Kuanzia tarehe 1 Januari 2027, kutakuwa na kiongozi mpya katika ghorofa ya 38 ya Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, na baada ya miaka 10 madarakani, akitimiza mihula miwili ya ngazi ya juu zaidi Umoja wa Mataifa, António Guterres anang’atuka.

Mrithi wake atakabiliwa na changamoto kubwa za kisiasa na kifedha, huku pia akitarajiwa kuendeleza mageuzi muhimu ili kuhakikisha Umoja wa Mataifa unakuwa tayari kwa mustakabali katika wakati ambapo Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa zinakabiliwa na shinikizo kubwa za kila aina.

Collage ya picha nne za kitaalamu za wagombea wa nafasi ya Katibu Mkuu, ikionyesha kikundi tofauti cha wanawake na wanaume wakiwa wamevaa mavazi rasmi ya biashara.

Umoja wa Mataifa

Wagombea wanne wamepangwa kumrithi António Guterres kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuanzia Januari 1, 2027. Wagombea hao ni Michelle Bachelet (Chile), Rafael Grossi (Argentina), Rebeca Grynspan (Costa Rica), na Macky Sall (Senegal).

Wagombea wawasilisha dira zao

Leo Jumanne na kesho Jumatano, wagombea wawili wanaume na wawili wanawake wanashiriki katika mikutano ya Baraza Kuu, wakieleza maono yao kwa Umoja wa Mataifa na kujibu maswali kutoka kwa nchi wanachama na wawakilishi wa asasi za kiraia kuhusu uzoefu wao wa uongozi, mageuzi ya Umoja wa Mataifa, pamoja na nguzo tatu za shirika ambazo ni amani na usalama, maendeleo na haki za binadamu.

Wagombea hao ni Michelle Bachelet kutoka Chile, Rafael Grossi kutoka Argentina, Rebeca Grynspan kutoka Costa Rica, na Macky Sall kutoka Senegal.

Hatua muhimu katika mchakato wa uchaguzi

Mazungumzo hayo yanaongozwa na Rais wa Baraza Kuu, Annalena Baerbock, ambaye amesema ni hatua muhimu katika mchakato wa uchaguzi unaofanyika katika kipindi nyeti kwa Umoja wa Mataifa.

“Uteuzi wa Katibu Mkuu una athari kubwa zinazovuka mipaka ya jengo hili,” amesema Bi. Baerbock. “Chaguo letu litaelekeza mustakabali wa shirika hili la kipekee la kimataifa na kuonesha kama kweli Umoja wa Mataifa unawakilisha zaidi ya watu bilioni nane duniani, nusu yao wakiwa wanawake na wasichana.”

Ameongeza kuwa uteuzi huo si uamuzi wa kiutawala pekee bali ni kauli ya dhamira,

“Utatuma ujumbe wenye nguvu kuhusu Umoja wa Mataifa unasimamia nini na jinsi unavyokusudia kukabiliana na changamoto za dunia ya leo iliyounganishwa.”

‘Kazi ngumu zaidi duniani’

Bi. Baerbock ameielezea nafasi hiyo kama moja ya kazi ngumu zaidi lakini muhimu sana duniani.

“Kwa kifupi, hii ni moja ya kazi ngumu zaidi duniani,” amesema, “lakini pia ni moja ya kazi muhimu zaidi, kwani Katibu Mkuu ajaye ataathiri mustakabali wa taasisi hii na, kama mtetezi mkuu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, pia mustakabali wa utaratibu wa kimataifa unaozingatia sheria.”

Mazungumzo shirikishi yanaendeshwaje

Katika mazungumzo hayo ya saa tatu, wagombea watatoa hotuba ya ufunguzi ya hadi dakika 10, ikifuatiwa na maswali kutoka kwa nchi wanachama na wawakilishi wa asasi za kiraia ili kuchunguza zaidi uwezo wao wa uongozi na uzoefu.

Majadiliano yatafuata sehemu mbili kuu:

  • Uwezo wa uongozi, uzoefu na ujuzi wa wagombea kwa ajili ya shirika imara na linaloendana na wakati ujao
  • Nguzo tatu za Umoja wa Mataifa: amani na usalama, maendeleo, na haki za binadamu

Jinsi wagombea watakavyojibu maswali mbalimbali itakuwa hatua muhimu katika mchakato wa uchaguzi.

Mazungumzo yote manne yataoneshwa moja kwa moja kupitia chaneli ya mtandao ya Umoja wa Mataifa UN WebTV.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani kabla ya kuanza kwa midahalo ya wazi na wagombea wa nafasi hiyo, Rais huyo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Baerbock ameeleza kuwa uchaguzi huo una umuhimu mkubwa duniani kote, ukigusa maisha ya zaidi ya watu bilioni nane, nusu yao wakiwa wanawake na wasichana.

Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani

UN /Loey Felipe

Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani

Amesema katika kipindi cha miaka kumi tangu kuchaguliwa kwa Katibu Mkuu wa mwisho, dunia imekumbwa na mabadiliko makubwa, yakiwemo kuongezeka kwa migogoro, mabadiliko ya tabianchi, maendeleo ya kasi ya teknolojia, janga la afya duniani na kuongezeka kwa pengo la usawa.

“Uamuzi huu si wa kiutawala tu, bali ni ujumbe kuhusu maadili na mwelekeo wa Umoja wa Mataifa katika kukabiliana na changamoto za dunia ya leo,” alisema.

Mwana Mageuzi

Baerbock amebainisha kuwa Katibu Mkuu ajaye atahitajika kuongoza mageuzi muhimu ili kuhakikisha Umoja wa Mataifa, ulioanzishwa miaka 80 iliyopita, unaendana na mahitaji ya karne ya 21.

Kupitia midahalo hiyo ya saa tatu, wagombea watapata fursa ya kueleza dira zao na kujibu maswali kutoka nchi wanachama 193, wakionesha uwezo wao wa kuongoza katika nyanja kuu tatu: amani na usalama, haki za binadamu na maendeleo endelevu.

Ameongeza kuwa, pamoja na nchi wanachama, sauti za asasi za kiraia pia zitahusishwa ili kuhakikisha mchakato huo unakuwa wazi na shirikishi zaidi.

“Uamuzi kuhusu uongozi wa baadaye wa Umoja wa Mataifa unawahusu watu wote,” alisisitiza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *