Mwanachama wa ngazi ya juu wa harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Ansarullah nchini Yemen amemhimiza Rais wa Marekani Donald Trump kujiepusha na maamuzi ya uchochezi na kuheshimu haki za mataifa ya Kiislamu, akimwonya yeye pamoja na washirika wake kuhusu uwezekano wa kufungwa kwa Lango Bahari la Bab el Mandeb.

Hossein al‑Ezzi amesema katika ujumbe aliouchapisha kwenye akaunti yake ya X siku ya Jumamosi kwamba: “Iwapo Sana’a itachukua uamuzi wa kufunga Lango Bahari la Bab el‑Mandeb, hakuna yeyote atakayeweza kulifungua tena.”

Aliongeza kuwa: “Kwa hivyo, Trump na washirika wake ni vyema wakomeshe hatua na sera zote zinazozuia kurejeshwa kwa amani. Wanapaswa kuonyesha heshima kwa haki za mataifa ya dunia na kwa Umma wa Kiislamu.”

Awali, Waziri wa Ulinzi wa Yemen, Brigedia Jenerali Mohammed al‑Atifi, alisema kuwa majeshi ya nchi hiyo yako katika kiwango cha juu kabisa cha utayari na yako tayari kikamilifu kukabiliana na aina yoyote ya uchokozi dhidi ya ardhi ya Yemen.

Amesema kwamba mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yameonyesha kwa uwazi umuhimu wa umoja kati ya safu za muqawama (mapambano ya Kiislamu), na pia kuthibitisha ufanisi wa operesheni za kijeshi zinazotekelezwa na wapiganaji wa kile kinachoitwa Mhimili wa Muqawama.

Mnamo tarehe 28 Machi, Jeshi la Yemen lilitangaza kuwa lilishambulia malengo nyeti ya Israel katika sehemu za kusini za maeneo yanayokaliwa kwa mabavu kwa kutumia makombora ya balistiki, likionyesha kuwa taifa hilo la Kiarabu limeingia rasmi vitani ili kuitetea Iran wakati wa mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel.

Jeshi la Yemen lilisema katika taarifa kwamba hatua hiyo ilikuwa sambamba na tangazo la awali la Yemen kuhusu kuingilia moja kwa moja kijeshi kwa ajili ya kuunga mkono Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na pia safu za muqawama huko Lebanon, Iraq na Palestina.

Lango Bahari wa Bab el‑Mandeb ni njia nyembamba ya maji iliyopo kati ya Yemen katika Rasi ya Uarabuni na nchi za Djibouti na Eritrea katika Pembe ya Afrika. Njia hii inaunganisha Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden pamoja na Bahari ya Hindi. Ni mojawapo ya njia muhimu sana za kimkakati duniani kwa usafiri wa baharini, kwa sababu inaunganisha njia ya Mfereji wa Suez na njia kuu za usafirishaji wa kimataifa. Sehemu kubwa ya biashara ya dunia, ikiwemo mafuta, gesi na bidhaa zinazosafiri kati ya Ulaya na Asia, hupitia katika mlango huu wa bahari. Kwa hiyo, usumbufu wowote katika Bab el‑Mandeb unaweza kuathiri sana biashara ya kimataifa, gharama za usafirishaji wa meli, na usambazaji wa nishati, na kuifanya kuwa eneo nyeti kwa usalama wa kimataifa na uthabiti wa uchumi wa dunia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *