Shirika la Afya Duniani limetangaza kuanza kwa majaribio ya dawa zinazoweza kutibu aina ya virusi vinavyosababisha mlipuko wa sasa wa ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kuwa mgonjwa wa kwanza tayari ameandikishwa kushiriki katika majaribio hayo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kwa mujibu wa WHO, zaidi ya watu 1,400 wameambukizwa huku 438 wakithibitishwa kufariki dunia kutokana na mlipuko huo.

Kwa sasa hakuna chanjo au tiba iliyoidhinishwa dhidi ya aina ya virusi vya Bundibugyo, ambayo ni mojawapo ya aina za virusi vya Ebola na huambukiza kwa urahisi.

Utafiti huu unafadhiliwa na WHO na unaratibiwa kwa ushirikiano kati ya Institut National de Recherche Biomédicale, Institute of Tropical Medicine na University of Oxford.

Katika majaribio hayo, wagonjwa watapewa dawa mbili za kuzuia virusi (antiviral) ili kupima ufanisi wake.

Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Shirika la Afya Duniani (WHO) mjini Geneva, Tedros alisema:

“Hata bila tiba zilizoidhinishwa, baadhi ya watu wanapona ugonjwa huu. Hata hivyo, tunaweza kuokoa maisha mengi zaidi ikiwa tutakuwa na tiba salama na zenye ufanisi.”

Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Samuel Roger Kamba, amesema kuanza kwa majaribio hayo ni hatua muhimu ya maendeleo, inayotoa matumaini mapya kwa wagonjwa, familia zao na jamii zilizoathirika.

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, mlipuko wa virusi vya Ebola huenda ukaligharimu bara la Afrika kiasi cha dola za Marekani bilioni 3.6 pamoja na maelfu ya ajira na pengine kusababisha mzozo wa kimaendeleo kwenye bara hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *