Dar es Salaam. Taifa lililojizolea umaarufu duniani kwa kukomesha ubaguzi kwa vitendo, Afrika Kusini, sasa linakabiliwa na hali mpya ya sintofahamu inayofanana kwa mbali na historia yake ya enzi za ‘giza’.

Ripoti za vyombo vya habari kutoka nchini humo zinaonesha kuibuka tena kwa mashambulizi dhidi ya raia wa kigeni, yakichochewa na chuki, hofu na propaganda za kijamii.

Deutsche Welle (DW) inaripoti, serikali ya nchi hiyo imeahidi kuwasaka na kuwachukulia hatua wote wanaohusika na vitendo vya kuwashambulia wahamiaji, ikitaja hali hiyo kuwa tishio kwa utawala wa sheria na utulivu wa taifa.

Hata hivyo, tofauti na mifumo mingine, historia ya Afrika Kusini inaifanya hali ya sasa kuwa na uzito wa kipekee zaidi kisiasa na kihistoria.

Mbegu iliyopandikizwa na makaburu, ambao utawala wao ulikuwa wa kibaguzi wa wazi na wa kikatili kupitia mfumo wa Apartheid, iliacha majeraha makubwa ndani ya jamii.

Baadaye, kiongozi muasisi wa taifa hilo, Nelson Mandela, alijizolea umaarufu kwa kuhubiri maridhiano na kujenga taifa lisilo na ubaguzi.

Kauli za haki, utu na usawa zilitamalaki katika kinywa cha mwanamajumui huyo wa Afrika, Rais wa kwanza mweusi wa taifa hilo kubwa la kusini mwa Afrika.

“Hakuna anayezaliwa akimchukia mwenzake kwa sababu ya rangi yake au asili yake,” alisema Mandela katika moja ya nukuu zake maarufu akikosoa ubaguzi hadharani.

Leo, hata hivyo, taifa hilo linaonekana kurejea katika kivuli cha chuki, safari hii ikiwalenga Waafrika wenzao.

Sasa taifa hilo linaanza kupoteza heshima yake hiyo kufuatia ongezeko la mashambulizi dhidi ya wageni, jambo linalozua taharuki na sintofahamu kwa mataifa mengi yakiwemo Ghana, ambayo tayari yameonesha wasiwasi mkubwa.

Kwa mujibu wa DW, hivi karibuni Ghana ilimwita Balozi wa Afrika Kusini nchini humo ili kuelezea malalamiko kutokana na kushambuliwa kwa raia wake katika jimbo la KwaZulu-Natal, ambako raia mmoja alishambuliwa na kulazimishwa kuonesha nyaraka zake kabla ya kutakiwa aondoke nchini humo.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afrika Kusini inaripotiwa imekiri kufanyika kwa vitendo hivyo ikilaani kuwa vinahatarisha misingi ya utawala wa sheria na vinaweza kuchochea visasi kutoka mataifa mengine.

Wadau na raia wanaoshiriki maoni yao katika mitandao ya kijamii kwenye kurasa zinazosambaza taarifa hizo wanaonya kuwa athari za hali hii zinaweza kuwa pana zaidi ya inavyoonekana kwa sasa.

Kwanza, katika biashara, wafanyabiashara wa kigeni wanaowekeza katika taifa hilo wanaweza kuingiwa hali ya tahadhari au kuondoka kabisa, hali inayoweza kudhoofisha uchumi wa ndani.

Aidha, katika diplomasia ya bara la Afrika, hali hii inavuruga mshikamano wa Umoja wa Afrika ambao msingi wake ni umoja na ushirikiano wa Waafrika.

“Wanachofanya Waafrika Kusini wanaweza kusababisha raia wa nchi hiyo waanze kufanyiwa hivyo hivyo katika mataifa waliyopo,” wameandika baadhi ya watoa maoni mitandaoni.

Pia wanatahadharisha kuwa taswira ya Afrika Kusini kimataifa inaendelea kuchafuliwa, kutoka kuwa mfano wa mafanikio ya kupambana na ubaguzi hadi kuwa kitovu cha migogoro ya kijamii ikihusisha unyanyasaji wa raia wa kigeni.

Hali hii inaendelea kuimarika baada ya kusambaa video ikimuonesha raia aliyedaiwa kuwa ni Mtanzania, Jumamosi Aprili 25, 2026, akishambuliwa katika moja ya mji nchini humo, siku moja baada ya kusambaa video nyingine ikimuonesha raia anayeonekana kuwa wa bara la Ulaya, akijihami na kupambana na wenyeji waliokuwa wakimshambulia.

Kwa ujumla, kinachoendelea sasa si tu tishio la matukio ya uhalifu kwa wageni, bali ni ishara ya changamoto ya kijamii na kisiasa.

Swali linalobaki ni je, Afrika Kusini itasimama imara kulinda misingi yake ya haki na usawa iliyojengwa kwa gharama kubwa, au historia ya ukaburu itarejea kwa sura mpya isiyotangazwa rasmi lakini yenye madhara yale yale.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *