Makubaliano hayo yaliyowekwa saini Aprili 8, 2026, yanalenga kutambua madini ya ujenzi na viwandani yaliyosahaulika, kukuza ujenzi usioharibu mazingira na kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Katika Kituo cha mafunzo ya usanifu majenzi cha TAWAH, kilichopo kijiji cha Mhaga, Kisarawe mkoani Pwani, viongozi waandamizi wa mashirika wa TAWAH na UNDP na wasichana wenye ari ya kuwa wasanifu majenzi wamekusanyika bila kujali mvua kubwa iliyokuwa inanyesha.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP nchini Tanzania yawaunga mkono wanawake kuendeleza ujenzi wenye mnepo.
Ushirikiano huu unalenga kuleta mageuzi makubwa kwa kutumia rasilimali za ujenzi zinazopatikana eneo hili, ikiwemo udongo, mawe, na mchanga ili kutengeneza nyumba bora na za gharama nafuu. Msimamizi miradi wa TAWAH, Joyce Saidi anaeleza.
“Tunayo furaha kubwa sana kwa siku ya leo ambapo TAWAH imesaini makubaliano ya miaka mitatu na UNDP Tanzania kwa ajili ya kuendeleza yale mafunzo tunayofanya kwa wanawake hususan kwenye madini ya ujenzi yaliyosahaulika, ambapo sisi tunatumia udongo.”
Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Tanzania, Shigeki Komatsubara, akafunguka kuhusu makubaliano hayo akisema, ni zaidi ya karatasi. Ni mwitikio wa vitendo kwa changamoto tatu zinazotukabili: hitaji la haraka la nyumba zinazohimili mabadiliko ya tabianchi, umuhimu wa kulinda mazingira katika ujenzi, na kutanua fursa za kiuchumi kwa wanawake na makundi yasiopewa kipaumbele.”
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP nchini Tanzania yawaunga mkono wanawake kuendeleza ujenzi wenye mnepo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TAWAH, Victoria Heilman, ambaye aliwahi kuwa Mhadhiri Chuo Kikuu cha Ardhi anasema,
“Nia yetu ni kuangalia hii taasisi ni jinsi gani itasaidia wanawake hasahasa huku vijijini kuweza kufanya kitu kwa kuboresha maisha yao. Sasa tumejiunga ili kutumia taaluma zetu, kama wasanifu majenzi, au wahandisi. Sasahivi tunafundishana jinsi gani ya kutumia udongo ambao tunauchimba hapahapa kijijini kwetu. Kutengeneza tofali ambazo ni imara na vilevile kujenga nyumba”
Godfrey Nyamrunda, Mwakilishi wa UNDP huko Zanzibar na Meneja Mradi wa kuendeleza madini yaliyopuuzwa kama yale ya ujenzi na viwandani amezungumzia ushirikiano wao na TAWAH..
“Tumeingia makubaliano na wenzetu wa TAWAH ambao wao wamebobea katika masuala ya ujenzi wa usanifu wa miundombinu na majengo lakini sisi tumebobea upande wa kuendeleza haya madini ya ujenzi na madini ya viwandani.”
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP nchini Tanzania yawaunga mkono wanawake kuendeleza ujenzi wenye mnepo.
Wanufaika ni familia zenye hali duni na hawalipi chochote. Baada ya mafunzo ya miezi minne, wahitimu wanapelekwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini Tanzania, VETA, huko wanapata vyeti rasmi vinavyotambuliwa na Serikali.
Umri wa wasichana hawa ni miaka 18 hadi 35, hususan walioshindwa kupata elimu rasmi, kutoka pande zote za Tanzania, mmoja wao anatupatia simulizi yake.
“Ndoto yangu mimi kubwa ni kuwa mfanisi majengo, kwahiyo hapa nimekuta wanajenga nikashawishika, halafu wanajenga vitu vizuri na kuna elimu kubwa zaidi, nikaamua nije nianzie hapa safari yangu ya kuwa mfanisi majengo.”
Tangu mwaka 2021 hadi sasa, mradi huu umetoa mafunzo kwa wanawake 140, ambapo 50 miongoni mwao wamepata vyeti vya VETA, huku nyumba 17 tayari zimejengwa.