Njombe. Maonyesho ya Wiki ya Usalama Pahala pa Kazi (Osha), yanayofanyika mkoani Njombe, yameujaza mji huo hadi wakazi wake kulazimika kuhama nyumba zao na kuzikodisha kwa wageni.

Hilo limethibitishwa leo na Jumatatu Aprili 27, 2026 na Mkuu wa Mkoa, Antony Mtaka alipokuwa akifungua maonyesho hayo yanayofanyika viwanja vya Mji Mwema mkoani humo.

Maonyesho hayo yameanza Aprili 24, 2026 na yanatarajiwa kufika kilele kesho licha ya kuwa washiriki wengi watasalia hapo hadi kilele cha Mei Mosi.

Kwa mujibu wa Mtaka, wageni waliohudhuria maonyesho hayo ni zaidi ya 5,000, huku nyumba za kulala wageni katika mkoa hazizidi vyumba 1800.

“Osha inaweza kuona maonyesho haya ni jambo dogo imelifanya lakini niwahakikishie ni kubwa kwani wapo watu wamefanya biashara ya kukodisha nyumba zao kutokana na hoteli kujaa.

Mabanda mbalimbali yakiwa yamepangwa katika viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema, ambako maonesho ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) yanaendelea kufanyika.

“Pia wapo waliokosa nyumba za kulala, wameenda kulala Makambako na kila siku wanaenda na kurudi hapa hili sio jambo dogo lina maslahi kwa wananchi wetu ambapo wameweza kuuza huduma na bidhaa mbalimbali,” amesema.

Hata hivyo, Mtaka amesema kutokana na fursa hizo, yeye ni miongoni mwa waliowashawishi watu kupangisha nyumba zao na kati ya hao wapo wanaolipwa hadi Sh150,000 kwa siku.

Mtaka amesema katika maonyesho hayo zaidi ya kampuni na taasisi 150 zimeshiriki ikiwa ni ongezeko kutoka washiriki 70 walioshiriki mwaka jana wakati maonyesho hayo yalipofanyika mkoani Singida.

“Mwaka huu tumepanga kufanya matukio sita ambapo mwaka jana tulikuwa na watunza kumbukumbu ambapo bajaji zilifanya kazi nyama ziliuzwa, mboga ziliuzwa hivyo ndio tunataka mji wetu uwe.

“Na sisi tushasema huu ni mkoa wa uchumi na biashara, kwa hiyo tunaomba kila mwenye mkutano aje Njombe kwa kuwa kuna hali nzuri ya hewa ataachana na AC za huko mjini,” amesema Mtaka.

Baadhi ya wananchi waliopangisha nyumba zao, Winfrida Moses, amesema baada ya kupiga hesabu ya kupata hela ndefu akipangisha nyumba yake, aliamua kwenda kukaa kwa ndugu zake.

Winfrida amesema nyumba yake ameikodi kwa moja ya taasisi ambayo kwa siku inamlipa Sh200,000 na wameichukua kwa siku saba, hela ambayo hakutarajia kuipata katika kipindi hiki.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda, akizungumza na wajasiriamali pamoja na waendesha bodaboda mkoani Njombe waliohudhuria mafunzo yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema, Halmashauri ya Mji wa Njombe.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Usalama na afya Mahala pa Kazi (Osha), Khadija Mwenda, amesema maonyesho hayo yameanza kufanyika tangu mwaka 2004 malengo yakiwa ni kutoa elimu na ushauri kwa wafanyakazi na wananchi kwa jumla kuhusiana na masuala ya usalama na afya mahala pa kazi.

Khadija amesema kaulimbiu ya maonyesho hayo kwa mwaka huu ni ‘Mazingira bora ya kisaikolojia na kijamii kazini ni njia ya kuimarisha ustawi wa wafanyakazi na kuje nga taasisi imara.’

Walichosema wananchi

Julius Mwangonga, amesema ujio wa maonyesho hayo ni faraja kwao na kueleza kuwa alikuwa amejenga vyumba vinne nje ya nyumba anayoishi kwa ajili ya kuzipangisha na alikuwa amebakiza sehemu ndogo kumalizia.

Hata hivyo, baada ya kusikia fursa hiyo ya ugeni wa watu wa maonyesho, alikwenda kukopa hela mahali akamalizia haraka na zote nne zimepata wapangaji na kila moja akiipangisha kwa Sh50,000.

Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa maonyesho, Naomi Michael, amesema amelazimika kulala kwenye gari baada ya kukosa nyumba, ila kuna wenyeji wanamfanyia mpango wa kupata nyumba ya mtu leo.

Huku waliipata nyumba, wameshauri uongozi wa mkoa wawe wanazitambua ili kuhakikisha kunakuwa na usalama lakini uzingatiaji wa usafi unafuatwa.

Mmoja wa wasimamizi wa hoteli ambaye hakutaka jina lake liandikwe, amesema hoteli yake ilishajaa wiki mbili zilizopita.

Hata hivyo, amesema kuna cha kujifunza kwa wakazi wa Njombe kuwekeza pia katika ujenzi wa nyumba za kulala wageni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *