
OFISA Michezo Wilaya ya Chakechake iliyopo Mkoa wa Kusini Pemba, Issa Adam Hamza, amewataka wananchi kuvitumia viwanja vinavyojengwa kwa kufuata utaratibu uliowekwa.
Ameyasema hayo, wakati akizungumza na Mwanaspoti ofisini kwake kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba, huku akibainisha kwamba, viwanja vinavyojengwa vipo kwa ajili ya wananchi, hivyo wavitumie kwa lengo la kuibua vipaji vya vijana.
Pia, amesema Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar inaisisitiza jamii kuvitunza viwanja, hivyo na kutoa hamasa kwa vijana kuchangamkia fursa hiyo kwa kuonesha vipaji vyao ili kujiajiri.
“Viwanja hivi vinajengwa kwa ajili ya wananchi kwa maana hiyo wanapaswa kuitunza miundombinu hiyo na wasiharibu,” amesema.
Sambamba na hilo, amewasihi vijana kuchangamkia michezo ambayo haina wachezaji wengi na kuomba nafasi za kuwa wasimamizi wa viwanja hivyo.
Amesema, licha ya hayo yote, bado hamasa ipo kwa wananchi kwani kila mmoja anatamani kucheza kwenye viwanja vilivyojengwa.
Kwa mujibu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuna viwanja 17 vinajengwa katika visiwa vya Unguja na Pemba ambapo upande wa Pemba, vipo sita. Viwanja hivyo vinajengwa vitatu kila mkoa huku kisiwa hicho kikiwa na mikoa miwili, Pemba Kaskazini na Pemba Kusini.