Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 yalitikisa misingi ya Taifa na kwamba kuyapuuza au kuyaficha ukweli wake, ni kujidanganya kama nchi.

Akizungumza leo Aprili 23,2026 wakati akipokea ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani, Rais Samia amesema  licha ya maumivu yaliyotokea, Taifa limepata funzo kubwa lililosaidia kuimarisha hatua za ulinzi na udhibiti wa vurugu.

“Tutakuwa tunajidanganya tusiposema ukweli kwamba yaliyotokea wakati ule yalitikisa Taifa letu,” amesema.

Hata hivyo, ameeleza kuwa kupitia tukio hilo la majonzi, Taifa limejifunza na kupata mwelekeo mpya wa namna ya kushughulikia changamoto za kiusalama.

“Hata hivyo, kupotea njia ndiyo kujua njia, tumegusa kaa la moyo na limetuunguza. Tumejifunza,” amesema.

Rais Samia ametaja mchango wa vyombo vya ulinzi na usalama katika kudhibiti vurugu hizo kuwa ndio uliosaidia kuokoa Taifa dhidi ya hali mbaya zaidi ambayo ingeweza kutokea.

“Jitihada za vyombo kudhibiti vurugu zile ndiyo imefanya Tanzania leo iwe hivyo ilivyo, vinginevyo tungekuwa tunazungumza hadithi nyingine,” amesema.

Hata hivyo, amesema kuwa hatua za udhibiti hazipaswi kuondoa uwajibikaji kwa waliokiuka sheria, akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya wahusika.

“Hii haimaanishi kuwa kwa wale ambao tutabaini wamekiuka sheria na taratibu za kazi zao kwamba hatutawawajibisha. Ukweli ni kwamba tutawajibishana,” ameeleza.

Kuhusu taarifa zilizozagaa baada ya matukio hayo, Rais Samia amesema kulikuwa na upotoshaji mkubwa wa takwimu za vifo na majeruhi, baadhi ya watu na makundi walitoa taarifa zisizo sahihi.

“Kufuatia ghasia zile kumekuwa na taarifa nyingi zilizotolewa bila usahihi… takwimu hizo zilikusudia kufifisha au kutia chumvi kiwango cha madhara yaliyotokea,” amesema.

Amesema sasa Taifa limepata takwimu rasmi zilizochambuliwa na tume hiyo, ambazo zinaweka bayana idadi ya waliopoteza maisha, waliojeruhiwa na waliopata madhara mbalimbali.

“Leo tumepokea takwimu zilizochambuliwa vizuri na tume hii. Tume imewasilisha taarifa yake inayotokana na uchunguzi wa kitaalamu na ukweli umebainika,” amesema.

Rais Samia pia amegusia uwepo wa madai ya baadhi ya wananchi kutowajua au kuwaona ndugu zao, akiahidi kuwa Serikali itaendelea kufanya uchunguzi wa kina kubaini ukweli wa hali hiyo.

“Tumeelezwa kuhusu uwepo wa madai ya wananchi ambao hawajaweza kuwaona ndugu zao, niwaahidi kuwa Serikali itaendelea kufanya uchunguzi wa kina na wa kitaalamu ili tujue mambo haya kwa usahihi wake,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *