Mwakilishi Maalumu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini, ambaye aliwasili Tehran kwa ajili ya mashauriano na viongozi wa Iran, amekutana na kuzungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.

Katika mazungumzo yake na Chang Byung-ha Mwakilishi Maalumu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Araqchi ameutaja uvamizi wa kijeshi wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran kuwa ni chanzo cha ukosefu wa usalama katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Mlango-Bahari wa Hormuz.

Amesema: “Iran, ikiwa kama nchi ya pwani mwa Mlango-Bahari wa Hormuz, imechukua hatua kwa mujibu wa sheria za kimataifa na sheria zake za ndani ili kulinda usalama wake na maslahi ya taifa mkabala wa mashambulizi na vitisho vya Marekani na utawala wa Kizayuni; na ni wazi kuwa pande vamizi ndio zinazobeba dhima ya hali inayoshuhudiwa hivi sasa.

Araqchi, ameeleza jinai zilizofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel wakati wa uvamizi wa kijeshi wa pande hizo dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa ipo haja kwa nchi za dunia kueleza waziwazi misimamo na maamuzi yao na kulaani mashambulizi hayo ya kinyama dhdi ya watu wa Iran.  

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Tehran, Mwakilishi Maalumu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini amesema ameridhishwa usitishaji vita na kwamba anatumai kuwa: “Kwa kufuata mchakato wa kidiplomasia, vita vitahitimishwa kikamilifu na amani na utulivu vitarejea katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *