Unguja. Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves baada ya kuiweka timu hiyo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa tofauti ya pointi tano, hivi sasa ana hesabu mpya ndani ya kikosi hicho akibainisha kwamba, anahitaji kuimarisha jeshi lake kuhakikisha anashinda mechi zote tatu za Kombe la Muungano ili kutetea ubingwa wao.

Kauli ya Pedro ameitoa baada ya kikosi cha Yanga kutua Unguja jana Jumatatu tayari kwa kuanza kutetea Kombe la Muungano ambalo timu hiyo ililibeba mwaka jana ilipoifunga JKU katika fainali iliyochezwa Uwanja wa Gombani, Pemba, huku pia akiwa na hesabu za kubeba Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la CRDB wakitinga robo fainali.

Yanga leo Jumanne itacheza dhidi ya Muembe Makumbi City kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja kuanzia saa 1:15 usiku katika mechi ya Kombe la Muungano ambapo mshindi atakutana na atakayeshinda kati ya KVZ na Azam zitakazokutana kesho Jumatano.

“Tumefika hapa, kama ilivyo kawaida hii ni timu ambayo wakati wote inahitaji mafanikio, tumekuja kama bingwa mtetezi, tunataka kuendeleza yale ambayo tuliyafanya msimu uliopita,” alisema Pedro ambaye atashiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo huku akiwa na kumbukumbu ya kubeba Kombe la Mapinduzi 2026 kisiwani hapa.

“Nilikuwa hapa wakati wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi, najua namna ilivyo ngumu kushinda dhidi ya timu za hapa, hatuwezi kuchukulia rahisi timu ya Mwembe Makumbi.

“Tumekuja na timu kamili, wachezaji ambao tumewaacha nyuma ni wale ambao tunaona sio rahisi sana kucheza msimu huu lakini wengine wote wako hapa tutakuwa na mechi tatu mpaka kufika fainali,” alisema.

Aidha Pedro alisema Yanga haiwezi kuogopa mpinzani yeyote ambapo kikosi chake kitacheza kwa kiwango kikubwa kulingana na ubora wa mpinzani aliye mbele yao wakitumia ubora wao.

“Hakuna nafasi ya kuhofia timu yoyote unapokuwa unafanya kazi na timu kama hii ya Yanga, tuna wachezaji waliokomaa, wanajua namna ya kucheza mechi za presha, tutawaheshimu wapinzani ambao tutakutana nao, kila timu tutakuwa na mpango wa kucheza nayo,” alisema.

Mchezo wa mwisho kwa Pedro kushinda kisiwani hapa ni pale alipoichapa Azam kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026, iliyopigwa pale Gombani, Januari 13, 2026.

Yanga ili kutetea ubingwa wake, inapaswa kushinda mechi tatu kwa kuanza leo dhidi ya Muembe Makumbi, kisha nusu fainali na fainali.

Wakati huohuo, kikosi cha Yanga kitaikosa huduma ya kiungo wake, Mudathir Yahya ambaye amefungiwa mechi tatu na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), sambamba na kutozwa faini ya Sh1 milioni.

Kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya Ligi, Mudathir amefungiwa mechi hizo tatu dhidi ya Simba, KMC na Coastal Union, kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Pamba Jiji, Ibrahim Abraham wakati timu hizo zilipokutana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na Yanga kushinda 3-0, huku mabao mawili yakifunga na kiungo huyo.

Mudathir ambaye kwa siku za karibuni amekuwa na kiwango bora ndani ya Yanga, hivi sasa ana mabao saba kwenye ligi akiwa nyuma kwa bao moja dhidi ya vinara, Prince Dube (Yanga) na Fabrice Ngoy (Namungo) wenye manane kila mmoja, huku yeye akiwa sawa na Feisal Salum (Azam), Saleh Karabaka (JKT Tanzania), Pacome Zouzoua (Yanga) na Idd Seleman ‘Nado’ (Azam).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *