupata watoto, ni sawa na kama hataki pia ni sawa.
Anasisitiza kuwa hakuna anayepaswa kuhukumiwa kwa maamuzi yake. Kwa maoni yake, muhimu zaidi ni kila mtu kupata furaha kwa njia inayomfaa yeye binafsi.