
Serikali ya DRC na waasi wa M23 wamekubaliana kuruhusu kupitishwa kwa misaada ya kibinadamu na kubadilishana wafungwa ndani ya siku 10 zijazo, hii ni kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa mjini Geneva, Uswis.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, serikali ya Kinshasa na waasi hao wamekubaliana kuhakikisha misaada muhimu ya kibinadamu inawafikia raia wenye uhitaji bila masharti na kwa kuzingatika sheria za kimataifa.
Taarifa imeongeza kuwa, kila upande utajiepusha na vitendo ambavyo kwa namna moja au nyingine vitakwamisha misaada ya kibinadamu kufika kwa wakati kwenye eneo la mashariki mwa nchi.
Aidha pande hizo zilitiliana saini makubaliano kuhusu mifumo ya uthibitishaji wa kusitisha mapigano ili kuanza kufanya ufuatiliaji, uhakiki na kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wake.
Licha ya pande hizo kutia saini makubaliano ya Qatar na yale ya mwezi Desembamwaka jana jijini Washington, bado kunaripotiwa mapigano ambayo yamesababisha maelfu ya raia kuendelea kukimbia maeneo yao.
Tangu mwaka 2021, waasi hao wanaosaidiwa na Rwanda, wanadhibiti maeneo makubwa ya mashariki mwa nchi ya DRC, eneo ambalo linashuhudia machafuko kwa zaidi ya miaka 30 sasa.
Mazungumzo ya Uswis, yalianza April 13 hadi 17 na kuhudhuriwa wajumbe kutoka Qatar, Marekani, Uswisi, Togo, kamishna wa umoja wa Afrika pamoja na wapatanishi wake.