SIMBA leo Aprili 23, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, imepata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar, huku ikijikatia tiketi ya kwenda nusu fainali ya Kombe la Muungano ambapo sasa itakutana na Mlandege.
Ni walewale Januari 13, 2024, Mlandege waliyoishangaza Simba kwenye Uwanja wa Amaan wanakwenda kukutana tena hapo, lakini safari hii ni nusu fainali ya Kombe la Muungani, huku ikikumbukwa mara ya mwisho walikutana fainali ya Kombe la Mapinduzi 2024 na Mlandege kushinda 1-0, kupitia bao la Joseph Akandwanaho anayecheza TRA United hivi sasa.
Nusu fainali hiyo ya pili itachezwa Aprili 26 mwaka huu saa 2:15 usiku, ikitanguliwa na nusu fainali ya kwanza Azam dhidi ya Yanga, Aprili 25, 2026.
Katika mechi ya leo, haikuwa rahisi kwa Simba kupata ushindi huo ikilazimika kusubiri mpaka dakika ya 53 kipindi cha pili mashabiki wake kushangilia bao hilo pekee mfungaji akiwa mshambuliaji, Seleman Mwalimu ‘Gomes’.
Mwalimu aliingia mwanzoni mwa kipindi cha pili, akichukua nafasi ya Baraka Mwangosi na kwenda kuifungia Simba bao hilo akiunasa mpira kutoka kwa mabeki wa Mafunzo waliokuwa wakihangaika kuokoa.
Simba ilianza na kikosi chenye wachezaji wengi wanaokosa nafasi kwenye mechi za Ligi Kuu Bara hatua ambayo licha ya kucheza vizuri ikakosa makali ya kutengeneza ushindi mkubwa.
Mapema kipindi cha kwanza kilichomalizika bila bao lolote, timu zote zilipoteza nafasi za wazi ambapo Simba dakika ya 38 ikashindwa kutumia shambulizi zuri mshambuliaji wake Mwangosi akashindwa kumalizia krosi ya David Kameta ‘Duchu’.
Mafunzo nayo dakika ya 40, mshambuliaji Fahad Hassan akashindwa kumalizia krosi ya beki Saleh Mbarouk, timu hizo zikienda mapumziko bila kufungana.
Dakika ya 85, Lebase Gueye aliyeingia dakika ya 65 kuchukua nafasi ya Bashir Kibaila, akashindwa kumalizia vyema nafasi nzuri kuipa Simba bao la pili, shuti lake linatoka nje kidogo.
Matokeo hayo yanaipeleka Simba nusu fainali ya michuano hiyo ikiifuata Mlandege ambayo mapema leo imeing’oa Singida Black Stars kwa mabao 2-1. Nusu fainali hiyo itachezwa Aprili 26, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Kwenye mchezo ambao Simba wameshinda na kufuzu nusu fainali, pia mashabiki wa timu hiyo wakafanikiwa kumuona kiungo mshambuliaji wao, Mkenya, Mohamed Bajaber ambaye alicheza kwa dakika 45 za pili akiingia kuchukua nafasi ya Ladack Chasambi.
Bajaber aliyekuwa akisumbuliwa na majeraha, mara ya mwisho kucheza mechi ilikuwa Januari 18, 2026 dhidi ya Mtibwa katika ligi ambapo alianza, akashindwa kumaliza baada ya kuumia.