Dar es Salaam. Siyo jambo baya mtu kupambania anachokipenda. Yaani ni sawa na zile simulizi za washikaji ambao hutembea kwa miguu zaidi ya kilomita kumi kumfuata binti.

Mfano huu naufananisha na alichokifanya mwanamuzi wa nyimbo za asili, Saida Karoli ambaye amevuka zaidi ya mikoa zaidi ya mitano kufika Dar es Salaam kupambana na muziki ambao ulilitambulisha jina lake kwa ukubwa hapo awali.

Saida mwanamama ambaye sauti yake ina ujao wa kutosha na kuvutia. Huku akiwa na nyimbo zinazoishi kama ile ‘Maria Salome’ ameliambia Mwananchi amerudi rasmi Dar es Salaam kupambania jina lake.

 “Ukweli nimekaa kimya muda mrefu kwenye vyombo vya habari nina miaka saba sasa. Nimeona niuvunje ukimya nitoke na kibao kipya cha ‘Nakubembeleza’. 

“Kilichofanya niwe kimya ni kifo cha Ruge  nikapata changamoto, nikarudi kijijini nyumbani. Ikawa  ngumu hata vyombo vya habari kunipata vilevile suala la pesa, ukikaa Dar es Salaam mji wetu unataka uwe na hela changamoto zilikuwa hizo,” alisema.

Msanii huyu ambaye ameachia wimbo mpya ‘Nakubembeleza’ ambao umetazamwa zaidi ya mara elfu moja kwenye mtandao wa YouTube ameongezea kuwa hatarajii kuacha kuimba muziki wa asili.

“Muziki wa asili ndio ulionitoa. Na asili hiyohiyo ndiyo inaendelea kunibeba na kuwa mahili kwenye tasnia ya muziki wa Tanzania. Siwezi kuiacha Tanzania yangu mimi ndiyo nimeibeba kwa wasanii wanaoimba nyimbo za asili,” anasema 

Akizungumzia wasanii wa kizazi kipya kufanya muziki wa asili anasema wengi wao wanaona hauna pesa.
“Wasanii wa sasa wanaona nyimbo za asili hazina maisha. Hizi nyimbo wanazozifanya wao wanalipwa hela nyingi na hata ukiangalia maisha yao ni mazuri sio kama mimi. Hawawezi kutamani asili ninazofanya mimi.

“Malipo yangu yanakuja polepole licha ya kuwa nyimbo zinakaa sana kwenye ulingo hazishuki haraka zinazidi kuhiti kila siku lakini hazina  hela. Lakini kwa sasa vijana wanaangalia pesa,” anasema.

Atabanana hapahapa

Lengo lake kubwa ni kurudisha himaya yake kama ilivyokuwa miaka ya 2000, hivyo anasema amejipanga kubanana na vijana ambao kwa sasa ndio wametawala gemu.

“Vijana ni wengi wanaofanya muziki ni kitu ambacho hakipingiki, kwa hiyo tutapambana na sisi kadri ya uwezo wetu  tufanane na wao,” anasema Saida.

Aidha Saida kwa sasa hafikirii kuondoka kwenye jiji la Chalamila.
“Dar kuondoka labda itokee dharura tena. Lakani sina meneja, wala promota ambaye atanizuia kukaa. Ninachohitaji ni Watanzania waniunge mkono, hata wasanii wenzangu na serikali kama wapo tayari kuniunga mkono.

“Kwa sasa nimepanga nyumba. Mtaa wangu ni wa kiswahili sana nimejificha ndani ndani  maeneo ya Magomeni ndiyo ninapokaa nimechukua nyumba miezi sita,” anasema.

Hata hivyo mama huyu anaeleza kuwa anatamani tangu awali angekuwa anajisimamia mwenyewe kwenye muziki wake.
“Kitu ambacho nakijutia natamani kama tangu mwanzoni ningekuwa najisimamia bila promota. Kwasababu sasahivi nina nyumba  mbili kumbwa siyo vibanda. Moja ipo Mwanza na nyingine Bukoba.

“Dar sina nyumba ndiyo maana naishi kwa kuhangaika. Kipindi kile nina mameneja sikujenga hata banda.  Hii ni nguvu yangu ambayo nimepambana mimi mwenyewe natamani tangu zamani ningekuwa  najisimamia,” anasema. 

Ameeleza kuwa nyumba zake za mikoani wapo watu aliowaacha ikiwemo familia yake.

“Dar ndiyo sehemu ya kutobolea ndiyo maana napaamini. Kipindi nakuja sikuwa Saida Karoli  jina limekulia hapa nimekuja kutetea jina langu nione kama litarudi. 

“Watoto wangu ndio wananisisitiza wananiambia sauti yangu nzuri ila kwa kukaa kijijini hata nilie kiasi gani, kilio changu hakiwezi kufika popote. Wameniambia nirudi Dar ndiyo vyombo vya habari vilipo sina kazi nyingine muziki ndiyo maisha yangu,” anaeleza.

Saida anasema yeye ni mama wa watoto sita ujauzito wa kwanza aliupata akiwa na umri wa miaka 13. Hivyo katika hatua za ukuaji akajikuta anapata watoto 6 kila mmoja na baba yake.

Aliingia mkenge kisa Diamond

Anasema wakati mwanamuziki Diamond anatoa wimbo ‘Salome’ miaka tisa iliyopita kuna watu walimshawishi amshtaki msanii huyo kwa kuchukua baadhi ya vionjo kutoka kwenye wimbo wake ‘Maria Salome’

“Wakati Diamond anatoa Salome kuna watu walinipigia simu nikiwa kijijini wakasema kuna dili la haraka nikawaambia sina nauli. Wakasema niweke kitu sehemu nipate nauli.

“Nikauza gari yangu kwa laki tatu. Akatokea dalali mmoja nikampa na kadi wakanipa hela   nilivyofika kijijini nikakuta wanasheria  wakaniambia nimshtaki Diamond pamoja na boss wangu wanilipe nikawaambia mimi nilishalipwa zamani,” anasema.

Nakubembeleza 

Akieleza kuhusiana na kazi yake mpya  anasema ni maalum kwa ajili ya wapendanao.

“Nakubembeleza nimeimba na mtoto wangu anaitwa Maria Rosa yeye akabeba kipande cha mpenzi na mimi nikabeba kipande cha  mwanamke,” anasema.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *