
Kupitia taarifa iliyotolewa leo, jijini Paris, Ufaransa, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Khaled El-Enany, amesisitiza kufanyika uchunguzi wa kina.
“Ninalaani mauaji ya Amal Khalil na kutoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa kina. Waandishi wa habari wana jukumu muhimu katika kuhakikisha mtiririko wa habari ambao ni muhimu kwa ujenzi wa amani katika hali za migogoro,” amesema Bw. El-Enany, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO.
Ameeleza kuwa ulinzi wa waandishi wa habari ni jambo la msingi kwa pande zote zinazohusika kwenye mzozo unaoendelea ukanda wa Mashariki ya Kati, “Natoa wito wa kuheshimiwa kwa Azimio namba 2222 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopitishwa kwa kauli moja mwaka 2015 kuhusu ulinzi wa waandishi wa habari, wataalamu wa vyombo vya habari na wafanyakazi wanaohusika kama raia katika hali za migogoro, hadhi ambayo imesisitizwa tena katika Mkataba wa Baadaye (Pact for the Future).”
Alipokea vitisho kabla ya kifo
Bi. Amal Khalil amekuwa akifanya kazi kama ripota wa gazeti la ndani la Lebanon liitwalo Al-Akhbar. Imeelezwa kuwa ameuawa akiwa safarini kikazi kwenda kuripoti matukio katika mji wa Bint Jbeil, baada ya nyumba aliyokuwa ameingia kupata hifadhi dhidi ya mashambulizi huko Al Tayri, kupigwa na kombora la shambulio la anga. Mnamo Septemba 2024, Amal Khalil anaripotiwa kupokea vitisho vya kuuawa vilivyohusiana na kazi yake.
Shirika la UNESCO linahamasisha usalama wa waandishi wa habari kupitia uelimishaji wa kidunia, kujenga uwezo, na kwa kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Utekelezaji wa Umoja wa Mataifa (UN Plan of Action) kuhusu Usalama wa Waandishi wa Habari na suala la kupuuzwa na kutokujali.