Uhondo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya utaendelea tena leo kwa mechi za marudiano ya robo fainali ambapo katika dimba la Alianz Arena, Ujerumani, vigogo wawili watakutana kutafuta nafasi ya kwenda nusu fainali.
Wenyeji Bayern Munich watakuwa na faida ya kucheza nyumbani baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 ugenini wiki iliyopita wakati wapinzani wao Real Madrid watakuwa na kibarua cha kupindua matokeo na kujihakikishia kutinga nusu fainali.
Hata hivyo, Madrid hawajapoteza michezo yao minne ya mwisho ambayo walicheza ugenini dhidi ya Bayern ambapo walishinda mara tatu na kutoka sare mechi moja.
Jijini London, England, Arsenal wataikaribisha Sporting CP kwenye dimba la Emirates. Katika mechi ya kwanza iliyopigwa Ureno, Washika Mitutu hao wa London waliondoka na ushindi wa bao 1-0 na leo wana kibarua kingine cha kuhakikisha wanatinga nusu fainali.
Akizungumza na vyombo vya habari kuelekea katika mchezo huo, meneja wa Arsenal, Mikel Arteta amewataka wachezaji wake kucheza bila hofu katika mchezo huo. Kauli hiyo inakuja wakati presha ikiongezeka kwa miamba hiyo ya London Kaskazini kufuatia matokeo mabaya, ikiwemo kupoteza fainali ya Kombe la Carabao dhidi ya Manchester City, kutolewa katika Kombe la FA na Southampton na kichapo cha nyumbani dhidi ya Bournemouth.
Matokeo hayo yameifanya Arsenal kukaribia kumaliza msimu wa sita mfululizo bila taji. Hata hivyo, Arteta amesema bado wana nafasi kubwa ya kubadili hali hiyo.
Meneja Mkuu wa Arsenal, Mikel Arteta. Picha na Mtandao
“Hakuna hofu, ni motisha tu. Hiyo ndiyo ninayotaka kuona kwa wachezaji na mashabiki,” amesema Arteta.
Hata hivyo, timu hiyo inakabiliwa na changamoto ya majeruhi, huku Declan Rice, Bukayo Saka, Martin Ødegaard na Jurrien Timber wakikosa mazoezi.
Mshindi wa jumla kati ya Arsenal au Sporting CP atakutana na Atletico Madrid ambayo jana iliitupa nje Barcelona wakati mshindi wa jumla kati ya Bayern au Madrid atakutana na PSG ambayo jana ilitinga nusu fainali kwa kuitoa Liverpool.