
Israel na Lebanon zimekubaliana siku ya Jumanne, Aprili 14, kuendelea na mazungumzo kuelekea amani ya kudumu kufuatia mazungumzo yaliyoonekana kuwa na tija huko Washington kati ya wawakilishi wa nchi hizo mbili, ya kwanza ya aina yake tangu mwaka 1993. Haya ni mafanikio katika upande wa kidiplomasia.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Pande zote zimekubaliana kuanza mazungumzo ya moja kwa moja katika tarehe na mahali ambapo pande zote zitakubaliana,” Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imeeleza katika taarifa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, ambaye alikutana na Balozi wa Israel Yechiel Leiter na Balozi wa Lebanon Nada Hamadeh Moawad, hapo awali alipongeza “fursa ya kihistoria” kwa Lebanon na Israel kufanya amani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio anaonya kwamba “mazungmzo si ya siku moja na yatachukua muda.”
Mkutano wa Jumanne ulidumu kwa zaidi ya saa mbili. “Tuligundua leo kwamba tuko upande mmoja,” balozi wa Israel aliwaambia waandishi wa habari. “Sote tumeungana katika nia yetu ya kuikomboa Lebanon” kutoka kwa kundi la Washia la Hezbollah, lnalounga mkono Iran, aliongeza. Mwenzake wa Lebanon alielezea “mkutano wa maandalizi” kama “wenye kujenga” na kutoa wito wa kusitisha mapigano kati ya Israel na Hezbollah.
Hezbollah, ambayo haikushiriki katika mkutano huo, iliita majadiliano hayo “kujisalimisha” na kudai kuhusika kwa mashambulizi ya roketi kwenye miji kumi na mitatu ya mpakani mwa Israel.
“Itachukua muda”
Ingawa upande wa Iran utulivu umetawala tangu makubaliano ya usitishaji mapigano yalipoanza kutekelezwa Aprili 8, Lebanon haijajumuishwa katika makubaliano hayo, kulingana na Israel, ambayo inaendelea kuishambulia Hezbollah na haijajiondoa kutoka kusini mwa nchi.
Rais wa Lebanon Joseph Aoun amesema anatumai mazungumzo huko Washington yataashiria “mwanzo wa mwisho wa mateso ya raia wa Lebanon.” Lakini “utulivu hautarejeshwa kusini mwa Lebanon ikiwa Israel itaendelea kuchukua udhibiti wa maeneo kusini mwa nchi,” ameongeza.
Majadiliano ya Jumanne yalilenga “kufafanua mfumo ambao amani ya kudumu inaweza kujengwa,” alisema Marco Rubio. “Mazungumzo haya si ya siku moja; yatachukua muda.” “Ni wakati wa Israel na Lebanon kufanya kazi pamoja,” alisihi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliweka masharti mawili: kupokonywa silaha kwa Hezbollah na kutafuta “makubaliano ya kweli ya amani,” kwani nchi hizo mbili zimekuwa vitani kwa miongo kadhaa.
Israeli haitaki Ufaransa kushirikishwa katika mazungumzo
Balozi wa Israel nchini Marekani siku ya Jumanne alikosoa jukumu la Ufaransa nchini Lebanon, akisema kwamba Paris haikuwa na shughuli yoyote katika mazungumzo kati ya Israel na Lebanon. Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Israel na Lebanon huko Washington, Yechiel Leiter alisema: “Ni hakika kwamba hatutaki kuona Ufaransa ikiingilia mazungumzo haya.”