
JAPOKUWA Singida Black Stars iliondolewa na Mlandege kwa kufungwa mabao 2-1 katika michuano ya Kombe la Muungano hatua ya robo fainali, lakini kocha wa timu hiyo, Muhibu Kanu amesema walitoka na kitu muhimu kwao, ambacho wanakifanyia kazi kwa sasa.
Kanu amesema ingawa michuano hiyo ni ya mtoano iliyolazimu Singida Black Stars kucheza mechi moja pekee, lakini iliwasaidia ni namna gani wachezaji ambao walikuwa hawapati nafasi, walipocheza wamegundua ni kitu gani kinapaswa kuongezwa kwao.
“Hilo kwa sasa tunalifanyia kazi katika mazoezi ya kujiandaa na mechi dhidi ya Coastal Union ambayo tutacheza nayo Tanga, Mei 2,” amesema Kanu na kuongeza:
“Kuna wachezaji wanatakiwa mazoezi ya fitinesi kutokana na kutocheza muda mrefu, wengine kujengewa kujiamini ili kurejea katika ari ya kazi.”
Amesema nguvu yao kubwa kwa sasa ni kuhakikisha wanashinda mechi zilizopo mbele yao, zitakazowasaidia kufikia malengo ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) msimu ujao.
“Tunatambua mechi za mzunguko wa pili zinakuwa ngumu, kila timu inakuwa inapambania malengo yake, kwa upande wetu haijalishi tulitolewa Muungano Cup mapema, hilo haliwezi kuyumbisha malengo yetu ya Ligi Kuu,” amesema