Trump aashiria “mpango maalum” kuhusu Mashariki ya KatiTrump aashiria “mpango maalum” kuhusu Mashariki ya Kati

Trump na matumaini mapya

Rais Trump alisema Jumapili kwamba “kuna nafasi ya kweli ya ukuu katika Mashariki ya Kati,” akieleza kupitia mtandao wake wa Truth Social kwamba pande zote “zimekubaliana kwa mara ya kwanza” na kwamba “tutalifanikisha.”

Kauli hiyo imekuja siku moja kabla ya Netanyahu kuwasili White House kwa mazungumzo yanayotarajiwa kuangazia vita vya Gaza na suala la Palestina. Trump tayari amedai kwamba “anaona mpango” wa kumaliza mapigano na kuwarejesha mateka nyumbani.

Katika hotuba yake kwenye Umoja wa Mataifa wiki iliyopita, Netanyahu alikataa wazo la kuundwa kwa taifa la Palestina na kusisitiza kuwa Israel “lazima imalize kazi” dhidi ya Hamas, licha ya mataifa mengi ya Magharibi kutangaza kutambua taifa la Palestina.

Vita vya Gaza vilizuka baada ya mashambulizi ya Hamas Oktoba 7, 2023 ambayo yaliua watu 1,219 nchini Israel na kuwateka 251. Kati ya mateka hao, 47 bado wanashikiliwa Gaza, ikiwemo 25 ambao jeshi la Israel linasema wamefariki.

Kwa upande wa Wapalestina, Wizara ya Afya ya Gaza inayoongozwa na Hamas imesema zaidi ya watu 65,500, wengi wao raia, wameuawa katika mashambulizi ya Israel, idadi ambayo Umoja wa Mataifa unaiona kama inayoaminika.

Mfalme Abdullah wa Jordan pia amesema maelezo ya awali ya mpango wa Trump “yanaendana na yale yaliyokubaliwa” katika majadiliano ya kimataifa, ingawa hakutoa maelezo zaidi.

Marekani Washington 2025 | Benjamin Netanyahu na Donald Trump katika mkutano Ikulu ya White House
Benjamin Netanyahu na Donald Trump katika mkutano Ikulu ya White House Aprili 07, 2025.Picha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Shinikizo kwa Netanyahu

Hata hivyo, Netanyahu anakabiliwa na shinikizo kali kutoka ndani ya serikali yake ya muungano wa mrengo mkali wa kulia. Viongozi wa walowezi na mawaziri kama Itamar Ben-Gvir na Bezalel Smotrich wanataka Israel kuendeleza vita hadi Hamas ishindwe kabisa na pia kutwaa baadhi ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi.

Ben-Gvir alisema Netanyahu “hana mamlaka ya kusitisha vita bila ushindi kamili,” huku Smotrich akitoa masharti matatu: Hamas ivunjwe na silaha zake ziondolewe, Mamlaka ya Palestina isipate nafasi ya kuongoza Gaza wala Ukingo wa Magharibi, na Israel inyakuwe maeneo ya Ukingo wa Magharibi bila kutambua taifa la Palestina.

Kwa mujibu wa ripoti ya Times of Israel, Trump anapanga kumpa Netanyahu mpango wa hatua 21 unaojumuisha kuachiliwa kwa mateka wote waliobaki kwa kubadilishana na mamia ya wafungwa wa Kipalestina, pamoja na kuondoka kwa hatua kwa hatua kwa wanajeshi wa Israel kutoka Gaza.

Mpango huo pia unataja kuundwa kwa serikali ya mpito badala ya Hamas au Israel kutawala moja kwa moja Ukanda wa Gaza, jambo ambalo limeibua upinzani mkubwa miongoni mwa wafuasi wa mrengo wa kulia wa Israel.

Kwanini Israel inayashambulia majengo Gaza City?

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Licha ya upinzani huo wa ndani, jumuiya ya kimataifa imesisitiza suluhu ya mataifa mawili kama njia ya kudumu ya amani. Netanyahu, hata hivyo, amekuwa akikataa waziwazi wazo hilo.

Israel ilitwaa Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki mwaka 1967, na sasa zaidi ya walowezi 700,000 wa Kiyahudi wanaishi katika maeneo ambayo Wapalestina wanataka yawe sehemu ya taifa lao la baadaye.

Macho yote yako kwenye mkutano wa White House, ambapo Trump na Netanyahu wanatarajiwa kuweka wazi iwapo kutakuwa na mabadiliko ya kweli kuelekea kusitishwa kwa vita, au endapo shinikizo la kisiasa na kijeshi litaendelea kuongeza mgawanyiko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *