Tunapozungumzia fursa zinazopatikana mwambao, picha inayokuja haraka akilini mwa wengi ni ile ya mvuvi aliyeshika nyavu zake, akipambana na mawimbi usiku kucha ili apate samaki wa kuuza feri asubuhi. Picha hii, ingawa ni ya kweli, inatufumba macho tusione vizuri fursa nyingine ya mabilioni ya fedha yaliyolala kwenye maji mafupi na matope ya fukwe zetu.

Kwa miongo mingi, tumezoea kuvuna tu kile ambacho asili imetupa mpaka rasilimali zimeanza kupungua, lakini sasa dunia imebadilika. Soko la kimataifa, hasa kule barani Asia, lina njaa kubwa sana ya majongoo bahari na lulu asilia. Kiumbe huyu anayeonekana kama hana thamani yoyote anapojivuta kwenye tope au kujificha kwenye nyasi za baharini, ndiye anayepakuliwa kwenye sahani za kifahari katika hoteli kubwa huko ughaibuni kwa bei ya juu sana.

Kupitia mradi uliobuniwa na kusimamiwa na Shirika la Uhifadhi wa Bahari la Blue Ventures, na makala ya kitafiti iliyochapwa na jarida la kimataifa la Global Seafood Alliance, inaelezwa kuwa jamii za pwani nchini Madagascar zimebuni mfumo wa kimapinduzi wa “mashamba ya majongoo bahari”.

Ili kufanikisha hilo, wanakijiji wa Kijiji cha Tampolove kusini magharibi mwa Madagascar, kwa kushirikiana na wadau wa mazingira, walijenga vitalu vya wavu kwenye maji mafupi, kupandikiza mbegu za majongoo bahari au chaza wanaozalisha lulu (sea cucumbers), na kuwalea mpaka wakue. Huu ni ukulima wa bahari uliojengwa juu ya utaalamu na mahesabu ili kupata bidhaa bora inayohitajika na soko hasa mahoteli ya kitalii ambapo kiumbe huyu huliwa kama chakula cha kifahari.

Miongoni mwa kilichofanya mradi huu wa Tampolove ufanikiwe kwa kishindo si fedha za wawekezaji, bali ni nguvu ya umoja wa kijamii. Walitambua kuwa huwezi kujenga shamba lako peke yako baharini na ukalilinda usiku na mchana. Umoja wa kijamii unaofanana kabisa na dhana yetu ya Kiswahili ya ‘ujirani’ umewasaidia katika kushirikiana kiuchumi na kufanya shughuli hiyo kwenye mashamba ya pamoja.

Wanakijiji waliunda ushirika. Kila jirani alikuwa mlinzi wa mwenzake, kwani kuhujumu shamba la mwenzako ni sawa na kuhujumu mtaa mzima. Vilevile, kwa kuwa majongoo bahari hufugwa kwenye maji mafupi yenye kina cha kuanzia magotini hadi kiunoni, fursa hii iliwakomboa zaidi kinamama.

Kijadi, uvuvi wa maji marefu ni wa wanaume, lakini sasa kina mama wa Tampolove wamepata fursa ya kumiliki uchumi wao. Wanaenda mikokoni nyakati za maji kupwa, wanahudumia vitalu vyao, na kurudi nyumbani kuendelea na majukumu mengine.

Matokeo ni kama ilivyotegemewa. Majongoo bahari yamewatoa kwenye umaskini wa kutupwa. Nyumba za makuti zimeezekwa mabati, watoto wanaweza kupata mahitaji muhimu kama elimu, na wana zahanati yao wenyewe, miongoni mwa mengine. Pesa inazunguka ndani ya kijiji chao, na kila mtu angalau ana chanzo cha uhakika cha kipato cha mwisho wa mwezi kutokana na mauzo ya nje.

Hili ni darasa tosha kwa jamii zetu za pwani ya Tanzania. Bahari yetu ina uwezo wa kutupa utajiri endelevu na mkubwa sana kuliko tunavyojua. Sisi ni watu tuliounganishwa na udugu thabiti na maisha ya ujirani mwema. Ikiwa tutautumia ule umoja wetu tunaouonyesha kwenye misiba na sherehe, na kuupeleka kwenye kuunda ushirika wa uzalishaji wa rasilimali hizi, tutaushangaza ulimwengu; hasa kwa jamii za pwani, kwani jamii za kilimo zimeonyesha mfano huu.

Bahari ni hazina, na tunaishi kando yake kila uchwao. Kinachohitajika sasa si mtumbwi mpya, bali ni fikra mpya. Umaskini kwenye fukwe zetu unaweza kumalizwa endapo tutatazama matope ya bahari kwa jicho la utajiri unaosubiri kuvunwa, kama walivyofanya wenzetu wa Tampolove.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *