Tofauti zilizozuka kati ya Trump na Papa Leo wa 14 hazitokani na masuala ya kisiasa pekee, lakini zimesababishwa zaidi na hulka ya majivuno na ya kujikweza aliyonayo rais huyo wa sasa wa Marekani.

Katika muendelezo wa sera za kushupalia vita za utawala wa Marekani, rais wa nchi hiyo anajaribu kumlazimisha kiongozi wa Wakatoliki duniani aunyamazie uovu na uhalifu anaofanya.
Katika andiko lenye lugha ya matusi na ya kifidhuli aliloweka kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, Donald Trump amemtaja Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Leo XIV kuwa ni “mtu dhaifu sana” na akasema, hamtaki Papa anayemkosoa. Trump alitoa matamshi hayo baada ya Papa Leo wa 14, kutoa mjibizo, kwa ushupaliaji na uwashaji moto wa vita uliofanywa na rais huyo wa Marekani dhidi ya Venezuela na Iran, kwa kusema: “Yesu Kristo ni Mfalme wa amani asiyekubali vita, na hakuna mtu yeyote anayeweza kumtumia yeye kuhalalisha vita. Yesu hasikilizi maombi ya watu wanaoanzisha vita, na anawakataa.” Mwishoni mwa wiki iliyopita pia, kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani aliashiria moja kwa moja vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran na kuviita vita “vya kutisha na visivyo vya kiutu” na kuwataka viongozi wa dunia wachukue hatua badala yake, kwa kufuatilia diplomasia. Alisisitiza kwa kusema: “basi tena kwa uabudiaji wa sanamu la nafsi na pesa! Basi tena kwa uonyeshaji nguvu! Basi tena kwa vita! Nguvu za kweli huonyeshwa kwa kutumikia uhai”.
Pamoja na hayo, badala kuonyesha heshima kwa mmoja wa viongozi maarufu zaidi wa kidini duniani, mtu anayefuatwa na mamilioni ya Wamarekani, rais wa Marekani alitumia lugha ya matusi na ujeuri akidai kuwa Papa Leo XIV alichaguliwa kuwa mkuu wa Kanisa Katoliki kutokana na kuungwa mkono na rais wa Marekani.
Leo XIV ni Papa wa kwanza Mmarekani katika historia ya miaka elfu mbili ya Vatikani, na kwa sababu hiyo, Trump alitarajia kwamba kupitia Papa Mmarekani, angeweza kuendeleza sera zake za kijinai na za kuchochea moto wa vita.

Papa Leo (kushoto) na Trump

Hata hivyo, katika muda wa mwaka mmoja tangu ashikilie wadhifa wa Upapa, Leo XIV ameonyesha ni kwa kiwango gani asivyokubaliana na utawala wa Trump. Papa huyo wa sasa, sio tu amepinga moto wa vita uliowashwa na Trump katika nchi za Venezuela na Iran, lakini tangu mwanzo wa kutawazwa kushika wadhifa wa kuongoza Kanisa Katoliki, amekuwa na misimamo ya wazi pia dhidi ya vita vya Ghaza na mauaji ya Wapalestina, na ametamka bayana kwamba, sera za utawala wa Trump dhidi ya wahamiaji si za kibinadamu.
Misimamo hiyo ya Papa imesababisha kuongezeka mivutano katika miezi ya hivi karibuni kati ya Washington na Vatikani. Bila shaka, mivutano hii haitokani na masuala ya kisiasa pekee, bali inachochewa kwa kiwango kikubwa na hulka ya majivuno na kujikweza aliyonayo rais wa sasa wa Marekani. Kwa kutoa mfano ni kwamba, kabla ya kuchaguliwa Papa wa sasa, Trump alijitangaza katika mazungumzo na waandishi wa habari kuwa yeye ndiye mtu anayefaa zaidi kuongoza Kanisa Katoliki na akasambaza picha yake kwenye mitandao ya kijamii akiwa amevalia mavazi ya Upapa.
Siku chache zilizopita, Trump alikwenda mbali zaidi kwa kuvuka mpaka wa kudai Upapa, baada ya kujiweka katika nafasi ya Nabii Isa Masih AS, au Yesu Kristo. Katika picha mpya aliyoweka kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, Trump amejifanya kama Yesu Kristo anayetokea mbinguni kuja kubariki watu. Picha hiyo ya kutusi na kuudhi imechukiza na kuamsha hasira za mamilioni ya waumini.
Kwa mtazamo wa wafuasi wengi wa dini za tauhidi, vitendo hivyo vinachukuliwa kuwa vya kutusi na vya uvunjaji mkubwa wa heshima. Inavyoonekana, baada ya kutwaa tena kiti cha urais wa Marekani na kujaribu kujifanya mtawala mkuu wa dunia, Trump sasa amedhamiria kutwaa uongozi wa Kanisa Katoliki na kukaa kwenye nafasi ya watakatifu wa Ukristo. Jambo hili linaonyesha kuwa kujikweza kwa Trump kumevuka mipaka ya kawaida na kumfanya awe mtu hatari sana kwa dini na ulimwengu wa wanadamu.
Rais wa moja ya tawala zinazowasha moto mkubwa wa vita duniani, ambaye siku chache tu zilizopita alilitishia taifa la Iran lenye watu milioni 90 kwamba ataliangamiza na ustaarabu wake, sasa amekusudia kujifanya nabii aliyevalia vazi la amani na huruma na kutoa vitisho kwa kiongozi wa Wakatoliki duniani. Hata hivyo Papa Leo wa 14 ametamka bayana katika taarifa yake, kwamba hauogopi utawala wa Trump na wala hana nia ya kuunyamazia kimya moto wa vita unaoendelea kukolezwa hivi sasa duniani.
Pamoja na hayo, Trump ambaye amekasirika mno na kunyong’onyea kutokana na kugonga kwamba katika vita alivyoanzisha dhidi ya Iran, haonekani kama ataacha ufidhuli wake wa kumtusi na kumdhalilisha kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani, hatua ambayo inaweza kudhoofisha zaidi nafasi yake ya urais wa Marekani na wafuasi wake katika Chama cha Republican mbele ya mamilioni ya wapiga kura Wakatoliki wa nchi hiyo…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *