Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa Katika eneo la Maziwa Makuu Huang Xia na Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake UN Women Sima Bahous wametoa tarifa mbele ya wajumbe wa Baraza hilo kuhusu kuongezeka kwa ghasia hivi karibuni.
Licha ya juhudi za upatanishi mjini Doha na Washington, mvutano wa kikanda kati ya DRC, Rwanda na Burundi unaendelea kuwa mkubwa.
Huang Xia, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Eneo la Maziwa Makubwa, akitoa taarifa kwenye mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali katika Eneo hilo.
Huang Xia: Mgogoro wa DRC wazidi kuwa mbaya
“Ningependa kuleta habari njema kuhusu mgogoro unaotikisa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na eneo zima lakini mambo ni kinyume,” amesema Huang Xia, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu kwa eneo la Maziwa Makuu.
Tangu Oktoba mwaka jana, licha ya kuongezeka kwa juhudi za kidiplomasia, “hali ya kibinadamu na usalama imezidi kuwa mbaya kwa kiwango cha kutia wasiwasi”.
Amesema kuporomoka kwa imani kunachangia pengo kati ya ahadi za kisiasa na hali halisi kwenye uwanja wa mapambano. “Tofauti hii ndiyo changamoto yetu kuu ya pamoja,” amesisitiza.
Katika muktadha huo, ametaja michakato ya Washington na Doha pamoja na juhudi za Afrika kuwa zimefungua “fursa mpya”.
Ingawa kutiwa saini kwa Makubaliano ya Washington tarehe 4 Desemba 2025 kulikuwa hatua muhimu, kutekwa kwa Uvira na kundi la M23 siku chache baadaye kulikuwa na athari kubwa kwa raia na uhusiano wa kikanda.
Hata hivyo, amekaribisha kurejelewa kwa mazungumzo Washington, DC tarehe 17 na 18 Machi, yaliyosababisha hatua kadhaa za vitendo, ikiwemo kubainishwa kwa maeneo ya operesheni za kundi la FDLR.
Mgao wa chakula cha dharura unasambazwa kwa watu waliokimbia makazi yao huko Goma.
Hatari ya migogoro ya kijamii
Katika ziara yake ya hivi karibuni, amesema aliarifiwa kuwa operesheni dhidi ya FDLR zinaandaliwa, huku mamlaka za Congo na ujumbe wa MONUSCO zikishuhudia wanajeshi wa M23 wakiondoka katika baadhi ya maeneo.
Doha, kuanzishwa kwa mfumo wa kufuatilia na kuthibitisha usitishaji vita pamoja na kupitishwa kwa masharti ya uendeshaji wa mfumo uliopanuliwa, kulitajwa kuwa “maendeleo makubwa”.
“Gharama ya kibinadamu ya mgogoro huu wa muda mrefu bado haiwezi kuvumilika,” amesisitiza mjumbe huyo, akibainisha kuwa mamilioni ya watu wamekimbia makazi yao na wanakabiliwa na uhaba wa chakula, pamoja na ongezeko la ukatili wa kijinsia na mashambulizi dhidi ya wahudumu wa misaada.
Ameonya pia kuhusu “ongezeko la kutia wasiwasi” la kauli za chuki na mgawanyiko wa kijamii unaotegemea utambulisho, hali inayochochea visasi na kuvunja mshikamano wa kijamii.
“Hali hii inatishia kugeuza mgogoro wa sasa wa usalama kuwa vita hatari zaidi yenye sura ya kijamii,” ameonya.
Wanawake ni muhimu kwa amani Maziwa Makuu: UN Women
“Fursa za uongozi wa wanawake kwa ajili ya amani katika eneo la Maziwa Makuu ni za kipekee na zinaweza kubadilisha hali,” amesema Sima Sami Bahous, Mkurugenzi Mtendaji wa Shitrika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake UN Women akihutubia Baraza hilo la Usalama.
Sima Sami Bahous, Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women, anatoa taarifa kwa Mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali katika Eneo la Maziwa Makuu.
Amekumbusha Baraza kuwa azimio la kwanza kuhusu wanawake, amani na usalama mwaka 2000 lilichochewa kwa sehemu na msaada wa Nelson Mandela kwa wanawake wa Burundi kushiriki kikamilifu katika kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe.
“Mapendekezo yao, mawazo yao na nguvu zao zilijumuishwa katika makubaliano ya Arusha,” amesema. Vita vilimalizika na leo Burundi ina moja ya viwango vya juu vya uwakilishi wa wanawake katika siasa katika eneo hilo.
Ameongeza kuwa wanawake wengi wanahusika katika juhudi za upatanishi ngazi ya jamii ili kuzuia migogoro midogo isigeuke kuwa mikubwa.
“Amani katika eneo hili inategemea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,” amesisitiza Bi. Bahous akiongeza kuwa amani itapatikana tu pale wanawake watakapotambuliwa kama wadau muhimu wa utulivu na si “nyara za vita”.
Mamlaka muhimu ya MONUSCO lazima ilindwe
Bi. Bahous amesema eneo la Maziwa Makuu lina mazingira mazuri kwa uongozi wa wanawake, huku nchi 11 kati ya 12 za Mkutano wa Kimataifa wa Maziwa Makuu zikiwa na mipango ya kitaifa kuhusu wanawake, amani na usalama.
“Fursa ipo,” amesema. “Faida zake zinaweza kubadilisha mchezo kabisa.”
Amehimiza Baraza la Usalama kuunga mkono wito wa uwakilishi sawa wa wanawake katika juhudi za amani nchini DRC na kwingineko.
Aidha, amesisitiza kuwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani DRC, MONUSCO na mamlaka yake muhimu lazima ulindwe.
Ametaja mamia ya kesi dhidi ya wahusika wa ukatili wa kijinsia unaohusiana na migogoro, pamoja na asilimia 60 ya watetezi wa haki za binadamu wanawake katika jimbo la Kivu Kaskazini wanaoripoti vitisho vya moja kwa moja, kama ushahidi wa umuhimu huo.
Pia ametoa wito wa kuungwa mkono kwa mashirika ya kiraia yanayoongozwa na wanawake na kulindwa kwa nafasi ya kiraia.
“Tunawadaiwa na wanawake wa eneo la Maziwa Makuu kufanya kila juhudi zetu zilizo bora,” amesisitiza.