
Dar es Salaam. Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 imebaini kuwa ghasia zilizotokea siku hiyo na baada, zilichochewa na changamoto sugu za kijamii na kisiasa ambazo zilikuwa zimejengeka kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi.
Akiwasilisha ripoti ya tume hiyo, Mwenyekiti wake, Jaji Othman Chande amesema uchunguzi umebaini kuwepo kwa vyanzo vitano vikuu pamoja na vichocheo vinane vilivyosababisha matukio hayo.
Amesema tume ilipokea na kuorodhesha jumla ya maeneo 31 yaliyotajwa na mashahidi kuwa chanzo cha ghasia hizo, hatua iliyosaidia kubaini kwa undani mazingira ya matukio yaliyotokea.
Jaji Chande amesema chanzo kimoja kikubwa ni masuala ya kisiasa, yakiwamo madai ya Katiba mpya, hoja za kuimarisha demokrasia katika mfumo wa vyama vingi, malalamiko ya ndani ya vyama vya siasa pamoja na hitaji la maboresho ya Tume Huru ya Uchaguzi na mfumo mzima wa uchaguzi.
Ameeleza kuwa chanzo kingine ni changamoto za kiuchumi na kijamii, ikiwamo ugumu wa maisha, ukosefu wa ajira, ukosefu wa usawa katika fursa za kiuchumi, pamoja na mazingira yasiyo rafiki kwa biashara na uwekezaji.
“Pia, kumekuwepo na malalamiko kuhusu utitiri wa tozo na kodi pamoja na mifumo isiyo rafiki ya ukusanyaji mapato, hali inayochangia kuongeza msongo kwa wananchi,” amesema.
Mbali na hayo, tume imebaini kuwepo kwa changamoto za maadili na uzalendo, ikiwamo mmomonyoko wa maadili katika jamii na kukosekana kwa majibu ya haraka kwa kero za wananchi kama vile rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na madai ya utekaji na kupotea kwa watu.
Akitoa takwimu, Jaji Chande amesema kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, kati ya mwaka 2023 hadi 2025 jumla ya watu 758 waliripotiwa kupotea, kutekwa au kujiteka, huku watu 113 walipatikana.
Amesema mashauri nane yalifunguliwa kuhusiana na matukio hayo na upelelezi wake unaendelea, huku watu 445 kati ya waliopotea bado hawajapatikana.
“Takwimu hizi zinaakisi kwa kiasi kikubwa malalamiko ya wananchi kuhusu masuala ya utekaji na kupotea kwa watu, jambo ambalo lilitajwa kuwa miongoni mwa vichocheo vya ghasia,” amesema.