Vyombo vya habari vya Marekani vimetangaza kuwa, mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 31 aitwaye Cole Thomas Allen, ambaye alikuwa amedhamiria kuwashambulia kwa bunduki viongozi wakuu wa Marekani, amejeruhiwa na kutiwa nguvuni. Kwa mara nyingine tena, Marekani imeshuhudia tukio la ufyatuaji risasi kwenye hadhara ya viongozi wake wakuu akiwemo rais wake Donald Trump; mara hii ikiwa ni katika mkutano wa kila mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari wa Ikulu ya nchi hiyo, White House.
Katika mkutano huo uliofanyika kwenye Hoteli ya Hilton jijini Washington DC, mtu mmoja mwenye silaha alijaribu kuuvuka uzio wa maafisa wa usalama ili kufika kwenye ukumbi walikokaa wageni waalikwa; na kwa mujibu wa vyombo vya habari, lengo lake lilikuwa ni kuwafyatulia risasi viongozi wakuu wa Marekani.
Rais, makamu wake, mawaziri na baadhi ya wabunge, pamoja na waandishi wa habari mashuhuri wa Marekani, walikuwa miongoni mwa wageni waliohudhuria hafla hiyo ya dhifa ya chakula cha usiku. Tukio hilo ambalo lilipelekea kukatizwa hafla hiyo iliyohudhuriwa na Trump limeakisiwa mno na kwa hisia na mitazamo tofauti ndani na nje ya Marekani. Kama ilivyotarajiwa, baada ya tukio hilo, Trump alijitokeza hadharani na kujaribu kujionyesha kuwa ni shujaa mpambanaji aliyejipanga kimapambano na kutaka kuwaaminisha wafuasi wake kwamba, alikabiliwa na jaribio la kutaka kumuua kwa sababu ya hatua anazochukua.
Imesalia takribani miezi sita kabla ya kufanyika uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani, na inatabiriwa kuwa washirika wa Trump katika chama cha Republican watabwagwa na wagombea wa chama cha Democratic katika kinyang’anyiro hicho. Kwa sababu hiyo, baadhi ya watu ndani ya Marekani wamedokeza kuwa, tukio lililojiri Jumamosi usiku katika Hoteli ya Hilton huko Washington DC ni hila tu iliyopangwa na wafuasi wa Trump ili kuathiri matokeo ya uchaguzi ujao au kutoa fursa nyingine kwa wafuasi wa Trump ya kulitumia vibaya na kwa maslahi yao tukio hilo kuweza kuibuka washindi katika uchaguzi huo. Watu hao wanaashiria jaribio lililofeli la kumuua Trump lililotokea katikati ya kampeni za uchaguzi wa urais wa Marekani wa mwaka 2024 huko Pennsylvania, ambapo mgombea huyo wa Republican alijeruhiwa kidogo.

Picha ya Trump katika tukio hilo ilienezwa mno na vyombo vya habari na ikawa na taathira kubwa kwa yeye kuchaguliwa tena kuwa rais. Bila shaka, Marekani ina utamaduni wa tangu na tangu wa kuua marais wake, ambapo kati ya marais 47, wanne kati yao wameuawa kwa kupigwa risasi. Na hii ni katika hali ambayo, kuna uhuru wa kubeba silaha moto ndani ya nchi hiyo, na watu binafsi wanaweza kwa urahisi kupata na kumiliki kisheria silaha hizo na kuweza kuzitumia kuulia raia wenzao wakiwemo hata viongozi wa juu wa nchi. Sambamba na hayo, hutokezea marais wa Marekani, viongozi wengine waandamizi pamoja na wanasiasa wa nchi hiyo kuchukiza mbele ya umma kwa hatua na matendo yao na kuandamwa na visasi vya kisiasa vya maadui zao.
Wakati huo huo, kama haitakuwa sahihi kusema kwamba, chuki na manung’uniko waliyonayo Wamarekani kwa Trump kutokana na baadhi ya hatua na vitendo vyake vya kutatanisha anavyofanya yamefikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa, basi kwa uchache, ni za kiwango nadra kuwahi kuonekana zikionyeshwa dhidi ya rais wa nchi hiyo. Kwa sababu hiyo, kumekuwepo na majaribio kadhaa ya kumuua Trump, iwe ni wakati wa urais wake au kabla yake, hali inayoashiria pia udhaifu wa vyombo vya kiintelijensia na kiusalama vya Marekani katika kumlinda rais na viongozi wengine wakuu wa nchi hiyo.
Bila shaka, uchunguzi utakaofuatia utabainisha mhusika au wahusika wa shambulio la ufyatuaji risasi kwenye mkutano wa chama cha waandishi wa habari uliofanyika kwenye Hoteli ya Hilton mjini Washington, DC walifanya hivyo kwa lengo na madhumuni gani.
Pamoja na hayo, ni jambo la kutarajiwa, kwamba viongozi wa serikali ya Marekani, vyama na mirengo ya kisiasa nchini humo watalitumia tukio hilo kwa manufaa yao ya kisiasa; jambo ambalo Trump mwenyewe ana utaalamu nalo maalumu, ambao ni wa kuweza kwa wakati mmoja kulitumia kwa manufaa ya wafuasi wake na dhidi ya wapinzani wake. Lakini si hasha pia, jaribio hilo la mauaji likawa limefanywa kwa lengo la kuupumbaza na kuubabaisha umma wa Wamarekani ili uache kufuatilia matatizo na mazonge mbalimbali yaliyoitanza serikali ya Trump, kuanzia kadhia ya nyaraka za Epstein hadi matatizo ya kimaisha waliyonayo wananchi, sera za njezilizovurugika na vita visivyo na mwisho inavyopigana nchi hiyo nje ya mipaka yake…/