MABOSI wa ZED FC ya Misri, wanafuatilia uwezekano wa kumsajili nyota wa JKT Tanzania, Paul Peter Kasunda, kwa ajili ya msimu ujao, licha ya mshambuliaji huyo mkataba wake kikosini hapo unatarajiwa kumalizika 2027.

Taarifa kutoka Misri na watu wa karibu wa mshambuliaji huyo, zinaeleza ni kweli uongozi wa ZED FC unafuatilia maendeleo yake ili kuipata saini yake msimu ujao, licha ya kutokuwa na makubaliano yoyote yaliyofikiwa kati ya pande zote mbili.

“Msimu huu ukiisha anabakisha mkataba wa mwaka mmoja zaidi na JKT Tanzania, hivyo kwa kifupi bado ni mchezaji wao halali kikosini, ni mapema sana kuzungumzia jambo hilo ila, kama litakuwepo tutapeana taarifa kamili,” kimesema chanzo hicho.

Chanzo hicho kimesema mchezaji kuhitajika na timu za nje ni jambo nzuri kwake mwenyewe na kwa manufaa ya timu ya taifa kiujumla, ingawa kuhusiana na hilo hakuna makubaliano yoyote na kinachoendelea kwa sasa ni taarifa tu za mitandaoni.

“Mchezaji mwenyewe aliomba menejimenti yake kama kuna suala lolote la usajili asihusishwe kwa sasa hadi pale msimu huu utakapoisha, lengo ni kuweka akili yake yote JKT Tanzania katika mechi zilizobaki,” kimesema chanzo hicho.

Mshambuliaji huyo aliyeanzia timu ya vijana ya Azam chini ya miaka 20, hadi kupandishwa kuchezea ya wakubwa, amekuwa ni muhimili mkubwa kwa kikosi cha JKT Tanzania msimu huu, akishirikiana na nyota, Valentino Mashaka na Salehe Karabaka.

Nyota huyo aliyepandishwa kuichezea Azam na aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Mromania Aristica Cioaba, amechezea pia timu mbalimbali zikiwemo Mugabe FC, KMC FC, Tanzania Prisons na msimu uliopita alikuwa Dodoma Jiji.

Nyota huyo alijiunga na JKT, Julai 9, 2025, akitokea Dodoma Jiji, baada ya msimu wa 2024-2025, kufunga mabao manane ya Ligi Kuu, akiwa nafasi ya pili kwa wachezaji wazawa waliofunga mabao mengi, nyuma ya Clement Mzize wa Yanga aliyefunga 14.

Msimu huu wa 2025-2026 akiwa na JKT Tanzania, ameifungia mabao matano ya Ligi Kuu na matano ya Kombe la CRDB, huku ofa hiyo ya ZED FC ni ya pili kwake kutoka timu za Uarabuni, baada ya Januari 2025, kuhitajika pia na Al Dahra Tripoli FC ya Libya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *