
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Oktoba 29, Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman, amesema uchunguzi wao umebaini mali zilizoharibiwa za sekta binafsi na za umma zina thamani ya Sh125 bilioni.
Akiwasilisha ripoti ya tume hiyo leo Alhamisi Aprili 23, 2026, Jaji Chande amesema kati ya mali hizo, zile za sekta binafsi, zikiwamo za vituo vya mafuta, mali za Chama cha Mapinduzi (CCM) na taasisi za kifedha (benki), zina thamani ya Sh89 bilioni, sawa na asilimia 71.2.
Wakati mali za sekta ya umma zilizoharibiwa zikiwamo za Serikali na taasisi kama shule, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Jeshi la Polisi, Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), zina na thamani ya Sh36 bilioni, sawa na asilimia 28.8.
“Tume imebaini kutoka vyanzo mbalimbali kuwa mali zilizoharibiwa ina thamani ya Sh125 bilioni. Kati ya hizo, mali za sekta binafsi, zikiwamo za vituo vya mafuta, CCM na benki, zina thamani ya Sh89 bilioni, sawa na asilimia 71.2, huku sekta ya umma ikiwa na thamani ya Sh36 bilioni, sawa na asilimia 28.8,” amesema.
Jaji Chande amesema sekta binafsi imeathirika zaidi kuliko sekta ya umma, huku akieleza ushahidi wa waliopoteza mali zao unaonesha maumivu makubwa waliyonayo na wanaendelea kuyabeba.
Ametoa mfano wa mstaafu mmoja aliyeieleza tume hiyo kuwa, baada ya kustaafu alipata mkopo wa Sh180 milioni kutoka Benki ya Equity Tanzania kwa ajili ya kununua gari la biashara (tipa la mchanga), na alikuwa analipa marejesho ya Sh6 milioni kila mwezi.
Jaji Chande amesema mstaafu huyo aliieleza tume kuwa, baada ya kununua gari hilo, alikuwa akiliegesha Kimara Temboni baada ya kazi, na alikuwa amelimiliki kwa miezi miwili tu.
“Oktoba 29, 2025, gari hilo lilipokuwa limeegeshwa Kimara Temboni katika eneo la Tanroads, lilivamiwa na kuchomwa moto hadi kuteketea kabisa. Nilijaribu kufuatilia fidia kupitia bima, lakini haikuwezekana kwa kuwa nilikuwa na bima ya kawaida (comprehensive) na si bima ya majanga ya kisiasa,” alinukuliwa mstaafu huyo.
Jaji Chande amesema wajasiriamali wadogo na wa kati waliporwa na kuibiwa mali zenye thamani ya Sh10.6 bilioni. Akimnukuu shahidi mmoja kutoka Tegeta jijini Dar es Salaam aliyesema:
“Mimi ni mfanyabiashara wa simu. Siku ya uchaguzi mkuu, duka langu lilivamiwa na watu waliokuwa wakifanya vurugu, wakachukua simu zote. Simu hizo zilikuwa za mkopo. Hali yangu ni mbaya; sijui nifanye nini, siwezi kuendelea na biashara na nimeathirika kisaikolojia.”
Jaji Chande ameongeza kuwa, inawezekana thamani ya mali zilizoibwa kutoka katika kundi hilo ni kubwa zaidi, kutokana na changamoto za utunzaji wa kumbukumbu za biashara kwa baadhi ya wajasiriamali.
Katika maelezo yake Jaji Chande amesema kulikuwa na hasara katika sekta ya fedha, jumla ya Sh626.7 milioni ziliporwa kupitia mashine za ATM za benki tatu kubwa ikiwamo CRDB, NMB na NBC.
Ametaja sekta nyingine ziliathirika kiuchumi ikiwamo kushuka kwa masoko ya fedha, mabadiliko ya mzunguko wa fedha, usafiri na usafirishaji pamoja na utalii.
“Kwa mujibu wa taarifa ya Februari 2025 ya kampuni ya kimataifa ya kutathmini uwezo wa nchi kukopa, Tanzania imebakia katika kiwango cha B1, hali inayomaanisha inaendelea kuaminika kwa wakopeshaji kama ilivyokuwa kabla ya Uchaguzi Mkuu,” amesema Jaji Chande.
Hata hivyo, amesema wachumi waliokutana na tume hiyo walisisitiza kuwa, endapo changamoto za kisiasa hazitashughulikiwa ipasavyo, kiwango hicho kinaweza kushuka.
Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuunda Tume ya Uchunguzi ulikuwa mzuri, wa haki na ni hatua muhimu katika kujenga uchumi wa Taifa.
Rais Samia akizungumza kuhusu athari za kiuchumi baada ya kupokea ripoti huyo, amesema kama ghasia hizo zisingethibitiwa nchi ingepata athari kubwa zaidi na ingechukua miaka mingi kuinuka tena.
“Niwasihi Watanzania wenzangu ni rahisi kupoteza amani lakini si rahisi kuirejesha, ni rahisi kuiboma nchi lakini ni ngumu kuijenga, tufahamu kuwa hatima ya Tanzania ipo mikononi mwa Watanzania wenyewe nguvu ya ushawishi wa nje inabomoa usalama wa nchi, na kuijenga nchi yetu hufanyika kwa jitihada ya misaada ya masharti magumu yenye masharti ya uchumi na kisiasa ” amesema.
“Natambua wapo wafanyabiashara wadogo wadogo ambao kwa uwezo wao, hawawezi kuingia kwenye bima kubwa, tutaangalia hasara waliyopata na kuangalia faraja ya kuwapatia.”
Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo amesema ni muhimu Serikali kuchukulia jambo hilo kwa umuhimu wake kwa kuwa, halikuwa la kibiashara bali limetokea nje ya uwezo wao wapaswa kusaidiwa.
“Ni kazi ya Serikali kubeba jukumu, kwanza wafanyiwe tathimini ya kisayansi na si lazima walipwe mabilioni yaliyotajwa, bali wanaweza kukubaliana wasikatwe kodi kwa muda fulani,” amesema Profesa Kinyondo.
Amesema jukumu la Serikali ni kulinda raia na mali zao, na katika hilo Serikali ilishindwa huku akionesha wasiwasi na tume hiyo, akisema ilikuwa na watu wanaofanana.
“Tutakuwa tumefanya kosa kubwa kuangalia athari za kiuchumi kwa kuangalia walioharibiwa mali pekee, kuna wale ambao wanategemewa katika familia waliopata ulemavu au walipoteza maisha lazima wajukuishwe, hawana uwezo tena,” amesema.