
ILIPOISHIA
“Tuombee tumkute mzima. Mimi niko tayari kugharamia matibabu yake hata kama atapelekwa nje ya nchi”
“Unadhani ni kwanini dereva wako alimshambulia yule kijana?”
“Sijui. Na mpaka sasa sina hakika kwamba ni yeye aliyefanya kitendo hicho”
“Watumishi wa gesti walimuona na gari alilotumia walilikariri namba zake”
“Mlipomuhoji dereva wangu alisema nini?”
SASA ENDELEA…
“Anakanusha kwamba hakufanya kitendo hicho. Anachokubali yeye ni kugonga mtu tu.”
“Inawezekana watu walioona hilo gari walikosea namba. Hawakulikariri vizuri. Dereva wangu si jambazi. Kwanza atapata wapi bastola?”
“Bastola zinapatikana. Kwani majambazi wanazipata wapi? Kuna watu wanamiliki silaha kinyume cha sheria na kuna wengine wanazikodisha.”
“Hata kama watakwenda kupekua nyumbani kwao, hawatapata kitu. Watajisumbua bure.”
“Hawajisumbui bure. Wako kazini. Hata kama hawataipata hiyo bastola, tutajua ameificha mahali na tutambana hadi atatuambia ameificha wapi.”
Wakwetu aliishia kuguna.
Walipofika hospitalini walipelekwa katika chumba alichokuwa amelazwa Masumbuko. Wakwetu alimuona. Kijana huyo alikuwa bado katika hali mbaya.
Wakwetu akazungumza na daktari aliyekuwa akimtibu Masumbuko.
“Hali yake inaendeleaje?” akamuuliza.
“Hali yake ni kama unavyoiona. Tunajitahidi kumsaidia kadiri itakavyowezekana.”
“Mimi niko pamoja na nyinyi. Niko tayari kugharamia matibabu yake kwa kiasi chochote kile. Kama kuna kifaa kitahitajika au dawa, msisite kuniambia. Nitakuwa ninamtembelea kila siku kujua hali yake inavyoendelea,” Wakwetu alimwambia daktari huyo ambaye alichukua namba ya simu ya Wakwetu.
Wakati wako kwenye gari wakirudi, Inspekta Amour alimwambia Wakwetu.
“Ni kitendo cha ubinadamu kumsaidia yule kijana asiye na hatia.”
“Nimeamua kumsaidia kwa gharama yoyote ile ili kuokoa maisha yake.”
“Kama atapona, dereva wako atapata ahueni. Kosa la mauaji litamuepuka.”
“Mtamuachia kabisa?” Wakwetu akamuuliza Inspekta huyo.
“Hatuwezi kumuachia kabisa. Tutamfungulia shitaka la kujaribu kuua na kujeruhi.”
“Sasa hapo kuna ahueni gani?”
“Ahueni ipo. Shitaka la mauaji ni kubwa sana kuliko shitaka jingine lolote katika makosa ya jinai. Shitaka la kujaribu kuua ni dogo. Mahakama inaweza kukuachia kama utajitetea vizuri. Na kama ni adhabu, itakuwa kifungo, na pia mahakama inaweza kutoa dhamana wakati kesi inaendelea.”
“Sawa. Nitajiandaa kumuwekea wakili wa kumtetea.”
“Ni mapema mno. Subiri kwanza kesi ifike mahakamani.”
Walipofika kituo cha polisi walimkuta James amerudishwa kituoni hapo.
Inspekta Amour akazungumza na polisi mmojawapo miongoni mwa polisi waliokwenda kumpekua James.
“Je, mmefanikiwa?” alimuuliza.
Polisi huyo akatikisa kichwa.
“Hatukufanikiwa,” akasema na kuongeza,
“Hatukupata kitu.”
“Hamkupata ile bastola?”
“Hatukuipata. Inawezekana ameificha mahali pengine.”
“Je, pesa? Hamkukuta pesa ambazo zinatia mashaka kuwa ni za wizi?”
“Hatukukuta.”
“Kwanini?”
“Mtu mwenyewe anaishi maisha duni sana. Chumbani kwake kuna kitanda tu. Kama ni ujambazi, atakuwa anauanza sasa.”
“Hana akaunti ya benki?”
“Tumemuuliza, amesema hana akaunti.”
Inspekta Amour akabaki kimya akiwaza.
“Wakati wote anasisitiza kuwa si yeye aliyehusika katika lile tukio,” polisi huyo aliendelea kumwambia Inspekta Amour.
“Mliwauliza watu anaoishi nao kuhusu tabia zake?”
“Tumewauliza. Wamemtetea sana. Wamesema James ni kijana mwenye tabia nzuri sana kiasi kwamba hawaamini kama anaweza kumpiga mtu risasi.”
“Kwa hiyo mna wazo gani?”
“Wazo letu ni kumfikisha mahakamani kesho au keshokutwa.”
“Uchunguzi wetu hauwezi kukamilika kwa kesho au keshokutwa. Tunahitaji muda kidogo. Kwa vile mtuhumiwa mwenyewe hataki kukubali kosa, itabidi kesho tufanye gwaride la utambulisho. Wale watu waliomuona kule gesti waje wamtambue tena hapa.”
“Kama walimuona kule hawawezi kushindwa kumtambua. Hata mahakamani wanaweza kumtambua. Hatuwezi kuchelewa kumpeleka mahakamani kwa sababu ya hiyo.”
“Hapana. Ni lazima zoezi hilo lifanyike kabla ya kumpeleka mahakamani. Hii ni kesi ya jaribio la kuua na inaweza kuwa kesi ya mauaji endapo yule kijana atafariki, hivyo ni lazima tuzingatie kanuni zote.”
“Kama unaona hivyo ni sawa, lakini mimi nilitaka tuharakishe kumfikisha mahakamani. Mara nyingi tumekuwa tukilaumiwa kwa kuchelewesha kesi.”
“Inabidi tuvute subira kidogo. Wakili wake anaweza kutushambulia mahakamani kwamba tumembambikia kesi mteja wake. Acha tuzingatie sheria zote. Haraka haraka haina baraka.”
Polisi huyo mwenye pupa akashusha pumzi.
“Kwa hiyo hilo gwaride litafanyika lini?” akauliza.
“Nafikiri litafanyika kesho asubuhi. Nitakwenda kuwapa taarifa wale vijana wa gesti waje hapa kesho asubuhi.”
“Sawa, afande.”
Baada ya hapo Inspekta Amour alikwenda kumfahamisha Wakwetu kwamba kesho yake saa mbili asubuhi atahitajika awepo kwenye gwaride la kumtambua mtuhumiwa.
“Mbivu na mbichi zitaeleweka kesho.”
“Sawa.”
“Kwa hiyo usikose kufika saa mbili asubuhi.”
“Nitafika.”
Wakwetu aliporudi nyumbani kwake alimweleza mke wake kuhusu matukio yote. Alianzia kwenye suala la yule kijana aliyepigwa risasi.
“Huyo kijana aliyepigwa risasi hajafa lakini hali yake ni mbaya.”
“Ulikwenda hospitali kumuona?” Sharifa akamuuliza.
“Nilikwenda kumuona.”
“Eh! Kumbe hakufa?”
“Hajafa na nimewaambia madaktari nitagharamia matibabu yake mpaka apone.”
“Kama ana hali mbaya, unadhani anaweza kupona kweli? Usije ukaharibu pesa zako!”
“Ni vizuri kufanya juhudi za kuokoa maisha yake hata kama matumaini ya kupona kwake ni madogo. Kama itatokea bahati akapona, kesi ya mauaji haitakuwepo. Kesi ile ndiyo itafichua mambo.”
“Mambo gani?”
“James anaweza kusema kuwa aliyempiga risasi yule kijana ni mwanangu.”
“Kwani James alimuona?”
“Hakumuona lakini ndiye aliyekuwa akitumia gari. James tulimpeleka sisi kumuokoa Majaliwa.”
“Na huwezi kuwahonga polisi ili kesi hii waachane nayo? Naona inaweza kutuletea matatizo mimi, mume wangu na mtoto wetu.”
“Kusema kweli haitawezekana. Tukio limeshafahamika. Wakuu wengi wa polisi wameshalijua. Utamuhonga nani, utamuacha nani?”
“Sasa kama huyo kijana aliyepigwa risasi atapona huoni kuwa atakuja kumtolea ushahidi Majaliwa?”
“Ni kweli, lakini tutafanyaje sasa?”
“Ungemuacha huyo kijana afe ili asije kutoa ushahidi dhidi ya Majaliwa.”
“Mimi nilitaka kumsaidia ili kuepusha ile kesi ya mauaji. Najua itafika mahali James atasema ukweli kwamba tulimpachika, lakini aliyehusika ni Majaliwa.”
Sharifa akabaki kimya akiwaza.
“Mimi naona wazo la kumsaidia yule kijana ili apone ni zuri. Mimi sitaki hii kesi ya mauaji,” Wakwetu alimwambia.
Kwenye kituo cha polisi, Inspekta Amour alikuwa akimuhoji James ofisini kwake.
“Niambie ukweli, kwanini ulimpiga risasi yule kijana mwenzako?”
“Sijampiga risasi na wala simfahamu. Kusema kweli sijawahi kufika Mabawa. Labda nimefananishwa tu,” James alijibu.
Inspekta Amour aliusokota upande mmoja wa sharubu zake huku akimtazama James kwa macho makali.
“Nani aliyekuwa akiendesha lile gari?”
“Ni mimi.”
“Sasa unakataa nini?”
James akatikisa kichwa.
“Ninakataa. Kuendesha gari hakumaanishi kwamba nimempiga mtu risasi.”
“Aliyekuwa akiendesha lile gari ndiye aliyefika pale gesti na kusababisha lile tukio, na kuna watu walikuona na waliliona gari lako.”
“Waliniona mimi?”
“Ndiyo, wewe.”
“Mimi hawajaniona, walimuona huyo aliyefika hapo gesti ambaye si mimi.”
“Una maana kuna mtu mwingine uliyempa lile gari?”
“Sijui kama mzee alimpa mtu mwingine.”
“Madereva wake mko wangapi?”
“Ni mimi peke yangu.”
“Aliyegonga mtu ni nani?”
“Ni mimi.”
“Basi wewe ndiye uliyempiga mwenzako risasi. Tuambie umeificha wapi ile bastola?”
“Sina bastola.”
“Una kisa gani na yule kijana?”
“Kijana huyo sijawahi kumuona.”
“Kesho asubuhi tutafanya gwaride la utambulisho. Wale watumishi wa gesti waliokuona watakuja kukutambua hapa na kesho hiyo hiyo tutakufikisha mahakamani.”
“Mimi nasubiri hilo gwaride. Naamini watasema si mimi.”
Inspekta Amour akamwambia polisi aliyekuwa amesimama kando ya meza.