Dar es Salaam. Tanzania kuandika historia mpya kwenye ramani ya dunia baada ya kuthibitishwa rasmi kuwa mwenyeji wa mashindano ya 74 ya urembo duniani (Miss World) 2027. Tukio kubwa linalotarajiwa kuibadilisha taswira ya sekta ya burudani, utalii na utamaduni nchini.
Hatua hiyo imekuja baada ya kusainiwa kwa mkataba rasmi wa maandalizi ya mashindano hayo leo Aprili 20, 2026 jijini Dar es Salaam. Ambapo Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisaini kwa niaba ya Serikali.
Msemaji Mkuu wa Serikali,Gerson Msigwa (kushoto) na Mwenyekiti wa Miss World,Julia Morley wakipeana mikono ya pongezi baada ya kusaini mkataba wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya 74 ya Miss World 2027, jijini Dar es Salaam leo Aprili 20,2026 . Katikati ni Waziri wa Habari,Utamaduni ,Sanaa na Michezo,Paul Makonda. Picha na Michael Matemanga
Hafla hiyo pia ilishuhudiwa na Waziri wa Wizara hiyo, Paul Makonda, ikihitimisha mchakato uliokuwa ukiendelea kwa muda wa maandalizi ya makubaliano (MoU) kati ya Tanzania na waandaaji wa mashindano hayo ya kimataifa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Makonda alisema hatua hiyo ni ushindi mkubwa kwa Tanzania na ushahidi kuwa nchi imeanza kuchukua nafasi yake katika matukio makubwa ya kimataifa.
“Hii ni heshima kubwa kwa Tanzania, tumekuwa tukifanya kazi kwa muda kuhakikisha tunatimiza vigezo vyote vya waandaaji wa Miss World. Na leo tunajivunia kufikia hatua hii, mashindano haya yatafungua milango mikubwa ya utalii, uwekezaji na kuitangaza Tanzania kimataifa,” alisema Makonda.
Waziri wa Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo, Paul Makonda akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya 74 ya Miss World, jijini Dar es Salaam leo Aprili 20,2026. Picha na Michael Matemanga
Aliongeza kuwa maandalizi yatahusisha wadau mbalimbali wa sanaa, utamaduni na sekta binafsi ili kuhakikisha tukio hilo linakuwa la kiwango cha dunia
Kwa upande wake, Msigwa alieleza kuwa ujio wa Miss World 2027 ni jukwaa muhimu la kuionesha Tanzania kwa dunia nzima.
“Kupata uenyeji wa Miss World si jambo dogo. Hii ni fursa ya kipekee ya kuitangaza Tanzania kuanzia vivutio vya utalii, utamaduni wetu hadi ubunifu wa vijana wetu, Dunia itakuja kwetu, na tunapaswa kujiandaa kuitumia vyema nafasi hii,” alisema Msigwa.
Historia kwa Afrika
kwa mafanikio hayo, Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika kuandaa mashindano hayo makubwa ya urembo, ikiwa ni nchi ya pili baada ya Afrika Kusini.
Hatua hiyo inaendelea kuonesha dhamira ya Serikali kuimarisha sekta ya burudani na kuitumia kama nyenzo ya kukuza uchumi, sambamba na jitihada zinazoendelea za kuiweka Tanzania kwenye ramani ya matukio makubwa duniani.
Msukumo mpya kwa utalii na burudani
Kwa mujibu wa wadau wa sekta hiyo, mashindano ya Miss World yana mvuto mkubwa kimataifa na huvutia washiriki na watazamaji kutoka mataifa mbalimbali, hali inayotarajiwa kuongeza mapato ya utalii na kukuza ajira.
Tayari Tanzania imeanza kuonesha mwelekeo huo baada ya kufanikisha mashindano ya kitaifa ya Miss World Tanzania 2026, yaliyovutia ushindani mkali na kuibua vipaji vipya katika urembo na utamaduni.
Msemaji Mkuu wa Serikali,Gerson Msigwa (kushoto) na Mwenyekiti wa Miss World,Julia Morley wakisaini mkataba wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya 74 ya Miss World 2027, jijini Dar es Salaam leo Aprili 20,2026 .Katikati ni Waziri wa Habari,Utamaduni ,Sanaa na Michezo,Paul Makonda.Picha na Michael Matemanga
Safari ya kuelekea 2027 yaanza
Baada ya hatua hiyo ya kihistoria, sasa macho yote yanaelekezwa kwenye maandalizi ya kina ya kuhakikisha Tanzania inakuwa mwenyeji bora wa mashindano hayo. Kwa sasa, ni wazi Tanzania haiko tena nyuma, bali imeanza kusimama mbele ya jukwaa la dunia