KIUNGO mshambuliaji wa Kitanzania anayekipiga Fouad FC inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Misri, Oscar Evalisto amesema tangu alipojiunga na timu hiyo dirisha dogo la usajili, amekutana na ushindani mkubwa wa namba.
Evalisto aliyetua Fouad akitokea Makadi FC, amesema mazingira ya timu mpya ni tofauti na alikotoka, jambo linalomlazimu kupambana zaidi ili kupata nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza.
“Unajua nilibadili timu dirisha dogo, hivyo hii timu niliyokuja changamoto ni kubwa kidogo. Ushindani wa namba umekuwa mgumu zaidi tofauti na nilikotoka,” amesema Evalisto na kuongeza;
“Tangu nimefika hapa sijabahatika kuanza kikosi cha kwanza, nimekuwa nikitokea nje, lakini kiukweli hii timu ina wachezaji wengi wenye ubora wa ligi kuu kabisa,” ameongeza.
Licha ya changamoto hiyo, kiungo huyo amesema anaendelea kupambana na tayari amefunga mabao matatu na kutoa pasi moja ya bao.
Kabla ya kusajiliwa Fouad, Evalisto aliitumikia Makadi FC msimu mmoja na alifunga mabao matano na kutoa asisti nne na kutokana na kuonyesha kiwango kizuri, ndipo akapata nafasi ya kusajiliwa na timu hiyo.