Mkuu wa shirika la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa Volker Turk ametahadharisha juu ya janga jingine la haki za binaadamu katika mji wa al-Obeid, nchini Sudan na kuutolea wito ulimwengu kuchukua hatua haraka iwezekanavyo.

Turk amesema hayo mjini Geneva wakati wa mjadala wa dharura wa baraza la haki za binadamu la umoja huo kuhusiana na hali kwenye eneo hilo na kuongeza kuwa, ishara ziko wazi kwamba janga hilo linatokea Sudan na wakati huu katika makao makuu ya jimbo la kimkakati la Kordofan Kaskazini.

Mjadala huo uliitishwa na Ulingereza, ambayo ujumbe wake hapo kabla ulitahadharisha kuhusu hatari ya ukatili mkubwa kufuatia ripoti kwamba wanamgambo wa RSF na washirika wake wanapeleka wapiganaji kuuzunguka jiji la al-Obeid, hatua inayoweza kusababisha kuongezeka kwa mzozo.

Turk amewaambia wajumbe kwamba raia wamekuwa wakiishi katika hali ya mzingiro kwa miezi 18 wakikabiliwa na upungufu mkubwa wa maji safi na mashambulizi yasiyokoma ya droni huku jeshi la Sudan likipambana kudhibiti maeneo yanayounguka mji huo.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limesema katika ripoti yake kwamba, Kikosi cha Msaada wa Haraka nchini Sudan (RSF) kilitenda uhalifu dhidi ya ubinadamu na maangamizi ya kikabila wakati wa mashambulizi yake katika mji wa El-Fasher kati ya 2024 na 2025.

Shirika hilo lisilo la kiserikali limewahoji waathiriwa au mashahidi 247 kati ya mapema mwaka 2024 na Oktoba 2025 huko Darfur Kaskazini.

Limesema RSF ilishambulia kwa makusudi vitongoji vya kandokando ya El Fasher ambavyo vilikuwa makazi ya watu wa Zaghawa huko magharibi mwa Darfur.

Ripoti hiyo imedai kwamba ukatili mkubwa na wa kupanga ulifanyika dhidi ya watoto ikiwa ni pamoja na mauaji, utekaji nyara, kuajiriwa kwa kulazimishwa na ubakaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *