AZAM FC imekuwa timu ya pili kukata tiketi ya kutinga hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la Muungano ikiifuata Yanga, lakini kocha wa kikosi hicho chenye maskani yake Chamazi jijini Dar es Salaam, Florent Ibenge amewachimba mkwara mabingwa hao watetezi wa taji hilo.
Alichokisema Ibenge ni, kikosi chake hakina shida ya kwenda kukutana na Yanga kwenye mchezo wa nusu fainali ya kwanza itakayopigwa Aprili 25, 2026 akisema hizo ndiyo mechi wanazozitaka.
Ibenge ameongeza, Azam inapenda kucheza mechi ngumu kama zile dhidi ya Yanga na watakwenda kujiandaa kukupambana na bingwa mtetezi wa mashindano hayo.
Amesema Azam imeiondoa timu bora ya ligi ya Zanzibar, KVZ kwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa robo fainali na sasa wanakwenda kukutana na timu bora kwenye Ligi Kuu Bara ambayo ni Yanga.
“Ni kweli tunakwenda kukutana na Yanga, utakuwa mchezo mgumu lakini sisi Azam hizo ndio mechi ambazo wakati wote tunapenda kuzicheza, tutajiandaa sawasawa kukutana nao,” amesema Ibenge.
“Mechi za namna hii zinakuimarisha na kujua ubora wa timu yako, tumetoka kuitoa timu bora ya hapa Zanzibar, haikuwa rahisi lakini tutakwenda kukutana tena na timu bora ya Ligi ya Bara.”
Msimu huu Azam imeshakutana mara mbili na Yanga na mara ya kwanza ilikuwa kwenye Fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 na Yanga ikashinda kwa matuta baada ya mechi hiyo kumalizika suluhu ndani ya dakika 120.
Mchezo wa pili ulikuwa kwenye Ligi Kuu Bara ambapo timu hizo zilimaliza kwa suluhu ndani ya dakika 90 na sasa zitakwenda kuutana kwenye mchezo wa tatu msimu huu Aprili 25 kwenye nusu fainali ya Kombe la Muungano.
Timu hizo mbili zitamalizana msimu huu kwenye mechi ya mzunguko wa pili wa ligi itakayochezwa Juni 24 na Yanga itakuwa mwenyeji ikiwa ni mchezo wa nne ndani ya msimu mmoja.
Azam juzi wakati inacheza dhidi ya KVZ, makocha wanne wasaidizi wa Yanga walikuwa jukwaani wakiusoma mchezo huo huku wakionyesha hesabu zao kubwa zilikuwa kwa matajiri hao wa Chamazi.